VIVUKO KIGAMBONI: Mifumo inavyotishia uhai wa Temesa – 4

Dar es Salaam. Changamoto zilizobainika kwenye vivuko vya Magogoni – Kigamboni zinazotokana na kucheleweshewa matengenezo, zimeibua mambo mapya ndani ya Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (Temesa).

Haya ni ya mifumo ya uendeshaji inayozingatia zaidi utoaji huduma badala ya kufanya biashara, ambayo inauweka rehani uhai wakala huo.

Mifumo hiyo kwa mujibu wa uchunguzi wa takriban miezi mitatu wa Mwananchi, inasababisha Temesa kufanya kazi katika mazingira magumu, na hata kukabiliwa na lindi la madeni.

Kupitia uchunguzi huo, Mwananchi imebaini wakala huo licha ya kutekeleza jukumu la matengenezo ya magari ya taasisi za Serikali, haijalipwa mabilioni ya fedha.

Hali hiyo imechangia Temesa kuingia madeni ya zaidi ya Sh35 bilioni kutoka kwa wazabuni kutoka sekta binafsi ambao wanaisambazia vipuli kwa ajili ya matengenezo ya magari hayo.

Mmoja wa maofisa waandamizi wa Temesa (jina linahifadhiwa) anaeleza mfumo wa utendaji wa wakala huo upo katika misingi ya utoaji huduma.

Hilo linatokana na anachoeleza kuwa sheria ya kuanzishwa kwa wakala ya mwaka 2005 inautaja kuwa taasisi ya Serikali yenye lengo la kuhudumia na siyo kufanya biashara.

Anasema mifumo inataka Temesa itoe huduma ilhali uhalisia wa shughuli zake zina sura ya kibiashara.

“Temesa inajihusisha na matengenezo ya magari ya taasisi na wakala za Serikali, pia inahusika na uendeshaji wa vivuko, kwenye hizi shughuli zote tunakusanya mapato na kimsingi ni biashara, unapotaka tutoe huduma hatutapata kinachotarajiwa,” anasema.

Chanzo cha kuaminika ndani ya Temesa kinaeleza wakala huo upo mahututi kutokana na kukabiliwa na madeni.

Anasema kwa sababu wakala huo hauna mtaji, unalazimika kusimama katikati ya wazabuni wenye vipuli ambao ni sekta binafsi na taasisi za Serikali zenye magari.

Kutokana na hilo, anasema wanakopa vipuli kutoka kwa wazabuni ambao ni sekta binafsi kwa ajili ya kutengeneza magari ya taasisi za Serikali, zikiwamo halmashauri.

“Tunakopa kwa hawa wazabuni, tunatengeneza magari ili tukilipwa na taasisi za Serikali nasi tunawalipa wazabuni,” anasema.

Hata hivyo, anasema kazi ya matengenezo ya magari imekuwa janga kwa Temesa, kwani baadhi ya wateja wake, ambao ni taasisi za Serikali hazilipi gharama za matengenezo.

“Na hii siyo kwa Temesa, ni suala la mtazamo wa taasisi nyingi, zinapoona huduma inatolewa na wakala au taasisi nyingine ya Serikali huwa hazilipi,” anaeleza.

Katika mazingira hayo, anaeleza kuwa wakala huo umebaki kudaiwa na wazabuni kwa kuwa fedha za kuwalipa zipo kwa wateja.

Mwananchi imebaini taarifa ya mwisho ya madeni ambayo Temesa iliiwasilisha Hazina, inadai takribani Sh40 bilioni kwa taasisi za Serikali.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya mwanzoni mwa mwaka huu, pamoja na Temesa kudai kiasi hicho cha fedha, yenyewe inadaiwa na wazabuni zaidi ya Sh35 bilioni.

Fedha hizo ni za mkopo wa vipuli vilivyotolewa kwa Temesa.

Ofisa mwingine ndani ya Temesa anasema kila mwaka kwa wastani kuna asilimia kati ya 60 na 70 ya madeni ya kudai na kudaiwa ambayo huvuka mwaka mwingine wa fedha.

“Kwa hiyo ni kweli tunadaiwa kwa sababu nasi hatulipwi,” anasema ofisa huyo.

Ofisa huyo anaeleza ugumu wa kulipwa unatokana na wakala kukosa nguvu ya kisheria ya kukusanya madeni.

“Unamdai mtu lakini huna kitu chake chochote ulichoshika kama dhamana, ambacho unasema asipolipa nitauza hiki. Hata hivyo, hairuhusiwi kukamata gari hata kama unadai,” anasema.

“Benki zingekuwa zinakopesha na hazichukui dhamana ingekuwa hatari, hivyo ndivyo tunavyofanya kazi. Unamkopesha mtu na huna kitu chake chochote kwa ajili ya kushinikiza malipo,” anasema.

