Geita. Mkazi wa Kijiji cha Chigunga wilayani Geita, Stefano Mlenda(31) amefikishwa katika Mahakama Kuu Kanda ya Geita akishtakiwa kwa kosa la kumuua bila kukusudia mtoto Fredrick Stephano (7) baada ya kuiba Sh700 na kwenda kununua soda.
Kesi hiyo namba 12387 ya mwaka 2024 ilikuja mahakamani hapo kwa ajili ya mshtakiwa kusomewa maelezo ya awali.
Akisoma maelezo ya kosa mwendesha mashtaka wa Serikali, Scollastica Teffe ameieleza Mahakama kuwa mstakiwa huyo anashtakiwa kwa kumuua Stephano bila kukusudia kinyume na kifungu cha 95 & 98 sura ya 16 kilichofanyiwa marejeo mwaka 2022.
Mshtakiwa huyo anadaiwa Novemba 16, 2023 alimpiga mtoto wake huyo kwa kwa kutumia fimbo mtoto baada ya kuiba Sh700 na kutumia kiasi hicho cha fedha kununua soda.
Inadaiwa kuwa siku ya tukio alimkuta mtoto huyo akinywa soda eneo wanalouza vinywaji, alimchukua na kurudi naye nyumbani huku akimchapa kwa fimbo na alipofika nyumbani alimfunga mikono na miguu.
Wakili wa Jamhuri ameieleza Mahakama kuwa Novemba 17, 2023 mtoto huyo alifariki na mwili ulipofanyiwa uchunguzi wa kitaalamu ilibainika kifo cha mtoto huyo kimesababishwa na majeraha kwenye kichwa na sehemu mbalimbali za mwili wake.
Mshtakiwa huyo akiwa kwa mlinzi wa amani alikiri kuua bila kukusudia.
Hata hivyo, baada ya kusomewa maelezo ya awali mshtakiwa alikana kutenda kosa hilo na kesi hiyo imeahirishwa hadi pale itakapopangwa tena.