Sanaa na michezo ni sehemu ya utamaduni wa Taifa lolote. Ni kielelezo cha utamaduni, lakini pia hudumisha mahusiano na urafiki baina ya mataifa. Ni kivutio kikubwa cha utalii kwa wageni wanaoingia kwenye Taifa hilo. Kupitia sanaa na michezo wageni huburudika na kujifunza utamaduni wa jamii husika.
Katika wakati uliopita, wasanii na wanamichezo duniani kote walikuwa katika mfumo wa ridhaa. Hawakutambulika rasmi kuwa ni wachangiaji wa pato la Taifa. Hapa nyumbani walitumika kuhamasisha maelekezo ya viongozi kama kujikomboa, kufanya kampeni za afya, chakula bora, elimu (ikiwemo ya watu wazima) na za maendeleo kwa ujumla.
Baada ya hapo walishughulika na kuburudisha viongozi na wananchi baada ya kazi ngumu za ujenzi wa Taifa.
Kadiri muda ulivyokuwa ukienda mifumo nayo ilikuwa ikibadilika. Huko Ulaya na Marekani kuliibuka mapinduzi ya sekta binafsi ambapo michezo na sanaa ziliingizwa kwenye ajira rasmi.
Ilikuwa ni hiari ya mtu kuchagua kulipwa (professional) ama kubaki kwenye ridhaa (amateur) baada ya kujitathmini uwezo wake. Hapa kwetu tulichelewa kidogo, na sababu kubwa ilikuwa ni siasa yetu ya Ujamaa na Kujitegemea.
Lakini awali ya yote nilitaka kukumbusha kwamba wakati mfumo mpya unaingia uliwakuta wazee wetu waliopambania uhuru na uhamasishaji wa vijiji vya ujamaa wakiwa wameshachoka.
Hawakuifanya kazi ile ya uhamasishaji kwa malipo, bali uzalendo. Hivyo haikuwa rahisi kwao kuingia kwenye ushindani huu mpya.
Heshima waliyobaki nayo ilikuwa ni kuandaa misingi kwa wanamuziki wa kizazi kipya na historia ya mafanikio ya nchi yetu.
Ndipo sasa tukaanza kuona timu zetu zikianza kuwapa mikataba na kuwalipa wachezaji kutoka nje.
Wanamuziki wakaanza kupewa tuzo na kulipwa mirabaha kutokana na kazi zao, vyama vya siasa vilianza kuwalipa wasanii kwenye kampeni zao, na hata Serikali ilianza kutoa fungu kwa wale walioshiriki kampeni mbalimbali za kijamii.
Pale mwanzoni walikuwa wakilipwa posho iliyofanana na nauli tu.
Kutokana na kufanya kazi za ridhaa, wasanii hawa wazee hawakuweza kujijengea nyumba, kujinunulia magari wala kuweka akiba ya uzeeni. Na kwa kuwa nguvu zimeshawaishia hawawezi kuingia kwenye mfumo wa profeshno. Wamebaki kuwa mafukara wanaotegemea watoto, ndugu, jamaa na marafiki. Kwa maisha ya sasa, hiyo ni hali ngumu zaidi maishani, kwani ni sawa na kuomba lifti kwenye gari iliyojaa. Kila mmoja ana mzigo wa kuubeba.
Nakumbuka marehemu Gurumo aliwahi kupelekewa zawadi ya gari na mmoja wa wanamuziki wa kizazi kipya. Lakini naweza kusema gari hiyo haikumfaa ipasavyo kwa sababu alishakuwa na mahitaji ya vitu vingine tofauti. Kwa wakati ule shida yake kubwa ilikuwa chakula na matibabu. Ni ajabu sana kuona mtu akikosa hela ya kula akajaza mafuta kwenye gari. Au aache kwenda hospitali na badala yake apeleke gari sevisi.
Binafsi nimekuwa karibu na wanasoka na wanamuziki wa zamani. Kusema ukweli hali zao zinasikitisha sana, kwani wengi wao walitoka kwenye familia masikini, lakini wakategemewa kwa zile posho kidogo walizolipwa. Hivi sasa hawana namna nyingine ya kuishi zaidi ya kutegemea watu, watu ambao nao wanaelemewa na makali ya maisha.
Waliobahatika ni wale wanaosaidiwa na wenzao waliozaliwa na matajiri, ambao sasa ni wafanyabiashara.
Ukiondoa ufukara wao, bado ni watu wanaohitajika sana kwenye fani. Kwa mfano kwenye upande wa muziki wapo waliopata elimu kutoka kwa magwiji waliotokea nje ya Tanzania. Wana hazina kubwa ya ujuzi wasiyojua mahala pa kuipeleka. Pia kwenye michezo tunawaona walimu wachache wenye mbinu za hali ya juu.
Ninaamini iwapo hawa wazee wetu watathaminiwa, kutatokea maendeleo makubwa ya muziki na michezo zaidi ya Afrika Magharibi na Kusini.
Mama umekuwa mhamasishaji mkubwa wa sanaa na michezo. Kupitia jitihada zako tumeona timu zetu zikipanda madaraja ya kimataifa. Pia tumeona jinsi ligi zetu zinavyoongeza ladha ya michezo nchini.
Sasa ni wakati wa kukuza vipaji vyetu vya ndani ili sanaa na utamaduni vitoe nafasi kubwa ya ajira kwa Watanzania wengi ambao baadhi yao wanashindwa kuendesha maisha yao kutokana na kutotumia vipaji vyao kujiingizia kipato.
Natambua jitihada unazofanya kuwekeza kwenye sanaa na utamaduni, lakini kundi hili ni kubwa, zinahitajika jitihada za makusudi kuongeza uwekezaji kwenye eneo hili ili watu wengi zaidi wanufaike na fursa zilizopo kwenye sekta hiyo.
Natumia muda huu kukuomba msaada wako mama, uwaundie Wizara ama Taasisi itakayoshughulika nao moja kwa moja. Kupitia mwavuli huo tunaweza kuyatumia madini adhimu, na tukaachana na ile dhana ya jogoo aliyepiga teke kidonge cha dhahabu na kukimbilia punje ya mtama.
Hawa ni watu wanaotafutwa sana na wageni, na laiti wangelikuwa na uwezo wagekimbilia nje kuanza upya.
Walichumia juani, lakini hawakupata kulia kivulini baada ya mti kukatwa.