Trafiki 10 matatani madai ya wizi wa kimfumo

Dar es Salaam. Wizi kwa njia ya mifumo unaendelea kuota mizizi serikalini, safari hii ukiwahusisha baadhi ya askari wa usalama barabarani.

Kutokana na hilo, wanazuoni wameeleza namna unavyofanyika wakipendekeza mbinu za kuudhibiti.

Katika Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani, zaidi ya askari 10 kutoka mikoa ya Iringa, Pwani na Kilimanjaro wanadaiwa kuingia matatani kwa wizi huo.

Kwa mujibu wa taarifa ambazo Mwananchi imezipata, askari hao wamechepusha fedha zinazopaswa kuingia kwenye mfumo wa Serikali kwa kutengeneza mfumo  wao binafsi kupitisha fedha hizo.

Alipotafutwa jana, Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime amesema bado hajapokea taarifa akiahidi kufuatilia kujua ukweli wake.

“Taarifa za aina hiyo ndiyo nazisikia kutoka kwako, ngoja nifuatilie kuona kama kuna taarifa za namna hiyo,” amejibu.

Misime alipotafutwa jana amesema majibu aliyoyatoa jana ndiyo hayo hayo.

“Jibu ni lilelile la jana (anaendelea kufuatilia usahihi wa taarifa)” amesema Misime.

Rais Samia na wizi wa mifumo

Wizi kwa njia ya mifumo uliwahi kuzungumzwa Agosti 17, 2023 na Rais Samia Suluhu Hassan,  akieleza  baadhi ya halmashauri mkoani Mbeya, zimeunda mfumo nje ya unaotumiwa na Serikali kukusanya fedha.

“Nilikuwa Mbeya hivi karibuni kwenye Nanenane, nikakuta kadhia pale maofisa kabisa wa halmashauri wametengeneza mtandao wao mbali na ule unaokusanya fedha za Serikali, kiuhalisia kuna mwingine wa pembeni na umekusanya fedha nyingi sana,” alisema.

“Baada ya wao kufanikiwa wakawapa jirani zao, nilikuwa nasubiri ripoti kutoka Tamisemi, lakini hajaleta bado na mimi nalijua na naendelea kufuatilia kwa njia zangu, sasa hiyo ripoti ije ikiwa diluted (imechakachuliwa)” alisema.

Mbali ya Rais Samia, wizi kwa njia hiyo uliibuliwa na Mwenyekiti wa Chama cha Mawakala wa Utalii jijini Arusha, Wilbard Chambulo.

Katika kikao cha Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda na wadau wa utalii, Chambulo aliibua tuhuma dhidi ya Halmashauri ya Jiji la Arusha kumpa fomu ya malipo yenye taarifa tofauti na za kampuni yake.

Pia, amedai kutozwa ushuru wa Sh24 milioni, lakini risiti aliyopewa iliandikwa amelipa Sh3.6 milioni.

Katika wizi huo inadaiwa askari hao wanatumia mashine binafsi za POS (Point of Sale) na fedha wanazokusanya haziingii serikalini moja kwa moja bali zinaenda kwenye mifuko yao.

Kwa mujibu wa wataalamu wa mifumo ya kompyuta, wizi huo unafanyika kwa kuingilia mfumo wa malipo wa Serikali, jambo linalowezeshwa na mianya ya usalama katika mfumo huo.

Vyanzo vya habari kadhaa kutoka mikoa hiyo na ndani ya Jeshi la Polisi, vimelidokeza Mwananchi kuwa mkoani Iringa, trafiki saba wanadaiwa kufukuzwa kazi ndani ya wiki mbili, huku Pwani na Kilimanjaro wakishtakiwa kijeshi.

“Kule Iringa ndiyo ilikuwa worse (mbaya zaidi) kwa sababu mnyororo wa upigaji unadaiwa kumhusisha ofisa mwenye cheo cha juu. Yeye taratibu zake ziko tofauti kidogo ila naye anachunguzwa,” kimedokeza chanzo kimojawapo.

Habari zilizolifikia gazeti hili zinaeleza waliofukuzwa kazi mkoani Iringa wanadaiwa kujihusisha na rushwa na kuchepusha fedha za Serikali zinazotokana na makosa ya usalama barabarani na kujinufaisha nazo binafsi zikiingia kwenye mifuko yao.

“Tunaambiwa askari wawili walibainika kuwa na ile mashine ya POS ya kwao binafsi, kwa hiyo wakikusanya fedha haziendi serikalini. Serikali inapaswa ichunguze matumizi ya mashine hizi. Kuna kitu hakiko sawa,” kimedai chanzo cha habari.

Ofisa wa Jeshi hilo mwenye cheo cha Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP), amesema baada ya trafiki hao kuhojiwa walimtaja bosi wao kuwa naye yupo katika mnyororo wa mradi huo wa mapato binafsi.

“Juzi juzi hapa tulikuwa na kikao na askari tukaambiwa wenzenu huko Iringa wamefukuzwa kazi kwa kucheza na mapato ya Serikali. Huko Pwani nako ni vivyo hivyo, kuna askari wako kwenye mashtaka ya kijeshi,” amedai ofisa huyo.

“Sina hakika sana kama mashtaka yao yamemalizika au vipi lakini kulikuwa na mashtaka yalikuwa yanaendelea kule Pwani na mchezo ni huohuo tu kama wa Iringa. Inaonekana kuna mchezo mchafu kwa baadhi ya trafiki,” amedai.

