Waafrika Kusini leo Jumatano wanapiga kura katika uchaguzi wa kihistoria ambao kwa mara ya kwanza umeruhusu wagombea huru tangu mfumo wa ubaguzi wa rangi kumalizika nchini humo mwaka 1994. Inaripoti Mitandao ya Kimataifa… (endelea).
Zaidi ya watu milioni 27 wamejiandikisha kupiga kura katika kura inayoangazia kuongezeka kwa mgawanyiko wa kisiasa baada ya miaka 30 ya demokrasia.
Vyama 70 na wagombea huru 11 wanashiriki katika uchaguzi ambao utashuhudia Waafrika Kusini wakipigia kura bunge jipya, na mabunge tisa ya majimbo.
Kwa mujibu wa Tume ya Uchaguzi Tume Huru ya Uchaguzi (IEC), vituo vya kupigia kura, vimefunguliwa kote nchini kuanzia saa moja asubuhi, saa za Pretoria na kufungwa saa tatu usiku.
Uchaguzi wa mwaka huu unaelezwa kuwa mgumu kwa chama tawala ANC ambacho kimeshika madaraka kwa miaka 30, na wadadisi wa siasa wanasema huenda ikapata chini ya asilimia 50 ya kura.
Umaarufu wa ANC umeelezwa kushuka kuelekea uchaguzi huu kutokana na chama hicho kushindwa kukatatua changamoto ya ukosefu wa ajira hasa kwa vijana, kutofanya vya kutosha kupambana na uhalifu na changamoto ya kukatika kwa umeme kila wakati.
Vyama vya upinzani vikiongozwa na Democratic Alliance (DA), Economic Freedom Fighters (EFF) na chama kipya umKhonto we Sizwe (MK) vinatarajiwa kuleta ushindani mkubwa.
Chama kitakachokuwa na wabunge wengi, kitaongoza mchakato wa kuunda serikali mpya itakayokuwa madarakani kwa miaka mitano baada ya wabunge kumchagua rais.
Rais Cyril Ramaphosa amepiga kura yake katika kituo cha Chiawelo huko Soweto, akiandamana na mkewe Tshepo Motsepe.
Kwa mara ya kwanza, wapiga kura watapatiwa karatasi tatu za kupigia kura watakapoingia kwenye chumba cha kupigia kura.
Kura ya kwanza itakuwa na orodha ya vyama vinavyowania viti 200 vya ubunge nchi nzima.
Kura ya pili itaorodhesha vyama na wagombea huru, katika majimbo yanayowania viti vingine 200 vya ubunge.
Hii ni mara ya kwanza kwa kura hii kuanzishwa ili kuwapa nafasi wagombea huru kugombea ubunge, na kuimarisha uwakilishi wa majimbo katika chombo cha kutunga sheria.
Hakuna uchaguzi wa moja kwa moja wa rais. Bunge jipya litachagua rais, ambaye kwa kawaida ndiye kiongozi wa chama kilicho na wabunge wengi.
Kura ya tatu ni ya mabunge ya majimbo, moja kwa kila majimbo tisa ya Afrika Kusini.
Wapiga kura katika kila jimbo wanapigia kura bunge lao, na wakati huu wataweza kupiga kura kwa wagombea huru, badala ya vyama pekee.
Mikoa ina bajeti kubwa, na inawajibika kwa mambo kama vile elimu na afya, pamoja na serikali ya kitaifa.