Mume adai kudhulumiwa Sh4 milioni na mkewe

Dar es Salaam. Shahidi wa kwanza, Rashid Kiwamba amedai mahakamani kuwa mkewe Habiba Mohamed amemtapeli Sh4 milioni fedha ya nyumba waliyouza eneo la Ulongoni.

Inadaiwa kuwa kati ya Septemba 28, 2023 eneo la Ulongoni Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam mshtakiwa, Habiba alipokea Sh4 milioni kutoka kwa mumewe, Rashid Kiwamba kupitia benki ya NMB akimwaminisha kuwa fedha hizo zitakuwa salama wakati akijua siyo kweli.

Kiwamba akiongozwa na Wakili wa Serikali, Agnes Majula mbele ya Hakimu Mkazi mwandamizi wa Mahakama ya Wilaya ya Ilala, Rehema Lyana, amedai kuwa Septemba 28, 2023 akiwa na mkewe Habiba waliuza nyumba yao iliyopo eneo la Ulongoni kwa Sh14 milioni mbele ya Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Ulongoni B, Mohamed Mzala.

Amedai baada ya kuuza nyumba hiyo kiasi waliwapa madalali Sh2 milioni na Sh2 milioni waligawana yeye na mke wake ambapo kila mmoja alipata Sh1 milioni, huku fedha zilizobaki Sh10 milioni  walikubaliana kuzipeleka benki ya NMB tawi la Gongolamboto.

“Mteja alinunua nyumba yetu kwa fedha taslimu Sh14 milioni baada ya kutoa Sh4 milioni tulizogawana pamoja na madalali zilibaki Sh10 milioni, ambazo tukakubaliana kila mmoja achukue Sh5 milioni na nilipotaka kuchukua hela yangu mke wangu alihoji suala la watoto itakuaje?” amedai Kiwamba.

Kiwamba ameieleza Mahakama hiyo kuwa baada ya malumbano hayo Mwenyekiti wa Serikali ya mtaa huo, Mzala aliwashauri wanandoa hao waende nyumbani wakajitafakari kuhusu watoto na fedha hizo zipelekwe benki.

Amedai baada ya kushauriwa na mwenyekiti huyo alihoji kuwa yeye hana akaunti ya benki fedha hizo zitahifadhiwa wapi ndipo mkewe Habiba alimjibu kuwa anayo akaunti ya NMB zitawekwa huko.

Kiwamba amedai baada ya kuelewana fedha zinapelekwa kwenye akaunti ya mke wake ndipo Mwenyekiti Mzala alitengeneza mkataba wa makubaliano kuwa fedha hizo zitawekwa kwenye akaunti ya NMB ya Habiba.

Baadaye walikubaliana ndani ya wiki moja Oktoba 5, 2023 wakutane wote kwenye nyumba waliyouza lakini mke wake Habiba hakutokea ndipo alimpigia simu mwenyekiti huyo ambaye alimweleza ampigie simu kaka wa  mke wake ili kujua yupo wapi.

“Nilimpigia simu kaka yake mke wangu aliniambia tukutane Oktoba 7, 2023 ilipofika siku hiyo nilimtafuta lakini sikufanikiwa kuonana naye.

“Wakati nikiendelea kumtafuta nilipewa taarifa kuwa mke wangu alitoa fedha tulizokuwa tumeweka kwenye akaunti yake na alienda nazo   eneo la Chanika kununua nyumba ya Sh8 milioni,” amedai Kiwamba.

Kiwamba amedai baada ya mke wake kununua nyumba hiyo alimpatia Sh1 milioni badala ya Sh5 milioni kama walivyokubaliana kwenye mkataba.

Hakimu Rehema Lyana, ameahirisha kesi hiyo hadi Juni 25, 2024 itakapoitwa kwa ajili ya kuendelea na ushahidi.

Related Posts