Dar es Salaam. Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) inaendelea na safari yake ya kuwawezesha na kuwaendeleza wauzaji wake kupitia mpango unaojulikana kama (Retailer Development Programme).
Mpango huo ambao kwa kifupi unaitwa (RDP), ulizinduliwa Oktoba mwaka jana ukilenga kusaidia wauzaji kukuza biashara zao na kujifunza ujuzi mpya ikiwemo usimamizi wa fedha, hisa, masoko, mauzo na ukuzaji wa kibiashara kwa uwajibikaji.
Mafunzo maalumu ya kibiashara yatakayoendeshwa kuanzia leo Mei 29, 2024 wauzaji waliochaguliwa kwa awamu ya majaribio ya mpango huo watapitia mtaala wa ujuzi wa moduli sita, unaojumuisha miongozo ya wakufunzi na vitabu vya washiriki vilivyoandaliwa kulingana na mahitaji yaliyobainishwa ya wauzaji na kulenga kubadili tabia.
TBL ina zaidi ya wauzaji 28,000 kote Tanzania. Mpango wa maendeleo ya wauzaji, ambao utatekelezwa kwa awamu, unahakikisha kwamba wajasiriamali hawa wanajifunza mbinu mpya za biashara na wanaweza kuendana na mazingira ya biashara yanayobadilika, ambayo yanaendelea kuvurugwa na mabadiliko ya kidijitali.
Mkurugenzi Mtendaji wa TBL Michelle Kilpin, amesema kuwa mpango wa maendeleo ya wauzaji ni sehemu ya ahadi ya TBL ya kuleta athari chanya katika jamii ya Kitanzania.
“Tunajitahidi kila mara kuleta athari yenye maana katika jamii zetu na tumejikita katika njia ya ukuaji inayowalenga watu. Mpango huu wa maendeleo ni ishara ya ahadi hiyo, amesema Kilpin.
Mkufunzi wa programu hiyo kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dotto Kuhenga amesema kuwa wauzaji wanahimizwa kufikiria upya mifano ya zamani ya uendeshaji. “Tunawahimiza wauzaji kuwa wabunifu na wepesi zaidi katika uwezo wao wa kuhudumia wateja.”