Wajumbe kuamua hatima ya  Sugu, Msigwa kesho

Dar es Salaam. Baada ya tambo za siku 12, kesho watajulikana viongozi wa Chadema kwa nafasi za mwenyekiti na makamu wake katika kanda za Nyasa, Magharibi na Serengeti.

Kanda hizo zinaundwa na mikoa ya Mara, Shinyanga, Simiyu, Tabora, Katavi, Kigoma, Mbeya, Songwe, Iringa, Njombe na Rukwa.

Uchaguzi katika Kanda ya Nyasa utaamua ama Mchungaji Peter Msigwa atetee nafasi ya uenyekiti baada ya kuiongoza kwa awamu mbili mfululizo kuanzia mwaka 2016 au inyakuliwe na Joseph Mbilinyi ‘Sugu’.

Mchuano kati ya wawili hao unatarajiwa kuwa mkali, kutokana na umaarufu walionao wawili hao ambao wamewahi kuwa wabunge, Mchungaji Msigwa Iringa Mjini na Sugu (Mbeya Mjini).

Waliingia bungeni 2010 hadi 2020 na pia wote wameshika nyadhifa za ujumbe wa kamati kuu ya chama hicho.

Tayari uchaguzi umefanyika katika Kanda ya Victoria ambako Ezekia Wenje ametetea nafasi ya uenyekiti dhidi ya John Pambalu ambaye ni Mwenyekiti wa Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha).

Uchaguzi katika Kanda ya Victoria inayojumuisha mikoa ya Mwanza, Geita na Kagera ulifanyika Mei 25, Wenje alitetea nafasi hiyo kwa kura 59 dhidi ya Pambalu aliyepata kura 13.

Hata hivyo, Pambalu alijitoa katika mchakato huo.

Ushindani kati ya Sugu na Mchungaji Msigwa umesababisha baadhi ya makada wa Chadema wakiwamo wajumbe wa kamati, kujigawa kila mmoja akimuunga mkono mgombea anayemkubali.

Baadhi yao wakiwamo waliogombea ubunge mwaka 2020 wameonyesha wazi kumuunga mkono mgombea fulani katika uchaguzi huo utakaofanyika leo Makambako mkoani Njombe.

Wajumbe wa mkutano mkuu wa kanda takribani 120 wataamua nani awe mshindi kati ya Mchungaji Msigwa na Sugu.

Mei 25, Sugu na Msigwa walirushiana vijembe hadharani kwenye mdahalo ulioendeshwa na kituo cha televisheni cha Star uliopewa jina la ‘Nyasa tunakwenda na nani’ kila mmoja akisema yeye ndiye bora kuliko mwenzake.

Kanda ya Magharibi uchaguzi utawakutanisha vigogo wanne wakiwemo mawakili watatu wanaochuana kuwania nafasi ya uenyekiti.

Wagombea wanaochuana ni mawakili Dickson Matata, Gaston Garubindi na Ngassa Mboje, na Mussa Martine ambaye siyo mwanataaluma ya uwakili.

Takribani wapigakura 81 wataamua hatima ya Matata, Garubindi, Mboje na Martine katika nafasi hiyo.

Kanda ya Magharibi ni pekee ambayo wagombea wote wanne walipitishwa na Kamati Kuu ya Chadema iliyoketi kufanya usaili Mei 11 hadi 14.

Kanda za Serengeti, Victoria, na Nyasa baadhi ya wagombea walienguliwa kwa sababu mbalimbali ikiwemo kutokidhi vigezo.

Uchaguzi katika Kanda ya Serengeti leo utawakutanisha Gimbi Massaba, ambaye ni makamu mwenyekiti wa kanda hiyo kwa sasa atakayechuana na Lucas Ngoto aliyewahi kuwa mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Mara.

Tofauti ya Serengeti na kanda nyingine, hakuna mgombea uenyekiti anayetetea nafasi hiyo, wote wanawania kwa mara kwanza.

Katibu wa Kanda ya Nyasa, Gwamaka Mbughi amesema maandalizi ya uchaguzi yamekamilika, ikiwemo wajumbe, wagombea na wasimamizi, kuwasili mkoani Njombe.

Kwa upande wake, Katibu wa Kanda ya Serengeti, Jackson Mnyawani alisema:

“Kila kitu kinakwenda sawa, uchaguzi utafanyika Shinyanga mjini, tutaanza mkutano wetu saa tatu asubuhi.”

Related Posts