Watumishi 13 Arumeru wasimamishwa kazi tuhuma ubadhirifu wa Sh600 milioni

Arusha. Watumishi 13 wa sekta ya afya kutoka  Halmashauri ya Arusha Dc wilayani Arumeru, wamesimamishwa kazi kupisha uchunguzi wa tuhuma zinazowakabili za ubadhirifu wa fedha za umma Sh600 milioni.

Watumishi hao akiwamo Mganga Mkuu wa Halmashauri hiyo, Petro Mboya wamesimamishwa kazi baada ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda kumuagiza Mkurugenzi wa Arusha Dc, Selemani Msumi achukue hatua hiyo kwa lengo la kupisha uchunguzi.

Akizungumza jana usiku Mei 28, 2024 kwenye mkutano wa hadhara wa kusikiliza kero za wananchi, Makonda alisema anashangaa kuona watumishi aliowatuhumu kwa ubadhirifu wa fedha hizo Sh600 milioni Aprili mwaka huu kwenye mkutano, bado wapo ofisini wakiendelea na kazi.

“Mkurugenzi ebu njoo hapa, hawa watumishi tuliwatuhumu kwa ubadhirifu wa fedha za umma zaidi ya Sh600 milioni halafu bado wanaendelea na kazi wakati uchunguzi ukiendelea dhidi yao, hii ni sahihi kweli kumchunguza mtu wakati uko naye ofisini? ameuliza Makonda.

Hata hivyo, Mkurugenzi wa Arusha Dc, Msumi amesema tayari hatua zimeshachukuliwa na suala hilo sasa lipo mikononi mwa vyombo vya usalama.

Makonda alitaka majibu pia kutoka kwa Ofisa Utumishi wa Halmashauri ya Arusha Dc, Elizabeth Ngobei ambaye alisema wameanza kuwaandikia barua za kuwataka kujieleza.

Hata hivyo, akizungumza na Mwananchi Digital leo Jumatano Mei 29, 2024, Ngobei amesema tayari watumishi hao wameshasimamishwa kazi kupisha uchunguzi.

Baada ya majibu hayo, Makonda alicheka na kusema halmashauri hiyo imeoza na inanuka rushwa.

“Yaani hii tuliyobaini ni moja tu zaidi ya Sh600 milioni na bado wanaendelea na kazi, sasa naagiza wakae pembeni kupisha uchunguzi huu kuanzia sasa,” amesema Makonda.

Amesema atamuomba Kamanda wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (Takukuru) Salum Hamduni kumuongezea nguvu ili kupambana na vitendo vya rushwa mkoani humo.

Amejinasibu kuwa ataandika barua Tamisemi kuomba Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG) kurudi mkoani Arusha kufanya tena ukaguzi wa fedha katika halmashauri zote za mkoa huo.

“Kwa mtindo huu nitaongea na kaka yangu Hamduni aniongezee nguvu ya kupambana na vitendo hivi hapa maana naona vimekithiri na pia ofisi ya CAG irudi Arusha ifanye ukaguzi upya wa fedha za umma, hivyo kaeni chonjo,” amesema.

Katika hatua nyingine, Takukuru Mkoa wa Arusha imeanza uchunguzi wa tuhuma za Ofisa Ardhi wa Halmashauri ya Wilaya ya Arusha, Shevednaze Mwakyokola, za kushawishi na kupokea rushwa ya Sh5 milioni.

Kamanda wa Takukuru Mkoa wa Arusha, Zawadi Ngailo akizungumzia tukio hilo amesema kuwa wamepokea maelekezo kutoka kwa mkuu wa mkoa na wameanza kufanyia kazi tuhuma hizo.

Awali Makonda aliagiza mtumishi huyo asimamishwe kazi kupisha uchunguzi wa tukio hilo alilodai ameshuhudia kwa macho yake.

“Nilimuona kwa macho yangu akipokea rushwa ya Sh5 milioni, na alipobaini kuwa nimemuona, aliamua kuzitupa fedha hizo zilizokuwa kwenye bahasha kwa lengo la kuharibu ushahidi wa kushawishi na kupokea fedha hiyo kinyume cha sheria,” amesema.

Related Posts