SIKU moja baada ya nahodha, John Bocco kuaga mashabiki na wachezaji wenzake wa Simba, kaimu kocha mkuu wa timu hiyo, Juma Mgunda amesema yeye ndiye aliyemshauri straika huyo mkongwe awe kocha.
Bocco amedumu miaka saba ndani ya kikosi cha Simba baada ya kujiunga na Wekundu wa Msimbazi msimu wa 2017/18 na kutwaa mataji manne ya Ligi Kuu na kuisaidia timu hiyo kucheza robo fainali tano za michuano ya CAF, nne zikiwa za Ligi ya Mabingwa Afrika na moja ya Kombe la Shirikisho.
Akizungumza na Mwanaspoti, Mgunda amefichua siri kuwa uamuzi aliouchukua Bocco wa kustaafu kucheza soka na kusomea ukocha umechangiwa na ushauri wake huku akikiri kuwa anajivunia kuwa mmoja wa makocha waliomfundisha straika huyo wa mabao.
“Ukimtafuta na kumuuliza kuwa nani alimshauri asomee ukocha atanitaja mimi, Bocco ni kijana wangu, mbali na kumfundisha amekuwa muungwana sana na msikivu, namtabiria kuwa atakuja kuwa kocha bora miaka ujayo,” amesema Mgunda na kuongeza;
“Bocco ni mchezaji kiongozi na ndio maana mara nyingi timu alizopita alikuwa nahodha kwa sababu ni mchezaji ambaye anaweza kuishi na kila mtu na ni mwepesi wa kumwelekeza mtu akaelewa,” alisema.
Mgunda alisema Bocco ni mchezaji ambaye ataendelea kuishi mioyoni mwa Taifa na sio Simba tu kwasababu mambo makubwa aliyoifanyia hii nchi sio kwa upande wa klabu tu bali hadi timu ya taifa ‘Taifa Stars’.
“Naheshimu uamuzi wa mtu, amechagua kustaafu na kusomea ukocha, anatakiwa kupewa kipaumbele na kuheshimiwa kwani amefanya kazi kubwa kwenye timu zote alizopita alikuwa hazina kwa taifa kama mchezaji,” amesema na kuongeza;
“Sasa natarajia kumuona akiwa bora pia kwenye nafasi yake ya ukocha, natarajia kuona akiwa miongoni mwa makocha bora zaidi kwa miaka ya hivi karibuni,” amesema Mgunda.
Nahodha wa Simba, Mohammed Hussen ‘Tshabalala’ amesema Bocco ataendelea kuishi kwenye moyo wake kwani ndani ya miaka saba waliyofanya kazi naye pamoja alikuwa ni bora kwao.
“Ni kaka yangu na kiongozi wangu kwenye maisha yangu ya mpira, nafikiri hata kitambaa cha unahodha nimekipokea kutoka kwake, amenifunza mengi siwezi kuzungumza nikayamaliza,” amesema na kuongeza;
“Bocco ni mchezaji kiongozi na ni mlezi, nimeishi naye miaka saba ambayo ilikuwa na mafanikio makubwa kwangu na kwake pia, namshukuru kwa yote na nitaendelea kuzungumza naye kwa ajili ya kuniongoza ninapokwama,” amesema.