Umewahi kuwasikia wapiga debe wa kukupeleka ‘gesti’

Mbeya. Wakati wapiga debe kwa baadhi ya mikoa wakiwa wanalalamikiwa  kuwabughudhi abiria katika vituo vikuu vya mabasi, hali ni tofauti mkoani  Mbeya kwani wamekuwa mkombozi kwa abiria wanaofika kituoni hapo.

Hii ni kutokana na mbali ya kupiga debe kwenye mabasi lakini pia wamekuwa msaada katika kuwatafutia wageni wanaofika mkoani hapo  nyumba za kulala wageni.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti vijana wanaofanya shughuli hiyo akiwemo Frank Khatibu, amesema ameanza kazi hiyo ya kupiga debe miaka sita iliyopita.

Katika kila mteja amesema inategemea analipia chumba cha kiasi gani, ambapo akilipa cha Sh15,000,  hupewa Sh5000 na kwa anayelipa chumba cha Sh10,000, anapata Sh2000.

Kuhusu namna wanavyopata wateja licha ya kuwepo wapiga debe wengi eneo hilo, amesema;

 “Dada ndio maana hata Kariakoo maduka ni mengi yanauza  bidhaa zinazofanana na kila mtu anauza, vivyo hivyo hata sisi kwetu wapiga debe hali ipo hivyo.’’

Kupitia kazi hiyo, anasema anaweza kuendesha maisha yake ikiwemo kulipa kodi na kumtumia hela ya matumizi  bibi yake aliyoko kijijini Sumbawanga ambaye ndio amemlea tangu akiwa mdogo  baada ya wazazi wake kufariki.

Naye Manase Maginga amesema, wakati mwingine katika kazi hiyo abiria wanaoshuka katika stendi hiyo,  ndio huuliza sehemu za kulala kama wanazijua na hivyo kuitumia kama fursa.

“Abiria akishauliza hivyo, tunachotaka kujua kutoka kwake ni chumba cha bei gani angehitaji na kiweje, na kwa kuwa hoteli zote zilizopo katika stendi hiyo tunazijua , huwa nampeleka moja kwa moja ambayo najua atairidhia kuilingana na vigezo alivyonipa,”amesema Maginha.

Hata hivyo,  Maginga anasema guest wanazofanyia udalali na kupewa   cha juu ni hizo zinazozunguka stendi kuu, ila za nje ya hapo hazina utaratibu huo labda tu abiria mwenyewe aamue kumpa asante ya kumpeleka kwa kuwa wakati huo pia unaweza ukawa pia umemsaidia kumbebea mizigo yake.

Jaziu Juma, mmoja wa viongozi wa wapiga debe stendi, amesema katika ufanyaji kazi huo,  huwa wakisimamiana ili kuhakikisha abiria habugudhiwi kwa namna yoyote ile na mpaka sasa wapo wapiga debe zaidi ya 300.

Mojawapo ya faini kwa atakayetenda kosa, Juma amesema  ni pamoja na kufungiwa asifikie stendi hapo au kutozwa faini ya Sh30,000 hasa kwa wale wanaovuta mabegi ya abiria au kuwatolea lugha chafu.

“Ikitokea umefanya kosa na likafika kwa uongozi, adhabu ni kusimamishwa kwa muda usifike stendi au kufukuzwa kabisa kama mhusika atakuwa anafanya makosa kwa kujirudia,”amesema Juma.

Ukiacha kukutana katika kazi, Juma amesema huwa wakisaidiana katika masuala ya kijamii ikiwemo mwenzao akiugua, kufiwa na baba, mama, mke au mtoto ambapo hupeana kishika mkono cha Sh500,000 na kuendelea.

Msimamizi wa nyumba ya  wageni, aliyejitambulisha kwa jina moja la Frank, amesema wapiga debe hao wanawasaidia ukizingatia eneo hilo lina guest nyingi, hivyo wasipojiongeza kwenda kuwatafuta wateja huko  stendi ambapo kila sekunde kuna mabasi yanashusha watu hapo, wanaweza wakashindwa kuendesha biashara hiyo.

Anasema kwa mpiga debe aliye makini kwa siku anaweza kuondoka hata na Sh20,000 kwa kazi hiyo na huwa wakiwapa chao hapo hapo baada ya mteja kulipa na hata kama mteja atasema atalipa asubuhi wenyewe huwapa hela yao kabisa.

Wakizungumzia hilo baadhi ya abiria akiwemo John Issack mkazi wa mkoa wa Rukwa,  amesema kwa kiasi fulani wanasaidia hususani kwa wageni ambao wanafika jijini hapo kwa mara ya kwanza.

“Kwa mfano mimi nilishawahi kuja Mbeya kipindi cha nyuma kama mara mbili hivi, lakini sikuwahi kujua kama huku nyuma ya stendi kuna guest za bei rahisi za hadi Sh10,000,”amesema Issack.

Nuru Shkunzi mkazi wa mkoa wa Morogoro, anasema kwake anaona wapiga debe hao ni wasumbufu, kwa kuwa kuna wakati wanakujia hata kumi kila mmoja anakuambia twende nikakuonyeshe guest na maneno kibao hadi unachanganyikiwa uende na yupi na kushauri wafanye kazi hiyo kwa utaratibu mzuri.

Naye  Mkurugenzi Jiji la Mbeya, John Nchimbi, alipotafutwa kujua kama wanawatambua wapiga debe hao, amesema kisheria hawawatumbui bali watakuwa wanafanya biashara hiyo na wamiliki wa mabasi na wasimamizi hao wa nyumba za wageni.

Hata hivyo amesema kwa kazi ya kuwaonyesha abiria nyumba hizo za wageni ndio anaisikia,  huku akiahidi kufuatilia na kama wataona inafaa wanaweza wakairasimisha kazi hiyo kwa kuwa inaweza kuwa moja ya kivutio cha utalii jijini hapo.

Related Posts