Dar es Salaam. Zaidi ya wananchi 180 wa Mbagala, wapo kwenye hekaheka ya kusaka makazi ya kuishi, baada ya nyumba zao kubomoka kufuatia maporomoko ya tope na nyufa kwenye ardhi.
Wananchi walioathirika mpaka sasa ni wa mitaa ya Mkondogwa, Kilungule na Kiburugwa.
Kufuatia kadhia hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Sixtus Mapunda amesema tayari amekiandikia barua Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), kuomba wataalamu wa kufanya uchunguzi kubaini sababu ya ardhi kugawanyika na udongo kujongea kwenye eneo hilo lenye wananchi.
Mwananchi ilifika Mtaa wa Mkondogwa leo Mei 29, 2024 na kushuhudia baadhi ya nyumba zikiwa na nyufa kubwa, kutitia ardhini na nyingine zikiwa zimebomoka kabisa.
Wananchi hao wameiambia Mwananchi kuwa ni takribani wiki tatu tukio hilo limetokea na idadi ya nyumba zilizoathirika imeongezeka.
Wamesema jambo linalowatia hofu tope hilo kuendelea kujongea zaidi na kubomboa nyumba nyingi, kilio chao Serikali ichukue hatua za haraka kuwapatia mahala pa kujisitiri kwa muda ili kuondoka kwenye maeneo hatarishi.
Kwa sasa wameeleza kuwa, bado wanaishi kwenye nyumba zilizobomoka na wengine wakilala nje kwani hawajapata msaada.
Salma Mkugilo mkazi wa Saku amesema kwa wiki tatu sasa hana pa kukaa na amekuwa akilala chini kwa muda mrefu.
“Tunalala chini, tumeenda serikalini kuomba walau mahema tupate kujisitiri kwa muda bado hatujapata msaada, wapo wengine wanaenda kulala barazani kwa watu,”amesema.
Kilio chake kwa Serikali waharakishe uchunguzi lakini waondolewe kwenye eneo lenye matatizo kwa muda na kupatiwa makazi ya kujisitiri.
Maumivu ya kubomokewa kwa nyumba yapo pia kwa Hamza Said mkazi wa Saku mwisho ambaye amesema hajui hatma yake.
“Tulianza kushuhudia mpasuko wa ardhi baada ya mvua kukatika,ardhi inapopasuka nyumba inatitia na kuanguka, mpaka sasa hatujui tunakwenda kuishi wapi, nilikuwa na nyumba yenye vyumba vitano, bado nimeendelea kukaa humo na familia yangu sina pa kwenda,”amesema.
Kilio hicho hakitofautiani na cha Mwanaheri Kaisi ambaye kwake tope limejaa na nyumba kupata nyufa.
“Naomba Serikali iangalie haraka suala hili, maji yanaingia mpaka ndani bado hatujapata ufumbuzi viongozi wanakuja wanaondoka bila kutoa mrejesho wa nini hatma yetu,”ameeleza.
Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Mapunda amesema tangu mwaka 2014 eneo hilo lilipimwa na kubainika kuwa na chemchem.
“Watu waliambiwa wakati huo wahame, sasa tukio hili kwa wakati huu limetokea wakati hakuna mvua, tumewaomba watu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kuja kupima kujua tatizo nini,”amesema.
Kiongozi huyo wa wilaya amesema, mwaka 2014 tukio kama hilo lilivyotokea kulikuwa na mvua hivyo sasa limetokea wakati hakuna mvua ndio maana wameitisha uchunguzi kubaini chanzo.
Kwa hatua za awali, Mapunda amewaomba wananchi walioathirika baadhi yao kwenda kuishi kwa jamaa zao kwani hakuna eneo la kuwaweka kwa pamoja.
“Kwa wale ambao wana matatizo zaidi tunaendelea kuwatafutia msaada,”amesema.
Mbunge wa Mbagala, Abdallah Chaurembo amekiri kufahamu changamoto wanayopitia wananchi wake akisema tayari amewasilisha kero hiyo Serikalini.
“Tukio hilo nalifahamu, mimi ni mkazi wa Saku niwape pole wananchi wangu, jitihada zinaendelea na tunawasiliana na Serikali ili wananchi hao wapate faraja,”amesema.