Simba mpya Mgaboni, Matampi | Mwanaspoti

KAZI imeanza Simba. Na inaanzia langoni. Simba imeanza mchakato wa kusuka upya kikosi chake na tayari mezani ina majina mawili ya makipa wa kigeni ambapo watachagua mmoja.

Wamefikia uamuzi huo kwani wanaona kuna kila dalili ya kumpoteza kipa wao namba moja wa sasa, Mmorocco Ayoub Lakred licha ya kwamba inadaiwa mpenzi wake ameanza kupaelewa Bongo.

Kipa wa kwanza mezani kwa Simba ni Ley Matampi wa Coastal Union ambaye tayari wameshafanya naye mazungumzo ya awali ambayo yanatarajiwa kuendelea kesho baada ya Mkongo huyo kuja Dar akitokea mkoani Tanga.

Mbali na Matampi (35) ambaye ndiye kinara wa ‘clean sheet’ katika Ligi Kuu Bara msimu huu akiwa nazo 15 kuna kipa mwingine wa Gabon, Loic Owono ambaye inapambana kumvuta Msimbazi.

Owono ambaye anaitumikia FC 15 de Agosto de Akonibe ya Guinea, ndiye kipa bora pia kwenye Ligi Kuu nchini humo akiwa na clean Ssheet 14 msimu huu.

Simba ilikuwa inamtaka kipa huyo kuja nchini kumalizia mazungumzo na mabosi wa Wekundu hao lakini ratiba ya mechi za timu ya Taifa lake imetibua mambo hivyo wanalazimika kuwa wapole kwa muda.

Owono (24) ndiye kipa chaguo la kwanza la Gabon, kuna uwezekano mkubwa Juni 7 mwaka huu akaidakia timu hiyo ya Taifa lake itakapocheza dhidi ya Ivory Coast katika mchezo wa Kundi F wa kufuzu Kombe la Dunia 2026.

Mabosi wa Wekundu hao wanataka Owono awe chaguo namba moja, nje ya Matampi ambaye bado Simba haina uhakika wa kumpata licha ya kuendelea na mazungumzo. Mbali na Simba, Horoya nayo inamvizia kipa huyo ili imsajili kwa msimu ujao ikivutiwa na uimara wake ndani ya misimu miwili ingawa pia baadhi ya vigogo wanahofia uswahiba wake na baadhi ya mashabiki nguli wa Yanga.

Simba bado haina uhakika wa kusalia kwa kipa wao namba moja Ayoub Lakred ambaye inaelezwa huenda akaachana na timu hiyo baada ya kumaliza mkataba wake mwisho wa msimu huu huku juzi katika mchezo wa mwisho wa ligi dhidi ya JKT Tanzania akionekana kuwaaga mashabiki.

Lakred amekuwa na msimu bora zaidi ndani ya Simba ambapo amemaliza na ‘Clean Sheet’ 10 katika ligi akifanikiwa kwa kiasi kikubwa kuziba pengo la Aishi Manula ambaye ni majeruhi wa muda mrefu.

Simba msimu huu imekuwa na makipa watano ambao ni Lakred, Manula, Ally Salim, Hussein Abel na Ahmad Ferooz ambaye alikaa benchi katika mechi ya ligi dhidi ya Dodoma Jiji, huku golini akikaa Hussein Abel. Ferooz pekee ndiye hakucheza mechi yoyote lakini wengine wamedaka katika msimu wa 2023-2024.

Uamuzi wa Simba kuanza harakati za kusajili kipa ishu kubwa ni kutokana na Manula kuwa majeruhi na ana asilimia kubwa ya kuondoka Msimbazi huku Lakred akiwa njiani kuondoka ikielezwa kwamba ana ofa kutoka timu za nyumbani kwao Morocco.

Endapo Lakred akiondoka, watakaobaki ni Salim, Abel na Ferooz. Uongozi wa Simba unaona kubaki na makipa hao pekee haitakuwa sawa kwani wana kibarua cha kushiriki michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu ujao baada ya kumaliza nafasi ya tatu kwenye ligi msimu huu, hivyo lazima wapate kipa mzoefu wa kimataifa.

Kuhusu maboresho ya kikosi cha Simba kuelekea msimu ujao, Kaimu Kocha Mkuu wa Simba, Juma Mgunda amesema lazima hilo lifanyike, hivyo atawasilisha ripoti kwa Bodi ya Wakurugenzi kuainisha nini kifanyike kuijenga timu imara zaidi.

Mgunda ambaye aliiongoza Simba katika mechi tisa za mwisho katika ligi baada ya kuondoka kwa Abdelhak Benchikha raia wa Algeria, amesema usajili unaokwenda kufanyika ndani ya Simba utagusa maeneo mengi kulingana na kile alichobaini muda mfupi aliokaa na kikosi hicho.

“Unakuja usajili mpya na msimu mpya hivyo lazima vitu vipya viwepo. Kuna vitu ambavyo tumeviona tangu ligi imeanza hadi mwisho.

“Mimi nilipewa mechi tisa, katika mechi hizo nimeona mazuri ambayo yapo na kuna mapungufu pia yapo ambayo kwenye ripoti yataandikwa, lakini nikuhakikishie tu kwamba lazima kuna mambo yatafanyiwa mabadiliko. Nitawasilisha katika bodi mambo ambayo yatatakiwa kufanyika ili msimu ujao Simba ifanye vizuri zaidi,” alisema Mgunda.

Related Posts