Taarifa kutoka mkoani Kilimanjaro zinadai trafiki wanne kutoka Wilaya ya Mwanga wamefunguliwa mashtaka ya kijeshi kwa madai ya kwenda kinyume na mwenendo mwema wa Jeshi hilo unaosisitiza uadilifu.

Taarifa zinadai wiki mbili au tatu zilizopita, trafiki hao waliitwa makao makuu ya mkoa kwa Kamanda wa Polisi, Simon Maigwa na kuhojiwa wakidaiwa kumiliki kadi binafsi (chip) waliyokuwa wakiiweka kwenye kamera za kubaini mwendo wa gari.

“Ni kweli kuna hilo jambo maana walihojiwa-hojiwa sana hapa mkoani tukaona wamevuliwa utrafiki wakawa askari wa kawaida lakini hivi sasa tumeambiwa wamefunguliwa mashtaka ya kijeshi wanaendelea nayo,” kimeeleza chanzo cha habari.

Imeelezwa na chanzo hicho kuwa, trafiki hao kwa miaka miwili inadaiwa walikuwa wakipiga picha magari yanayovunja sheria kwa kwenda mwendo kasi eneo lisiloruhusiwa, kisha kufanya mazungumzo na madereva na kuchukua fedha.

“Inaonekana wamefanya hili kwa muda mrefu. Wanaingiza chip yao wanarekodi magari wakishavuta ‘mpunga’  (fedha) wanafuta picha na wanaondoa ile chip kama vile magari hayakukamatwa kumbe ni mradi wao,” amedai ofisa wa jeshi hilo.

Ubadhirifu huo unadaiwa kubainika wakati ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG )kwa mwaka 2020/2021 ikibaini mashine 89 za POS zinazotumiwa na trafiki kutoza faini hazikuwahi kurekodi muamala wowote.

Katika ripoti hiyo, CAG alibaini kuwapo POS hizo ambazo zilisajiliwa na zilikuwapo hewani katika mfumo wa TMS, lakini hazikuwahi kurekodi muamala hata mmoja kwenye mfumo.

POS hizo zilisajiliwa kati ya Julai 2019 na Februari 2021.

Msomi wa mifumo ya kompyuta wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Fatuma Simba amesema wizi wa aina hiyo unawezekana kwa kuhamisha mfumo.

Ameeleza katika malipo ya mtandao kuna mfumo unaowezesha kupeleka fedha kwa mpokeaji aliyelengwa, usipokuwa na ulinzi mahiri, unaweza kuingiliwa na fedha kuhamishwa njia.

“Kwa vyovyote vile hao watu wameuchezea mfumo, ukiuchezea inakuwezesha kuhamisha kwa kadri unavyotaka,” ameeleza.

Ili kudhibiti hali hiyo kwa mujibu wa Dk Fatuma, kunahitajika ulinzi mahiri wa mfumo husika ili usitoe mwanya wa kuingiliwa na wadukuzi.

“Lazima kila mfumo uwe na ulinzi, hiyo itazuia wenye nia ovu kuuingilia na hatimaye kufanya ubadhirifu. Upo uwezekano wa kufanya hivyo,” amesema

Mtaalamu mwingine kutoka UDSM, Dk Jimmy Mbelwa amefafanua ni vigumu kuingilia mfumo hasa unaohusisha namna ya malipo.

Ameeleza mfumo wowote huwa na msimamizi ambaye aghalabu huuendesha, nje ya huyo hakuna atakayefanya lolote.

Dk Mbelwa ameeleza iwapo itaonekana mfumo, hasa wa malipo umeingiliwa kwa namna yoyote, yupo mtu wa ndani kati ya wanaohusika na mfumo amehusika.

“Siamini kwamba mtu anaweza kuingilia mfumo kwa sababu huwa na usimamizi. Uwezekano wa kuingilia mfumo, hasa wa malipo unatokea pale mtu wa ndani kati ya wasimamizi anapohusika,” ameeleza.

Dk Mbelwa amependekeza kuangaliwa kwa mianya kwenye mifumo hiyo ili izibwe kudhibiti uwezekano wa kuingiliwa.

Ni mnyororo, ngumu kugundua

Mtaalamu wa Ukaguzi wa Hesabu, Edison Leons amesema wizi huo mara nyingi huhusisha mnyororo wa watu wakiwamo wenye mamlaka makubwa.

Kinachofanyika amesema ni kutengenezwa mfumo nje ya ule rasmi kwa ajili ya kupitisha fedha, ambao mara nyingi ni vigumu kuugundua kwa sababu hufanana.

“Katika mfumo unaotengenezwa huwa unakuwa na taratibu kama mfumo rasmi, watatumia mashine za POS, utapewa namba ya kumbukumbu ya malipo na risiti ya malipo, lakini fedha zinakwenda kwingine, siyo serikalini,” amesema.

Namna pekee ya kudhibiti hilo, amesema ni kufuatilia mnyororo wa wahusika wa mfumo, kisha kuwakabili.

Leons ambaye ni mkufunzi wa taaluma ya uhasibu,  amesema nguvu kubwa inahitajika kukabiliana na hilo, kwa kuwa wanaotengeneza mifumo huwa ni watu wenye mamlaka.

Related Posts