ATE YATAJA VIGEZO VIPYA TUZO YA MWAJIRI MPYA WA MWAKA 2024


Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waajiri Tanzania (ATE), akizungumza na waandishi wa habari kutangaza kuzinduliwa kwa tuzo ya Mwajiri Bora wa mwaka 2024. Hafla ya kuzinduliwa kwa tuzo hizo imefanyika leo Mei 30, 2024 katika ofisi za ATE zilizopo Mikocheni jijini Dar es Salaam.

Na Karama Kenyunko Michuzi Tv
CHAMA cha Waajiri Tanzania (ATE), kimeongeza vigezo vitatu vya utoaji tuzo ya mwajiri bora wa mwaka 2024 ikiwa pamoja na mwitikio dhidi ya ugonjwa wa ukimwi , utengenezaji ajira, pamoja na Afya na usalama mahala pa Kazi.

Hayo yamebainishwa leo Juni 30, 2024 na Mkurugenzi Mkuu wa ATE, Suzanne Ndomba-Doran jijini Dar es Salaam alipokuwa akitangaza kuzinduliwa kwa tuzo ya Mwajiri Bora wa mwaka 2024 inayotarajiwa kutolewa mwanzoni mwa mwezi Desemba mwaka huu.

Suzanne amesema kuwa ATE imeongeza vipengele hivyo vitatu lengo likiwa ni kutoa hamasa kwa waajiri kuendana na malengo ya serikali na yale Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs).

Amevitaja vipengele hivyo vipya vitakavyoshindaniwa ni afya na usalama mahala pa kazi, Mwitikio dhidi ya VVU na UKIMWI na utengenezaji wa ajira ambavyo vinapelekea vigezo hivyo kufikia 17.

“Katika kigezo cha Mwitikio dhidi ya VVU na Ukimwi lengo kuunga mkono jitihada malengo ya serikali yetu kupambana dhidi ya maambukizi ya virusi  vya UKIMWI sambamba na kupinga unyanyapaa na vifo . Pia ATE tunatekeleza agizo la Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alilotoa hotuba yake aliyoitoa kwenye utoaji Tuzo za mwaka jana”

Suzanne amesema kuwa tuzo ya utengenezaji ajira ATE imelenga kuwatunuku waajiri wanaounga mkono malengo ya maendeleo endelevu (SDGs).

“Utengenezaji ajira ni muhimu katika kukabiliana na umasikini na tunasisitiza ajira hizo ziwe zenye staha”

Pia kwenye kigezo cha Tuzo ya Afya na Usalama mahala pa Kazi ni kutekeleza mkataba wa kimataifa Na 155, wa Shirika la Kazi Duniani (ILO).

Suzzane amevitaja vipengele vya tuzo kwa mwaka huu kuwa ni pamoja na tuzo ya Ubora katika usimamizi wa Rasilimali watu, tuzo ya Utofautishwaji na Ushirikishwaji, tuzo ya masuala ya uongozi na mtawala, tuzo ya ukuzaji vipaji, tuzo ya wajibu wa taasisi kwa jamii, tuzo ya ushirikishwaji wa mwajiri, tuzo ya usimamizi ya utendaji, tuzo ya mafunzo ya ujuzi na uanagenzi , tuzo ya maudhui ya ndani, tuzo ya ubora , uzalishaji na ubunifu, tuzo ya mabadiliko ya tabianchi, tuzo ya namna ambayo waajiri wanakabiliana na majanga na kuathiri kazi na ajira.

Nyingine tuzo ya usawa wa kijinsi na usawa katika maeneo ya kazi , tuzo ya kampuni inayofuata miongozo na matakwa ya kisheria .

Tuzo nyingine ni ile ya mshindi wa jumla , Tuzo zinazotolewa kulingana na ukubwa wa kampani, tuzo ya mwajiri bora katika sekta binafsi, tuzo ya mwajiri katika sekta ya umma, tuzo ya masharika yasiyo ya kiserikali, tuzo ya mwajiri bora mzawa, tuzo ya mwajiri anayeimarika, na klabu inayofanya vizuri.

Suzanne amewaasa wanachama wao kutembelea tovuti ya Tuzo ya Mwajiri bora ambayo itawaongoza mpaka kwenye dodoso lililoko mtandaoni na makampuni shiriki yanaombwa kuwasilisha madodoso mawili moja likiwa limejazwa na uongozi au Mkurugenzi Mkuu au kitengo cha usimamizi wa rasilimali watu na jingine lililojazwa na mwajiriwa wa kawaida au mwakilishi wa chama cha wafanyakazi.

Amesema kuwa ATE itashirikiana na kampuni ya Auditax katika mchakato wa kumpata mwajiri bora.

Related Posts