Wanaodaiwa kusafirisha mifupa, meno, kucha za simba bado wanaendelea kuchunguzwa

Dar es Salaam. Upande wa mashitaka katika kesi ya kesi ya kusafirisha nyara za Serikali ikiwemo mifupa 1107 ya simba yenye jumla ya thamani ya Sh3.3 bilioni, inayowakabili washtakiwa 12 wakiwemo waliokuwa wafanyakazi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege ( TAA), umedai kuwa bado unaendelea za uchunguzi dhidi ya washtakiwa hao.

Washtakiwa hao ikiwemo kampuni ya usafirishaji ya AB Marine Products Ltd pamoja na Mkurugenzi Mkazi wa  Kampuni ya Airline Ltd, wanadaiwa kusafirisha nyara hizo kutoka Msumbiji na kuzileta Tanzania, ambapo zilikuwa kuzipeleka Kuala Lumpur nchini Malaysia bila kuwa na kibali kutoka kwa Mkurugenzi wa Wanyama Pori wa nchini hizo mbili.

Wakili wa Serikali, Titus Aaron ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, leo Jumatano Mei 29, 2024 wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kutajwa.

Wakili Aaron ametoa maelezo hayo, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu,  Gwantwa Mwankuga, kuwa kutokana na upelelezi kutokukamilika, wanaomba mahakama ipange tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.

Baada ya  maelezo hayo, Hakimu Mwankuga aliahirisha kesi hiyo hadi Juni 27, 2024 itakapotajwa na washtakiwa wapo nje kwa dhamana baada ya kwenda kuomba Mahakama Kuu.

Washtakiwa katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 28/2023 ni Abdulah Hamad (58) mfanyabiashara na mkazi wa Ubungo Maziwa,  Kampuni ya AB Marine Products Ltd iliyopo Ubungo Maziwa.

Wengine ni Meneja Mkazi wa Kampuni ya Airline Ltd, Roseline Achachi Wandera (43) mkazi wa Mikocheni, Kennedy Mwambeta na  Noel Kasaro( 41) Mratibu wa Mizigo na mkazi wa Tabata.

Walinzi wawili wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege( TAA), Tito Mwabe (34) na  Erasto Makinda (46),  Wakala wa mizigo, Theresia Lukanga(40) na Abubakari Pazi(32) Wakala wa mizigo kutoka kampuni ya Smart Ocean.

Vilevile, yupo Haipeng Guo(34) mfanyabiashara na raia wa China, Yassir Husein (50) mfanyabiashara na mkazi wa Arusha pamoja na  Peter Kikweka (50) ambaye ni mfanyabiashara na mkazi wa Ukonga Mombasa.

Katika kesi ya msingi, washtakiwa wakabiliwa na mashitaka 12.

Kati ya mashitaka 12 yanayowakabili washtakiwa hao, mawili ni ya kuongoza genge la uhalifu,  mashitaka matatu ni ya kughushi,  mashitaka manne ya kukutwa meno ya tembo, shitaka moja ni kujihusisha na nyara za Serikali na shitaka lingine ni kukutwa na mifupa ya simba kinyume cha sheria

Miongoni mwa mashitaka hayo, ni shitaka la kwanza na la pili ambalo ni kuongoza genge la uhalifu linalowakabili washtakiwa wote, ambapo inadaiwa kati ya Januari Mosi 2019 na Mei 27, 2023 katika uwanja wa Ndege wa Pemba uliopo mji wa Cabo Delgado Province, nchini Msumbiji, washtakiwa walipanga genge la uhalifu kwa kupokea, kuuza na kusafirisha vipande 166 vya meno ya tembo  vyenye thamani ya Dola za Marekani milioni 1.41 sawa na Sh3.28 bilioni mali ya Serikali, bila kuwa na kibali.

Washtakiwa pia, wanakabiliwa na shitaka la kukutwa na mifupa ya simba, ambapo kati ya Januari Mosi 2019 na Mei 27, 2023 katika uwanja wa Ndege wa Pemba uliopo mji wa Cabo Delgado Province, nchini Msumbiji,  isivyo halali walikutwa na mifupa 1,107 ya simba yenye thamani ya Sh61 milioni, kinyume cha sheria.

Pia wanadaiwa kujihusisha na kupatikana na nyara za Serikali ambazo ni meno ya tembo vipande  166 vyenye uzito wa kilo 236.82, bila kuwa na kibali kutoka kwa Mkurugenzi wa Wanyamapori, tukio wanalodaiwa kulitenda kati ya Januari Mosi, 2019 na Mei 27, 2023.

Vilevile, wanadaiwa kupatikana na meno 20 ya simba na kucha 65 za simba  zikiwa na thamani ya Sh57 milioni, na kusafirisha samaki aina ya kaa bila kuwa na vibali.

Related Posts