Njombe. Licha ya baridi kali inayopuliza katika mji wa Makambako Mkoani Njombe muda huu, wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wameendelea kusubiri kujua ni nani ataibuka mshindi wa nafasi ya mwenyekiti wa Kanda ya Nyasa.
Uchaguzi huo unaofanyika leo Mei 29, 2024, ambapo muda huu wajumbe wenye sifa ya kupiga kura, ndiyo wanaingia ukumbini kupiga kura za kuwapata viongozi kanda hiyo.
Uchaguzi wa viongozi wa mabaraza umeshafanyika na sasa kura zinaendelea kuhesabiwa.
Awali, baada ya kumalizika kwa uchaguzi wa viongozi wa mabaraza, viliitishwa vikao vya ndani ambavyo vimemalizika na sasa wajumbe wanarejea ukumbini kwa ajili ya kuwachagua viongozi hao wa kanda, ambao ni pamoja na nafasi ya Mwenyekiti, ambayo ina mchuano mkali na inawaniwa na Mchungaji Peter Msigwa ambaye anatetea nafasi yake na Joseph Mbilinyi ‘Sugu’.
Nafasi nyingine ni ya makamu mwenyekiti na mtunza hazina.
Pamoja na kumaliza uchaguzi wa mabaraza (Bawacha, Bavicha na Bazecha) lakini bado haijatangazwa rasmi washindi licha ya kuwapo fununu za waliopenya katika nafasi hizo.
Shauku ya wengi ni kujua mshindi kati ya wagombea wa nafasi ya mwenyekiti kutokana na nguvu waliyonayo wagombea wake ndani na nje ya chama hicho.