KATIKA kila nchi wapigakura huwa na mambo yanayowafanya kuamua chama gani wakichague wakati wa uchaguzi, ambapo wapo ambao hukichagua kuongoza kwa kuamini kutakuwepo na amani na wengine umuzi wao huegemea ukabila, dini, uchumi, elimu, afya na mambo mengine.
Lakini katika Bara la Asia na visiwa vya Caribbean, mtazamo wa chama cha siasa au serikali iliyopo madarakani juu ya mchezo wa kupiganisha majogoo huchangia kwa kiasi kikubwa chama gani kishike hatamu ya kuongoza nchi.
Hii inatokana na kila baada ya muda kusikika habari za watu kuuawa na majogoo wao wenyewe au wa watu wengine.
Hivi sasa serikali ya Ufilipino inatakiwa ifanye uamuzi mgumu juu ya mchezo huo. Ni ama kuupiga marufuku au uendelee na kufurahisha maelfu ya watu mijini na vijijini katika nchi hiyo yenye visiwa zaidi ya 1,700.
Hofu iliyopo ni kwamba ukipigwa marufuku mchezo huo sio tu nchi itapoteza mapato, bali serikali pia itapoteza kuungwa mkono katika uchaguzi. Katika tukio la mapema mwezi Mei, mpiganishaji majogoo mmoja katika kisiwa cha Kakinada, Gande Suryapraksha Rao (43) alikatwa na visu alivyomfunga jogoo wake kwenye mbawa.
Jamaa alikwenda kumpongeza jogoo wake kwa ushindi, lakini jogoo akamrukia na visu vilivyomuua jogoo aliyeshindana naye kabla, kwa kumchana vibaya na papo hapo kuiaga dunia.
Matokeo kama hayo yamewahi kuripotiwa sehemu nyingi katika miezi ya karibuni na hasa walipouawa watazamaji waliorukiwa na jogoo aliyefungwa visu vikali. Waswahili huwakebehi watu wa vijijini kwa kuwaambia “Jogoo la shamba haliwiki mjini”.
Msemo huo hutumika kupeleka ujumbe anapotokea mtu aliyetamba kijijini alikotoka, lakini mjini akajikuta anagonga mwamba. Kwa maana nyingine anaweza kuwika kwao shamba, lakini akashindwa hata kupiga chafya mjini.
Hapa nchini msemo huu uliwahi kutumika miaka ya nyuma katika kandanda kwa kuziambia timu za mikoani kwamba haziwezi kung’ara katika mashindano ya kitaifa kama Kombe la Taifa au Ligi Kuu.
Lakini, kuna tuliiona timu ya shamba la miwa ya kiwanda cha sukari cha Arusha Chini (Moshi), Tanganyika Planting Company ikiwika Dar es Salaam na miji mingine ya Afrika Mashariki. Hii ilikuwa katika miaka ya 1960 na 1970.
Mseto ya Morogoro ilikuwa Klabu Bingwa ya Tanzania katika miaka ya mwanzoni mwa 1980 na wachezaji nyota waliotoka shamba (nje ya Dar es Salaam) ndio waliwika katika timu ya taifa.
Majogoo nayo hushindanishwa na yapo mashindano ya kandanda na ya dunia ya mchezo huo. Mchezo wa kupiganisha majogoo wa aina inayoitwa Kuchi (asili yake Kutchi, India) ambao hapa nchini wapo na ndio wanaotumiwa katika mapigano hayo.
Bei za kuchi mahiri Tanzania na hasa Zanzibar
hufikia Sh500,000 na katika nchi ambapo watu hucheza kamari katika mchezo wa kupiganisha majogoo bei ya jogoo mahiri wa kupigana huzidi Dola 5,000 za Marekani (zaidi ya Sh16 milioni).
