Mkuu wa Mkoa wa Songwe Daniel Chongolo amempongeza Mbunge wa Songwe, Phillipo Mulugo (CCM) kwa kukicha posho za vikao vya Bunge la bajeti linaloendelea jijini Dodoma na kuunga naye katika ziara ya siku tatu ya kusikiliza na kutatua kero za wananchi. Anaripoti Ibrahim Yassin, Songwe… (endelea).
Hayo yamejiri wakati Chongolo aliyetua mkoani humo hivi karibuni, kuendelea na ziara ya kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo na kusikiliza kero za wananchi katika Wilaya ya Momba, Ileje na Songwe.
Katika ziara hiyo, Chongolo amekagua miradi ya barabara ya Mkwajuni, mradi wa maji Ngwara na taa za barabarani- Iseche. Pia ametembelea kampuni ya uchimbaji madini Shanta Mining, kampuni ya utafiti wa madini madini Rare Earth Elements katika kata ya Ngwala, miradi ya afya na elimu pamoja na Umeme.
Akizungumza na wananchi wa jimbo hilo, Chongolo alimpongeza mbunge huyo na kuwaeleza wananchi hawakukosea kumchagua Mulugo kwani amedhihirisha kuwa mbunge anayewajali wapiga kura wake.
‘’Mulugo anaakili sana, anajua waliompeleka bungeni ni ninyi ndiyo maana kaona aungane nami kuzunguka jimbo zima kusikiliza kero zenu. Mwenyekiti wa halmashauri Abraham Sambira ni mtu na nusu, kazi zilizofanyika kwenye jimbo hili zimeleta tija kwa wananchi… hongereni sana,’’ amesema Chongolo.
Aidha, amesema asilimia 96 ya miradi iliyokaguliwa imekamilika kwa ufanisi mkubwa isipokuwa mradi wa maji Ngwala ambao ulisitishwa kwa sababu ya ubabaishaji wa mkandarasi.
Akizungumza jana Jumatano kwa niaba ya wananchi wenzie, Chitanda Mathew mkazi wa Songwe amesema aliwapongeza viongozi wake ambao ni mkurugenzi mtendaji, Mbunge na mwenyekiti wa halmashauri kwa kujenga ushirikiano bora kutatua kero za wananchi wao.
“Bunge linaendelea, lakini tunafarijika kuona Mbunge wetu ameambatana mkuu wa mkoa na kamati ya usalama wakiwemo wataalam wa idara zote za mkoa na wilayani kuja kushiriki katika zoezi hili, maswali yote yamejibiwa na changamoto zetu zimetatuliwa na zingine zinafanyiwa kazi,’’ amesema Mathew.
Kwa upange wake Mbunge Mulugo amesema ziara hiyo ni muhimu kuliko posho za vikao vya Bunge hivyo ameamua kusitisha vikao kwa siku tatu ili aungane na mkuu wa mkoa kusikiliza kero na kutoa maombi mbalimbali ili miradi izidi kutekelezwa kwenye jimbo lake.