Wataka elimu ya afya ya akili itolewe shuleni

Dar es Salaam. Wakati matukio ya watu kujiua yakiendelea kushika kasi nchini yakiwahusisha watoto na vijana, wito umetolewa kwa kuwepo mkakati utakaowezesha elimu ya afya ya akili kujumuishwa kwenye mitaala ya elimu sambamba na huduma za unasihi kutolewa shuleni.

Hatua hii itawezesha kuwasaidia wanafunzi kujua njia sahihi za kukabiliana na changamoto zao hasa zinazowaathiri kisaikolojia.

Msaikolojia tiba,  Isack Lema amesema mlipuko wa magonjwa ya akili unaanzia miaka 14 hivyo ni muhimu kwa hatua mathubuti kuchukuliwa kwa rika hilo ili kuwaepusha kuangukia kwenye wimbi la changamoto ya afya ya akili.

Lema ameyasema hayo leo wakati wa kukabidhi mradi wa afya ya akili katika sekondari ya Mashujaa uliokuwa ukitekelezwa na asasi  ya Tap Elderly Women’s Wisdom for Youth (TEWWY).

Msaikolojia hiyo ambaye alikuwa mkufunzi katika mradi huo amesema watoto na vijana wa rika balehe wanakabiliwa na changamoto lukuki ambazo zinaweza kuwafanya waangukie kwenye changamoto ya afya ya akili.

“Programu hii imesaidia kuwabaini wanafunzi wenye changamoto na wakapewa afua ambazo zimeweza kuwaepusha dhidi ya matatizo ya afya ya akili. Walimu wamefundishwa kutofautisha tabia za kawaida za watoto na changamoto.

Hapo awali ilikuwa vigumu kumbaini mwanafunzi mwenye changamoto ilikuwa inawekwa kwendi moja kwamba ni utukutu au ujeuri hivyo waliishia kupigwa na kupewa adhabu zilizoongeza tatizo lakini sasa wamebadilika,” amesema Lema.

Hilo limethibishwa na Mkuu wa sekondari Mashujaa, Joyce Kivelege ambaye ameeleza kuwepo kwa mabadiliko makubwa ya kitabia kwa wanafunzi hali inayochangia kupanda kwa kiwango cha taaluma.

“Tumeona mabadiliko makubwa katika kipindi hiki cha mwaka mmoja tangu mradi huu uanze kutekelezwa hapa shuleni, watoto wamekuwa huru kuzungumza  wanayopitia  na tunashirikiana kutatua changamoto zao wanaendelea vyema na masomo,” amesema Joyce.

Mkurugenzi wa TEWWY Rustika Tembele amesema shule ni sehemu muhimu kwa elimu ya afya ya akili kupelekewa ili kuwanusuru watoto na vijana wa rika balehe wasitumbukie kwenye janga hilo ambalo limeshagharimu maisha ya wengi.

Kulingana na takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) zaidi ya watu 700, 000 hupoteza maisha kwa mwaka kutokana na kujiua, hiyo ikiwa sababu ya nne ya vifo vinavyotokea kwa vijana wenye umri kati ya miaka 15 hadi 29.

Afya ya akili inatajwa kuchangia kwa kiasi kikubwa hali hii ya kuwasukuma watoto na vijana kukatisha uhai wao au hata kuangukia kwenye matumizi ya dawa za kulevya, ngono zembe na vitendo vya uhalifu.

Related Posts