Aliyembaka, kumuua mtoto wa miaka nane ahukumiwa kunyongwa hadi kufa

Arusha. Mahakama Kuu ya Tanzania, Masijala ndogo ya Manyara iliyoketi Mbulu imemhukumu mkazi wa Kijiji cha Dumbeta, Paskali Qamara kunyongwa hadi kufa baada ya kupatikana na hatia ya kumbaka na kumuua kwa kumnyonga, mtoto mwenye umri wa miaka minane.

Hukumu hiyo imetolewa Mei 27, 2024 na Jaji John Kahyoza baada ya kubaini ushahidi wa mashahidi wanne wa upande wa mashtaka na vielelezo walivyowasilisha mahakamani, vimethibitisha makosa dhidi ya mshtakiwa bila kuacha shaka yoyote.

Jaji huyo alisema tukio hilo lilitokea Jumapili ya Pasaka Aprili 9, 2023 katika Kituo cha kuhudumia wagonjwa wasiojiweza na wahitaji, kinachomilikiwa na Kanisa Katoliki Jimbo la Mbulu, ambako mtoto huyo alikuwa akilelewa.

Katika kumtia hatiani Qamara, Jaji Kahyoza alitumia pamoja na ushahidi wa kimazingira, maelezo aliyoyatoa wakati akihojiwa Polisi kwenye maelezo yake ya onyo, alipokiri kumuua mtoto huyo.

Akisoma hukumu hiyo, Jaji alisema upande wa mashtaka ulithibitisha kuwa katika kutekeleza azma yake ya kubaka, alisababisha kifo cha mtoto huyo.

“Nimeona imethibitishwa kuwa mtuhumiwa alimbaka mtoto huyo na katika kipindi hicho alisababisha kifo chake. Ubakaji unaadhibiwa kwa kifungo kisichopungua miaka 30, lakini kwa kuwa mshtakiwa alikuwa na nia ya kutenda kosa la ubakaji lakini alimuua pia mtoto huyo kwa ubaya,” hivyo anahukumiwa kunyongwa hadi kufa. alisema.

Jaji huyo alisema anaona upande wa mashtaka umethibitisha sambamba na ushahidi wa kimazingira pasipo shaka yoyote kwamba Qamara alimuua mtoto huyo.

Hivyo, alisema anamtia hatiani kwa kosa la mauaji kinyume na kifungu cha 196 na 197 cha Kanuni ya Adhabu, sura ya 16 kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2002.

“Ametiwa hatiani kwa kosa la mauaji, ambalo lina adhabu moja tu, kunyongwa hadi kufa kama ilivyoelezwa kwenye kifungu tajwa hapo juu na kifungu cha 322 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA). Kwa bahati mbaya mikono yangu imefungwa, sina nafasi ya utetezi kutaka apewe adhabu nafuu, ninamhukumu Paskali kunyongwa hadi kufa chini ya vifungu hivyo,” alisema Jaji.

Qamara alifikishwa mahakamani hapo akikabiliwa na kosa la mauaji ya mtoto huyo mbaye alikufa kifo cha kikatili kwa kubakwa,kunyongwa wakati au baada ya kutendeka kosa hilo ambapo alikufa kwa kukosa hewa ya kutosha.

Upande wa mashtaka katika kesi hiyo uliongozwa na Wakili wa Serikali Mary Lucas na Amilioni Mosses  huku mashahidi wa upande huo wakiwa wanne ambao ni Padri James Leonard, Joseph  Panga , Dk Denis Paskali na Sajenti  Joseph na vielelezo vinne ikiwemo maelezo ya onyo ya mshtakiwa.

Ingawa mshtakiwa huyo aliyejitetea chini ya kiapo, alijaribu kukana kukiri wakati wa utetezi wake mahakamani hapo na kudai kesi hiyo ni ya uzushi dhidi yake.

Padri huyo ambaye ni Msimamizi na Meneja wa kituo hicho alisema kuna wanufaika wanaokaa hapo na wengine wanaohudumiwa wakiwa nje ya hapo ambapo siku ya tukio waliandaa tafrija ya wanaoishi pale na wale wasioishi hapo na marehemu alihudhuria akiwa mnufaika asiye na makazi. Tafrija hiyo iliisha saa 12 jioni.

Panga aliyehudhuria maombi ya jioni, alieleza mahakama kuwa Mzee Benedict alimweleza kuwa simu yake ya mkononi aliiacha kwenye kibanda chake kwa ajili ya kuichaji na alipokwenda kuichukua alikuta kibanda kimefungwa, hivyo alimuomba yeye ambaye ndiye mmiliki wa, amsaidie kuchukua simu yake.

