Dodoma. Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Jerry Silaa, ameanzisha kituo cha huduma ya ardhi, ikiwa ni hatua ya kukabiliana na migogoro ya ardhi katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
Hatua hiyo imekuja siku moja baada ya Bunge kupitisha bajeti ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa mwaka 2024/25, huku wabunge wengi wakilalamikia kuhusu migogoro ya ardhi inayosababishwa na umiliki wa kiwanja kimoja zaidi ya mtu mmoja.
Wabunge hao walilamikia hali hiyo kujitokeza kwa kiwango kikubwa katika Jiji la Dodoma, ambapo alisema wabunge zaidi ya 30, naibu mawaziri sita ‘wamepigwa’ kwenye masuala ya ardhi jijini humo.
Silaa ameyasema hayo leo Mei 28,2024 katika ofisi za Kamishna wa Ardhi Mkoa wa Dodoma alipokutana na kitengo cha ardhi cha Halmashauri ya Jiji.
Amesema mwaka 2019, Serikali ilifanya uamuzi iliwaondoa watumishi wote wa ardhi chini ya halmashauri na kuwapeleka kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Amesema nia ilikuwa ni njema ya kutengeneza utaratibu mzuri wa kiutendaji na kuifanya wizara hiyo kufanya shughuli zake kiweledi.
Amesema maeneo mengine kwa sababu ya mfumo wa zamani ikiwemo Wilaya ya Mpwapwa na nyingine lazima kuwe na ofisi inayoanzisha michakato na miamala ya masuala ya ardhi kabla ya haijaenda kwenye mkoa.
Amesema maswali ya kujiuliza ni kama kuna umuhimu wa kuwa na ofisi mbili katika eneo moja zinazofanya mchakato mmoja.
“Mtu yoyote aliyekwenda shule jambo lolote analifanyia tathimini. Sasa tumekaa na kufanya tathimini na inaonyesha kwa utendaji wa kuwa na ofisi mbili zinazofanya jambo moja kwa mwananchi mmoja lazima utaleta mgongano,”amesema.
Amesema timu iliyoundwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ilikuta watu 3,000 wakiwa wamepewa viwanja vyenye umiliki wa zaidi ya mtu mmoja.
Amesema Halmashauri ya Dodoma Mjini itabaki na kazi kama mamlaka ya upangaji kama sheria inavyotaja majukumu yake.
Aidha, amewaondoa hofu wabunge na Watanzania amesema kliniki za ardhi zitafanywa katika maeneo ambayo yana changamoto zilizokithiri.
Naye Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Geofrey Pinda amesema wakati anaingia katika wizara hiyo mwaka jana, kwake palikuwa ni mahali pagumu kutokana na hali iliyokuwepo katika wizara hiyo.
“Wote tunakiri kwamba bajeti hii imepita bila mazonge yoyote sasa kwa ubinadamu wetu changes (mabadiliko) za maisha lazima tuwe flexible (tuzikubali). Na kuwa jambo alilolifanya linakwenda kuwa ni chanzo kizuri cha kufanya mabadiliko,”amesema.
Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Antony Sanga amesema kuwa hakuna mkoa wenye viwanja vyenye hati zaidi ya moja kama Dodoma ambapo kuna hati zaidi ya 3000.
“Kuna wakati zilifika hati 3,900, niwapongeze kwa hatua mbalimbali ambazo mmeendelea kuzichukua za kukabiliana na hilo baada ya kuwa mnapima kule Mahomanyika,”amesema.
Amesema wizara imeamua kufanya mabadiliko hayo kwa kuhamishia masuala yote ya ardhi kwa kamishna wa ardhi ili kuondoa kero zote zilizopo Dodoma.