Mwaka mmoja uliopita kulikuwa na shinikizo la kuitaka Temesa kushirikiana na Kampuni ya Toyota.

Hata hivyo, mifumo ya utendaji wa Temesa ndiyo iliyokwamisha ushirikiano huo, baada ya Toyota kuweka masharti magumu ambayo pengine yasingekuwa na tija kwa wakala huo.

Kwa mujibu wa ofisa ndani ya Temesa, katika ushirikiano huo walianza kwa kukaa vikao, timu za uratibu wa shughuli ziliundwa, na ulifika wakati wa kujua masharti gani Toyota inatoa ili kufanya kazi na wakala huo.

“Walileta orodha hiyo balaa… kwanza wakataka kwenye bajeti ya matengenezo ya magari inayotolewa na Serikali asilimia 50 iingizwe kwao,” anaeleza.

Sharti lingine anasema Toyota ilitaka anapopatikana mteja, fedha za vipuli zilipwe kwao na za ufundi ndizo zilipwe Temesa.

Iwapo hilo lingetokea, anasema Toyota ingekuwa na nguvu ya kukamata magari ambayo hayatalipia huduma na Temesa ingekufa kwa kukosa fedha za kujiendesha.

“Temesa haitaweza kujiendesha kwa mapato ya ufundi pekee, ni madogo mno,” anasema.

Anasisitiza kushindikana kwa hayo kumetokana na ukweli kwamba, bado Serikali haijajua inataka kutoa huduma au kufanya biashara kupitia Temesa.

Walipotafutwa watendaji wa Kampuni ya Toyota, walidai mwenye mamlaka ya kuzungumzia hilo hayupo nchini.

Hata hivyo, juhudi za kumtafuta aliyetajwa kuwa na mamlaka hayo hazikuzaa matunda, kwani kampuni hiyo haikuwa tayari kutoa mawasiliano ya mhusika huyo.

Mtendaji Mkuu wa Temesa, Lazaro Kilahala akizungumzia madai hayo, anasema mipango ya mabadiliko ya utendaji wa wakala huo inaendelea.

Anataja mipango hiyo pamoja na mambo mengine, inahusisha mageuzi ya utendaji ili kuhakikisha wakala unazalisha faida katika shughuli zake.

Hata hivyo, Kilahala anakiri wakala huo kuwa na madeni kutoka kwa wazabuni, akieleza yanalipwa kwa kadiri fedha zinavyopatikana.

“Wadeni wote wanalipa kwa mujibu wa taratibu, msisitizo ni kuhakikisha wakala unakuwa na ufanisi, ndiyo maana tunatarajia kufanya mageuzi ya utendaji wa wakala,” anasema.

Mkuu wa Idara ya Fedha wa moja ya halmashauri katika Mkoa wa Dar es Salaam (jina linahifadhiwa), anasema bajeti za OC (fedha za matumizi mengineyo) za halmashauri nchini hazihusishi matengenezo ya magari.

Anasema kwa kuwa hakuna bajeti hizo kutoka Serikali Kuu, halmashauri zinalazimika kukopa matengenezo na zinashindwa kulipa kwa sababu hakuna pa kupata fedha.

“Si umeona magari mengi ya Serikali kwenye halmashauri yakiharibika kidogo tu, yanaachwa yanaoza, sababu ya yote haya ni kukosekana bajeti ya matengenezo ya magari,” anasema.

Ili kutatua changamoto hizo, mwanazuoni wa biashara za kimataifa, Profesa Francis Matambalya anasema kuna umuhimu wa kubadilishwa sheria iliyoanzisha Temesa ili wakala huo, ujiendeshe kibiashara.

Katika mabadiliko ya sheria, anapendekeza suala la uendeshaji wa vivuko liondolewe chini ya Temesa na utafutwe utaratibu mwingine.

“Iwe taasisi tendaji, isiwe wakala kwa sababu inakuwa na watu wengi wenye maamuzi, hata unapofukuza watumishi iwe kwa sababu za kitendaji na si maelekezo ya mwenye maamuzi,” anasema.

Pendekezo la namna hiyo limetolewa pia na mmoja wa maofisa waandamizi wa Temesa alipozungumza na Mwananchi.

Kwa mujibu wa ofisa huyo, uendeshaji wa vivuko ni moja ya majukumu yanayoibebesha mzigo Temesa, hivyo anaeleza kuna umuhimu wa kufanya mabadiliko.

“Ianzishwe kampuni kwa ajili ya kuendesha vivuko, shughuli za utengenezaji magari ndizo ziachwe kwa Temesa ili kuipunguzia mzigo,” anasema.

Related Posts