Dar es Salaam. Baadhi ya wananchi wamekuwa na maoni tofauti kuhusu uendeshaji wa vivuko nchini, wengine wakishauri ili kukabiliana na changamoto zinazojitokeza vibinafsishwe kwa sekta binafsi, huku wengine wakipinga.
Hayo yameelezwa leo Mei 29, 2024 kwenye mjadala ulioendeshwa na Mwananchi Space, ukiwa na mada isemayo ‘Nini kinaweza kuwa suluhu ya changamoto inayoikabili Temesa kuhusu huduma za vivuko?’
Akichokoza mada, Mwandishi Mkuu wa gazeti la Mwananchi, Elias Msuya amesema kutokana na changamoto zilizopo ni muhimu vivuko vikabinafsishwa kwa sekta binafsi kuviendesha na Serikali ibaki kubwa mdhibiti.
“Ili kukabiliana na changamoto ya vivuko, Serikali iweke mazingira mazuri ya kibiashara kwa sekta binafsi kuendesha vivuko kwa bei ya kibiashara. Wakifanya hivyo, watakuwa wamejihakikishia usalama wa abiria na Serikali itabaki kama mdhibiti,” amesema.
Akichangia mjadala huo, Melcksedeck Mbata amesema karakana za Temesa (Wakala wa Ufundi na Umeme) zibaki kutengeneza vivuko na shughuli zingine iachiwe sekta binafsi, zikiwamo za usafirishaji.
Amesema baadhi ya wanaopewa nafasi kwenye taasisi kama vile Temesa wanazingatia masilahi binafsi kwanza, badala ya kuangalia ya umma.
Kaimu Msemaji wa Sekta ya Miundombinu wa Chama cha ACT-Wazalendo, Filbert Macheyeki amesema haamini kila jambo likienda tofauti suluhisho liwe kubinafsishwa.
“Tukienda kwa mtindo huo ipo siku watasema hata ndege ya Rais tumeshindwa kuiendesha apewe mwekezaji binafsi, jukumu la Serikali ni kuhudumia wananchi. Wananchi wa Kigamboni wako ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” amesema.
Amesema wananchi hao wanastahili kupewa huduma sawa kama wa maeneo mengine, hivyo Serikali ione umuhimu wa kuboresha vivuko.
“Tunatambua ziko hujuma kwa baadhi ya watu wanashirikiana na Temesa, kuhujumu vivuko hivi ili ionekane Serikali imeshindwa na viendeshwe na watu binafsi.”
“Tunafahamu Serikali imekuwa ikitenga bajeti ya ukarabati na utengenezaji wa vivuko, lakini bado hatuoni changamoto hii ikiisha katika maeneo mbalimbali. Hata ukisoma ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) inaonyesha kuna uzembe uliokuwa ukifanywa na Temesa kwenye vivuko,” amesema.
Akichangia mjadala, Rhimba Kupere, mwananchi aliyejitambulisha kuwa yuko mkoani Tanga amedai watendaji wengi nchini ni wazuri katika kuzungumza lakini si katika kutenda kwa kujali maisha ya wengine.
Amesema baadhi ya viongozi hawako makini katika kusimamia mambo, akitoa mfano wa eneo la Jangwani ambalo hukumbwa na mafuriko mara kwa mara wakati wa mvua lakini wananchi waliachiwa wakajenga nyumba za makazi.
Mbali ya viongozi, amesema wananchi pia kwa upande wao wamekuwa wakisababisha matatizo kwa kutowawajibisha viongozi wazembe.
Macheyeki ameshauri kiundwe chombo kingine nje ya Temesa kitakachosimamia usafiri wa vivuko nchini katika kukabiliana na changamoto zinazoonekana.
“Temesa ibaki na majukumu yake ya ufundi, umeme, ukarabati na ujenzi wa vivuko. Huduma ya usafirishaji ibaki serikalini lakini kuwe na kitengo kingine cha kusimamia usafiri,” amesema.
Pia ameshauri iundwe tume kuchunguza hujuma zinazosemekana kuwapo akidai baadhi ya watu kwa makusudi wamekuwa wakihujumu kwa lengo la kutaka apewe mwekezaji binafsi.
Tangu Jumatatu Mei 27, 2024 Mwananchi imekuwa ikitoa ripoti maalumu kuhusu wanayopitia wananchi katika vivuko vya Magogoni-Kigamboni na yanayoendelea ndani ya Temesa.