Ilidaiwa shahidi huyo wa pili, alienda na Benedict kwenye kibanda hicho ila walikuta kimefungwa kwa ndani. Waligonga kwa mti kulazimisha mlango kufunguliwa na alipotumia tochi ya simu kumulika ndani, alimwona Qamara amelala na kando yake kulikuwa na mtoto.

Ilidaiwa Qamara alijaribu kumfunika mtoto huyo bila mafanikio na Panga aliona msichana aliyevaa fulana tu.

Baada ya mlango kufunguka mtuhumiwa huyo aliruka na kutaka kutoroka lakini walipiga kelele kuomba msaada na kumkamata.

Padri alidai kuingia ndani ya chumba hicho na kumkuta mtoto huyo akiwa amelala chini huku miguu ikiwa imepanuka na akivuja damu sehemu zake za siri na chupi ilikuwa kando na akuwa alihisi kwamba hakuwa hai.

Ilielezwa kuwa shahidi huyo alikimbilia nje kumwokoa Qamara ambaye alizingirwa na umati wa watu wenye hasira waliolenga kumuua na alimchukua na kumweka kwenye chumba salama na kuweka walinzi kumwangalia.

Padri huyo alimwita Dk Dennis ambaye alikuwa ofisa kliniki aliyekuwa anajitolea katika kituo hicho kabla ya kuajiriwa katika Zahanati ya Huruma na kumchunguza mtoto huyo.

Jaji alieleza kuwa ushahidi wa mashtaka ulieleza kuwa uchunguzi ulibaini michubuko ukeni na alama za misumari kwenye shingo yake na kugundua kuwa, alibakwa na kunyongwa.

Dk Dennis alimshauri padri huyo kuhakikisha mwili wa marehemu hauguswi na ulihamishwa katika chumba kingine na kuripoti tukio hilo polisi ambao walikwenda eneo hilo asubuhi ya siku iliyofuata ambapo Sajenti Joseph alikuwa mmoja wa askari waliokwenda eneo la tukio.

Shahidi wa nne wa mashtaka, alisema alipofika eneo hilo alikuta mafuta ya ngozi aina ya topline, sketi, chupi na kiatu kimoja huku mwili wa marehemu ukiwa umelazwa katika chumba kingine ambapo alichukua vitu hivyo.

Aliongeza kuwa mtuhumiwa alipohojiwa alikiri kutenda kosa hilo maelezo yake ya onyo yalirekodiwa na mwili wa marehemu kupelekwa Kituo cha Afya cha Dongobesh.

Qamara ambaye ni mkazi wa Kijiji cha Dumbeta, alipokutwa na kesi ya kujibu, alijitetea akidai siku ya tukio aliwapeleka watoto wake watatu katika kituo hicho kwa ajili ya huduma na wawili kati yao walikuwa na kifafa na mwingine alikuwa akisumbuliwa na kifua.

Alidai siku ya tukio, majira ya saa nane mchana alikuwa kanisani kwa ajili ya kusali na aliamua kwenda jikoni kaungalia kama kila kitu kilikuwa sawa kama sehemu ya majukumu yake na alipofika alimkuta Panga akiwa amesimama karibu na lango la kituo hicho.

Alieleza mahakama kuwa shahidi huyo wa pili, alimwomba achukue simu yake ya mkononi aliyokuwa ameiacha akiichaji chumbani kwake na alipoingia kuanza kutafuta simu, Panga aliingia chumbani na kumuuliza kuna nini (akinyooshea kidole nyuma ya mlango).

Alidai alipoangalia na kuona mwili wa msichana mdogo ukiwa nusu uchi walitoka chumbani na kwenda kwenye lango la kituo ambako Panga aliwaambia watu kulikuwa na mwili katika chumba chake na walienda na kushuhudia, lakini hakukuwa na maelezo ya nini kilimtokea mtoto huyo.

Alidai kuwa alikamatwa saa 10 jioni na kuwekwa katika chumba ambacho kinatumika kuhifadhi wahalifu kituoni hapo, asubuhi iliyofuata Polisi walimpeleka kwenye kibanda cha Panga, wakamtesa na kumlazimisha kukubali kutenda kosa hilo na kuwa licha ya mateso na vitisho, alishikilia msimamo hana hatia.

Alidai mahakamani hapo kuwa baada ya mateso hyo alilazimika kukiri kuua katika maelezo ya onyo na kudai kuwa maelezo hayo yaliandikwa bila hiari yake na kuomba mahakama kumuachia huru kwani hana hatia.

Baada ya kusikiliza pande zote, Jaji alieleza imethibitika kuwa Qamara alikutwa amelala kando ya maiti ikiwa nusu uchi, ikiwa na michubuko shingoni na akivuja damu sehemu zake za siri, mazingira yanayothibitisha bila pingamizi kuwa sit u mshtakiwa alimbaka mtoto huyo, bali pia alimuua kwa kukusudia.

Related Posts