Jogoo moja nchini Thailand wa umri wa miezi 16 alipopelekwa Irak aliweka rekodi kwa kununuliwa kwa Dola 10,000 (takriban Sh27 milioni). Kabla ya hapo jogoo aliyeuzwa kwa bei kubwa Irak ilikuwa ni Dola 8,000 (takriban Sh25 milioni).
Mchezo wa kupiganisha majogoo unavutia watu wengi barani Asia, Ufilipino, Amerika Kusini na visiwa vya Carribbean ambapo vipo viwanja maalumu vya kupiganisha majogoo vya watazamaji hadi 20,000.
Mahasimu wakubwa wa mchezo huo ni Ufilipino na Dominica ambao wanasifika kuwa na mbegu nzuri za majogoo wanaopigana kwa umahiri na kuwauwa kikatili. Katika nchi ya Puetro Rico mchezo huo unatambulika kama wa kitaifa na unatoa ajira kwa watu 27,000. Makao makuu ya mchezo huo ni Kabul, Afghanistan.
Zipo sheria na kanuni za mchezo, lakini hukiukwa. Kwa mfano, jogoo anayeshiriki mashindano anatakiwa azidi umri wa mwaka mmoja na miezi mitatu na uzito usiopungua kilo mbili.
Mashindano huwa ya uzito kama ule wa ndondi na ya mizunguko mitatu, sita na tisa, na jogoo hupewa mafunzo ya kuelewa atapigana mizunguko mingapi.
Mashindano huwa ya ligi na mtoano na ni ya nusu saa, lakini mara nyingi humalizika baaada ya dakika tano au 10.
Wapo majogoo ambao kabla ya kushiriki mashindano huonyeshwa video na wamiliki ili kujua mbinu za mpinzani. Yapo mashindano yanayotangazwa moja kwa moja na vituo vya redio na televisheni. Utasikia “Jogoo Santa ananyemelea hatua ya kwanza…ya pili, anaruka anampiga teke mpinzani na kumdonoa.”
Ni ruhusa kumvalishwa jogoo visu au vijembe vinavyokubalika katika kucha au mbawa, lakini visiwe na visipakwe sumu au dawa ya kulevya. Majogoo mawili huachiwa wapigane mpaka mmoja afe au hoi na hawezi kuendelea.
Ni kawaida kuona mashabiki wanalia jogoo wanayempenda anapodhalilishwa na wakati wa mapumziko jogoo hupewa ushauri kama anavyofanya kocha wa kandanda. Sheria haziruhusu jogoo kupigana zaidi ya mara mbili kwa mwezi. Mchezo huo ulianza karibu miaka 6,000 iliyopita Uajemi (Iran) na ukasambaa India, China, Ugiriki na Uturuki.
Katika miaka ya nyuma mabaharia wa Ufilipino walipiganisha majogoo melini kama burudani. Zipo nchi zilizoingiza mchezo wa kupiganisha majogoo katika katiba na zilizoupiga marufuku kwa kuwa unakiuka haki za wanyama kuishi kwa raha na furaha.
Lakini mashabiki wa mchezo wanasema ukatili mkubwa
hufanywa na walaji ambao huua kuku kwa mamilioni au maelfu kila siku na kutaka ulaji kuku upigwe marufuku. Wapo mashabiki wanaowapenda majogoo zaidi ya wake na watoto wao na huwapeleka katika saluni maalumu kuogeshwa na kupulizwa dawa, kutengenezwa kucha na kuchuliwa misuli.
Mchezo huo ni maarufu katika ukanda wa pwani wa Tanzania, Bara na Visiwani. Ipo hadithi maarufu Zanzibar ya mzee mmoja aliyemuona mwanawe aliyepanda baiskeli akiwa amebeba jogoo anayepiganishwa akigongwa na mkokoteni na kuanguka.
Yule mzee alimshughulikia jogoo wake kwanza na tangu siku ile akaitwa “Jogoo”. Hawakukosea waliosema dunia hii ina mengi.