Dodoma. Wabunge wamecharuka wakilalamikia ahadi zisizotekelezwa za ujenzi wa barabara, mwingine akitoa ushahidi wa hotuba za Wizara ya Ujenzi za miaka mitano.
Mbunge mwingine ametoa ushahidi wa sauti iliyosikika ya Spika Dk Tulia Ackson na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi wa wakati huo, Profesa Makame Mbarawa, akithibitisha kuhusu ujenzi wa barabara ya kiwango cha lami katika Jimbo la Mbulu, mkoani Manyara.
Akichangia mjadala wa hotuba ya bajeti ya Wizara ya Ujenzi iliyosomwa bungeni leo Jumatano Mei 29 2024 na Waziri Innocent Bashungwa, mbunge wa viti maalumu, Halima Mdee alihoji kutotekelezwa mradi wa ujenzi wa barabara saba za kiwango cha lami zenye jumla ya kilomita 2,035 kwa kutumia utaratibu wa EPC+ F ndani ya mwaka mmoja.
“Tulitarajia mnakuja mnatuambia tunaomba msamaha tulikuwa hatujajipanga, tulikurupuka tukalidanganya Bunge. Mnakuja mnaandika kasentesi kamoja mnajua tumeshasahau, maisha yanaendelea,” amesema Mdee alipohoji utekelezaji wa mradi huo uliotiwa saini mwaka jana.
Mradi huo uliwasilishwa bungeni na Profesa Mbarawa kwenye hotuba ya mpango na makadirio ya mapato ya matumizi ya fedha kwa mwaka 2023/24 ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kwa wakati huo.
Profesa Mbarawa amesema: “Katika mwaka wa fedha 2022/23 wizara ilianza taratibu za manunuzi kwa ajili ya kuwapata makandarasi wa kujenga kwa kiwango cha lami barabara saba zenye jumla ya kilomita 2,035 kwa kutumia utaratibu wa Engineering, Procurement, Construction and Financing (EPC + F). Barabara hizi zitafungua fursa za kiuchumi katika maeneo zinapopita na kwa Taifa.”
Waziri Bashungwa kwenye hotuba ya bajeti kwa mwaka wa fedha 2024/2025 amesema:
“Serikali imepanga kutekeleza miradi saba ya ujenzi wa barabara zenye jumla ya urefu wa kilomita 2,035 kwa utaratibu wa EPC+F. Serikali inaendelea na mazungumzo na wafadhili ili kupata fedha za utekelezaji wa miradi hiyo. Napenda kuwahakikishia wabunge kuwa dhamira ya Serikali ya kutekeleza miradi hii ya EPC+F bado ipo palepale.”
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, katika maoni yalisomwa na mwenyekiti wake, Selemani Kakoso imesema:
“…hadi wakati kamati inakamilisha tathmini ya bajeti ya wizara kwa mwaka wa fedha 2023/24, miradi inayotekelezwa kwa utaratibu wa EPC + F ilikuwa haijaanza kutekelezwa kwa kuwa hakuna fedha iliyotolewa ya kutekeleza miradi hiyo.”
Kamati imeshauri Serikali ifanye tathmini kuhusu utaratibu huo kuona iwapo una tija.
Wakati wa utiaji saini mikataba hiyo na makandarasi Juni 16, 2023, Waziri Mbarawa amesema ujenzi wa barabara hizo wenye thamani ya Sh3.775 trilioni unatarajiwa kukamilika kwa muda wa miaka minne tangu wakati huo.
Mdee amehoji sababu za kutoanza kwa mradi huo ulioelezwa ungetoa ajira 20,300.
“Rafiki yangu mwenyekiti Kakoso kasema Tanzania inaandika historia ya kujenga barabara za urefu wa kilomita 2,035. Akasema awali tulikuwa tunajenga kilomita 200 tu mpaka 250 kwa mwaka. Tukapiga makofi maisha yakaendelea, mikataba ikasainiwa makandarasi wako huko tunaomba leo mtuambie,” amesema.
Mdee amehoji kuhusu Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) akieleza ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) za utekelezaji wa miradi ya maendeleo au za kaguzi mbalimbali za kitaalamu zilibaini mapungufu kwenye ubora wa barabara.
“Nitanukuu maeneo mchache Tanroads iliingia gharama Sh130.5 bilioni katika miradi sita, kwa sababu gani kuna upungufu mkubwa katika pembuzi yakinifu, dosari katika usanifu, katika usimamizi wa mikataba, kuchelewesha malipo Sh130 bilioni,” amehoji.
“Ulifanyika ukaguzi wa kiufundi na udhibiti ubora ulihusisha miradi minane kati ya 2009 hadi 2022, kati ya miradi minane ya barabara zilizokaguliwa, miradi saba ilikuwa na upungufu wa usanifu,” alisema.
Amemshauri Waziri Bashungwa kuifumua wizara hiyo kwa kuwa ina madeni ya riba ya Sh913 bilioni na kwenye hotuba ya bajeti hazijulikani zitapatikana wapi.
Mbunge wa Korogwe Vijijini, Timotheo Mzava ameingia bungeni na ushahidi wa vitabu vya bajeti za kuanzia mwaka 2019-2020, 2020-2021. 2021-2022, 2022-2023, 2023-2024 na sasa 2024-2025 akieleza zote zimeonyesha kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara yao ya Soni- Bumbuli hadi Dindila wilayani Korogwe yenye urefu wa kilomita 74, lakini hadi sasa haijajengwa.
Amesema hata ilani ya uchaguzi ya CCM ya 2010 ukurasa wa 76, ilani ya 2015 ukurasa wa 49 na ilani ya 2020, zote zinazungumzia ahadi ya ujenzi wa barabara hiyo, ambayo Serikali haijaitekeleza, akisema hata kwa bajeti iliyosomwa jana na Bashungwa hana imani nayo.
Mbunge wa Mbulu Vijijini, Flatei Massay amedai kupigwa ‘changa la macho’ baada ya ahadi alizopewa jimboni kutotimizwa na Wizara ya Ujenzi, akitumia kishikwambi kutoa ushahidi.
Massay aliwahi kuruka sarakasi bungeni Mei 23, 2022 kuonyesha msisitizo wa hoja yake kuwa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi haikutekeleza ahadi ya ujenzi wa barabara ya Mbulu hadi Haydom.
Mbunge huyo leo ameleta ushahidi wa sauti ya Dk Tulia na Profesa Mbarawa kuhusu ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami ilyotolewa bungeni.