Tuzo za TFF kutolewa mechi ya Ngao ya Jamii

TUZO za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kwa msimu huu zitafanyika wakati wa mchezo wa Ngao ya Jamii tofauti na mwanzoni zilipokuwa zinafanyika siku tatu kabla ya kumalizika kwa fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC).

Katika taarifa iliyotolewa na TFF ilieleza kwamba, sababu kubwa za tuzo hizo kufanyika kipindi hicho ambacho huwa ni kuashirikia msimu mpya ni kwa ajili ya kulifanya tukio hilo kuwa bora zaidi ili kukidhi malengo na mahitaji yake.

Tuzo za TFF ni tukio la kuwazawadia wanamichezo waliofanya vizuri katika mashindano yanayoandaliwa na shirikisho hilo na Bodi ya Ligi (TPLB) na matukio mengine rasmi yenye kuambatana na mpira wa miguu hapa nchini.

Kwa maana hiyo, sherehe hizo zitafanyika wakati wa mchezo wa ufunguzi kuashiria msimu mpya wa 2024/2025 ambapo bingwa wa Ligi Kuu Bara ambaye ni Yanga itakuwa ikicheza na mshindi atakayechukua taji la Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC).

Hata hivyo kutokana na Yanga kuingia fainali ya FA maana yake hata kama itashinda mchezo huo itacheza na Azam FC ambazo zote zitapambana Juni 2, mwaka huu kwenye Uwanja wa New Amaan Complex visiwani Zanzibar, mechi ikipigwa kuanzia saa 2:15 usiku.

Kitendo cha timu hizo kufika fainali ni ishara tosha kwamba zitakutana katika Ngao ya Jamii kwani licha ya kufika tu fainali ila inabebwa pia na kumaliza nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara uliohitimishwa rasmi jana Mei 28.

Hata hivyo wakati TFF ikisogeza tuzo hizo mbele kwa ajili ya kuzifanyia marekebisho ila ni kinyume kwani kanuni ya 11:11 ya Ligi Kuu Bara inayohusu vikombe na tuzo inazitaka zifanyie siku tatu baada ya fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC).

Kwa maana hiyo, tuzo hizo zilitakiwa kutolewa Juni 5, baada tu ya kuisha kwa mchezo wa fainali ya FA kati ya Yanga dhidi ya Azam FC.

Msimu uliopita Yanga ilipata jumla ya tuzo 12 zikiwemo za mmoja mmoja na zile za kikosi bora ambapo aliyekuwa nyota wa kikosi hicho, Fiston Mayele alichukuwa ya Mfungaji Bora, Bao bora la msimu, Mchezaji Bora wa jumla wa msimu yaani (MVP).

Kipa wa timu hiyo, Djigui Diarra alishinda tuzo mbili za kipa bora wa Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) na Ligi Kuu na Dickson Job akipata ya beki bora wakati Bakari Mwamnyeto akiwa mchezaji bora wa ASFC na wote waliingia katika kikosi bora.

Aliyekuwa Kocha wa Yanga, Nasreddine Nabi alikuwa kocha bora huku Clement Mzize akishinda tuzo ya mchezaji bora kijana chini ya miaka 20.

Simba ndiyo ilikuwa timu ya pili wachezaji wake kuchukuwa tuzo nyingi ikiongozwa na Saido Ntibazonkiza aliyebeba tatu ya mfungaji bora baada ya kufunga mabao 17, Fair Play (mchezo wa kiuungwana) na kiungo bora huku pia akiingia kwenye kikosi bora.

Wengine ni Henoc Inonga, Mohammed Hussein, Shomari Kapombe, Mzamiru Yassin, Clatous Chama ambao wote waliingia kikosi bora cha msimu.

Tuzo ya mchezaji bora chipukizi wa Ligi Kuu ilienda kwa Lameck Lawi wa Coastal Union huku mchezaji bora wa Championship alikuwa Edward Songo wa JKT Tanzania wakati Kamishina Bora wa Ligi Kuu tuzo hiyo ilikwenda kwa Isack Munisi

Tuzo ya mwamuzi bora wa Ligi ya Wanawake (WPL) msimu wa 2022/23 ilienda kwa Ester Adalbert wakati mwamuzi msaidizi ni Glory Tesha.

Mwamuzi bora wa Ligi Kuu Bara msimu huo tuzo hiyo ilienda kwa Jonesia Rukyaa huku tuzo ya mwamuzi Msaidizi ikienda kwa Frank Komba.

Tuzo ya seti bora ya waamuzi imekwenda kwa Jonesia Rukyaa, Zawadi Yusuph, Athuman Rajabu na Ally Simba katika mechi ya Geita Gold na Dodoma Jiji.

Mfungaji Bora wa Ligi Kuu ya Wanawake msimu uliopita tuzo hiyo ilienda kwa Jentrix Shikangwa wa Simba Queens aliyefunga mabao 17.

Kocha wa JKT Queens, Ally Ally alishinda tuzo ya kocha bora wa Ligi Kuu ya Wanawake huku mchezaji bora akiwa ni Donisia Minja.

Chipukizi bora wa Ligi ya Wanawake kwa msimu huo ilienda kwa Winfrida Charles wa Alliance Girls huku kipa bora wa Ligi ya WPL alikuwa ni Najat Abbas wa JKT Queens.

Related Posts