Ujenzi Daraja la Jangwani wanukia

Dodoma. Serikali imesema katika mwaka wa fedha wa 2024/25 itaanza utekelezaji wa mradi wa kimkakati wa ujenzi wa Daraja la Jangwani.

Ujenzi huo ni sehemu ya utekelezaji wa mradi mkubwa wa maendelezo ya Bonde la Mto Msimbazi.

Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amesema hayo bungeni leo Jumatano Mei 29 2024  alipowasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka 2024/25.

Wizara imeliomba Bunge kuidhinisha Sh1.7 trilioni, kati ya hizo Sh1.6 trilioni ni fedha za miradi ya maendeleo.

Amesema Mradi wa Uendelezaji wa Bonde la Mto Msimbazi (DMDP II) utatekelezwa kwa fedha za Serikali na mkopo kutoka Benki ya Dunia (WB) kwa kujenga miundombinu ya barabara, mifereji, maeneo ya wazi na masoko.

Mingine ni ya vituo vya mabasi, kurekebisha miundombinu ya taka ngumu, ya usafiri na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwa Jiji la Dar es Salaam.

Kuhusu mchakato wa ujenzi wa daraja la juu ‘Fly Over’ kuanzia Magomeni kupita Jangwani hadi Faya, amesema zabuni imeshatangazwa na mkandarasi atakayejenga atajulikana hivi karibuni.

Bashungwa amesema daraja litakalojengwa lina urefu wa mita 390 na barabara unganishi zenye urefu wa mita 710 na kina cha mita 15.5 kutoka usawa wa bahari.

“Daraja litakapokamilika litatatua changamoto ya kujaa maji katika Barabara ya Morogoro eneo la Jangwani wakati wa mvua na kusababisha kufungwa kwa barabara hiyo mara kwa mara. Tathmini ya zabuni ili kumpata mkandarasi na mhandisi mshauri zinaendelea,” amesema.

Akizungumza na waandishi wa habari Februari 7, 2024 jijini Dar es Salaam, mratibu wa mradi, Mhandisi Humphrey Kanyenye kutoka Tamisemi amesema wameshatangaza zabuni kwa ajili ya kumpata mkandarasi kuanza ujenzi.

Tayari baadhi ya wananchi wanaoishi eneo la mradi wameshafidiwa na wameondoka kupisha.

Amesema Serikali kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) imepanga kujenga barabara kuu zenye urefu wa kilomita 385 kwa kiwango cha lami, ukarabati wa kilomita 35 kwa kiwango cha lami, na ujenzi wa madaraja 17.

Amesema Tanroads itafanya ukarabati wa daraja moja, kufanya maandalizi ya ujenzi wa madaraja tisa na kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa madaraja mawili katika barabara kuu na baadhi ya zile za mikoa.

Amesema Serikali itajenga barabara za kuelekea katika vituo vya Reli ya Kisasa (SGR) zenye urefu wa kilomita 87.6.

Amesema zimetengwa Sh8.8 bilioni kwa ajili ya kuendelea na ujenzi wa barabara ya Kizota – Zuzu (kilomita 14).

Kazi nyingine ni kuanza ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara za kuelekea katika vituo vya reli ya kisasa ambazo ni Morogoro – Kihonda (kilomita 10), Rudewa – Kilosa (kilomita tatu), Gulwe – Gulwe (kilomita mbili), na Igandu – Igandu (kilomita 27).

Nyingine ni Ihumwa – Ihumwa Marshalling Yard (kilomita 5.5), Bahi – Bahi (kilomita 4), Mlandizi – Ruvu (kilomita 22), barabara za ndani za kituo cha SGR cha Dodoma (mita 100) na barabara ya Pugu – Kiltex (kilomita 6.7).

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, katika maoni yalisomwa na mwenyekiti wake, Selemani Kakosa imesema imebaini baadhi ya wananchi katika maeneo mbalimbali nchini walioachia maeneo kupisha miradi inayosimamiwa na Wizara ya Ujenzi bado hawajalipwa fidia.

“Kamati inaishauri Serikali kuhakikisha wananchi wote wanaodai fidia walipwe stahiki zao kwa mujibu wa sheria na iwapo Serikali haina uwezo wa kulipa fidia katika maeneo waliyotwaa, yarejeshwe kwa wananchi,” amesema.

Kamati ilizungumzia matuta barabarani ikisema kuna haja ya kuyaondoa ambayo si ya lazima.

“Kamati inashauri Serikali ifanye tathmini kubainisha maeneo ambayo hakuna umuhimu wa kuwepo matuta na iwapo maeneo hayo yana matuta, basi yaondolewe,” amesema Kakosa.

Amesema uwepo wa matuta una athari hasi za kiuchumi kwa watumiaji wa magari.

Hata hivyo, kwa maeneo yenye ulazima alisema matuta hayo yawe na viwango stahiki na vinavyolingana nchi nzima.

Related Posts