Wafanyabiashara Kariakoo walia kuzingirwa na majitaka

Dar es Salaam. Wananchi wa Mtaa wa Lindi Kata ya Gerezani Kariakoo wamesema wapo hatarini kupata magonjwa ya mlipuko kwa kuwa maeneo wanayofanyia biashara zao kuzungukwa na maji machafu yaliyo changanyika na vinyesi.

Wananchi hao wanaofanya shughuli zao hizo karibu na stendi zinapoegeshwa daladala za Gerezani -Buza wamesema wanashangaa kuona wanatozwa ushuru lakini usafi hauzingatiwi katika maeneo hayo.

Wameyasema hayo leo Mei 29, 2024 baada ya Mkuu wa mkoa huo, Albert Chalamila kufanya ziara katika eneo hilo na kusikiliza kero za wananchi kuhusu biashara wanazofanya.

“Maeneo haya licha ya kuwa na madimbwi lakini kuna chemba mbili nazo zinafurika maji ya mvua yanachanganyika kinyesi hivyo tupo  hatarini kiafya,” amesema Hezron Subi.

Mfanyabiashara mwingine wa eneo hilo, Fadhili Abdallah amesema changamoto ya madimbwi limekuwa tatizo sugu wamelalamika kwa zaidi ya miaka mitatu lakini hakuna hatua zinazochukuliwa.

“Barabara hii inatumiwa na kutegemewa na magari mengi ikiwemo hizo daladala zinazopaki hapo karibu viongozi wanaona lakini ndiyo hivyo,” amesema.

Naye Simbila Salumon ambaye ni dereva wa daladala zinazoenda Buza amesema kila siku wanatozwa ushuru Sh2,000, lakini stendi imekuwa chafu na kuhatarisha  usalama wao na abiria wanaosubiri usafiri.

“Bora umekuja ulibebe hili labda kilio chetu kitasikika baada ya kuhangaika muda mrefu,” amesema.

Akizungumzia kero hiyo, Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala, Jomaary Satura amekiri kuchukua ushuru kwenye eneo hilo kama maeneo mengine, lakini suala la ujenzi waulizwe Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (Dart).

Amesema kwa mwezi manispaa hiyo hukusanya ushuru wa zaidi Sh18 bilioni.

“Na hizi ni jitihada tu tunazozifanya katika ukusanyaji, lakini kuhusu ujenzi wa barabara hii waulizwe, Dart kwa kuwa kipande hicho cha barabara ni eneo lao,” amesema.  

Amesema Dart wakishatengeneza barabara hiyo na kuweka mifereji maji hayatatuama hivyo tatizo hilo litakuwa limetatuliwa.

Kwa upande wake, Mhandisi Joseph Lubilo wa Dart amesema wapo kwenye mchakato wa kujenga barabara hiyo.

“Lipo kwenye mchakato wa kujengwa na usanifu umeshafanyika na mkandarasi anayetakiwa kujenga ni yule anayejenga barabara ya Gongo la Mboto,” amesema.

Kufuatia maelezo hayo, Chalamila ameiagiza Dart kuitengeneza barabara hiyo kuanzia wiki ijayo.

“Nawataka Dart kuanzia wiki ijayo mkandarasi aje kuitengeneza barabara hii, kwani imekuwa mbaya na nitafuatilia kujua kinachoendelea,” amesema.

Vilevile, Chalamila ametoa maagizo kwa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira (Dawasa) kwenda kunyonya maji hayo machafu na kuiacha sehemu hiyo salama.

Related Posts