Daladala 20 kuongeza nguvu Barabara ya Morogoro

Dar es Salaam. Ili kukabiliana na tatizo la usafiri kwa wakazi wa Mbezi wanaokwenda maeneo ya Mjini kupitia Barabara ya Morogoro, Mamlaka ya Udhibiti  Usafiri Ardhini(Latra), imeruhusu kurejeshwa kwa daladala 20.

Daladala hizo ambazo kila moja inapaswa kuwa na uwezo wa kubeba abiria 40, zitawawezesha wakazi wa Mbezi na maeneo ya jirani kupata usafiri kwa urahisi baada ya kuwepo kwa kilio cha muda mrefu cha changamoto ya usafiri wa mabasi yaendayo haraka.

Katika malalamiko ya wakazi wa maeneo hayo, wamesema imekuwa ikiwalazimu kuyasubiri mabasi hayo muda mrefu vituoni hivyo kuchelewa katika shughuli zao za kila siku huku yale yanayofanya safari zake Mbezi  kwenda Kivukoni na Mbezi kwenda Gerezani ndio yameonekana kuwa na changamoto zaidi hasa asubuhi na jioni.

Mwaka 2016, daladala zaidi ya 8000 zilizokuwa zikitoa huduma katika barabara hiyo ziliondolewa.

Akizungumza na Mwananchi Digital, leo Alhamisi Mei 30 2024 Mkurugenzi wa Kitengo cha Mawasiliano na Mahusiano wa Latra, Salum Pazzi amesema wameamua kuziita daladala hizo kutokana na kuwepo kwa uhitaji mkubwa wa usafiri.

“Tunajua wenzetu wa mwendokasi wanatoa huduma katika barabara hiyo, Lakini mabasi hayatoshi, hivyo tumeona turuhusu daladala hizi chache ili kuwasaidia wananchi kuondokana na adha ya usafiri.

“Tunajua mtu akitoka Mbezi na kufika Mnazi Mmoja ni rahisi kwake kwenda Posta na ni rahisi pia kwenda Gerezani kwa kuwa pale kuna magari mengi yanayolekea maeneo hayo,”amesema Pazzi.

Hata hivyo, amesema vibali hivi ni vya muda wa mwaka mmoja kwa kuwa wanajua wakati wowote kuanzia sasa mabasi ya mwendokasi yataongezwa.

Sambamba na hilo amesema pia wametoa kibali cha kuongezwa daladala 10 kutoka Mbezi Mnazi Mmoja zinazopitia Barabara ya Korogwe, Kwa Mkuwa, Mabibo zenye uwezo wa kubeba abiria kuanzia 25.

Baadhi ya wananchi wakizungumzia hatua hiyo akiwamo Linda Francis mkazi wa Mbezi, amesema hiyo ni habari njema kwao kwa kuwa usafiri wa mwendokasi kwa sasa umekuwa ni mateso kwao.

Linda amesema ukiacha kukaa muda mrefu kuyasubiri vituoni, lakini wamekuwa wakijazana ndani ya mabasi hayo jambo linalohatarisha afya zao na usalama wao.

Nora Chami, amesema haoni kama daladala zilizoongezwa zitatosha na kupendekeza zingeongezwa 50 kutokana na ukubwa wa tatizo la usafiri.

“Mbezi ya mwaka 2016 wakati mradi huu wa mwendokasi unaanza ni tofauti na sasa, kumekuwepo na ongezeko la watu ikijumuisha na maeneo ya jirani kama Kibamba, Msumi, ambao wote hawa wakimwaga pale kituo cha Mbezi wanategemea usafiri wa mwendokasi.

“Hivyo kuweka daladalada 20 tu sidhani kama kutasaidia kupunguza tatizo hilo,’amesema Nora.

Frank Ulomi, amesema:“Hii Barabara ya Morogoro kutokana na uwepo wa abiria wengi huenda hawa wenzetu ikafika saa 12 wakawa wamefikisha hesabu zao na kwenda kulaza magari, tunaomba Latra isimamie hili kwa umakini ili kuona tija yake katika kuzirejesha,”amesema Ulomi.

Kutokana na hatua hiyo, Mwananchi pia ilitaka kujua kutoka kwa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (Dart), ni lini mabasi mapya yataletwa ili kuondoa changamoto hiyo ya usafiri kwa mabasi hayo.

Mtendaji Mkuu Dart, Dk Athuman Kihamia, amesema mchakato bado unaendelea.

 Wamiliki wa daladala, akiwamo, Ghalib Mohammed amesema haoni hilo kama lina tija na kueleza kuwa kitendo cha kutoa leseni mwaka mmoja sio sawa, lakini pia wanalipwa nini baada ya mwenye njia yake kuleta mabasi.

“Mbaya zaidi ni kwamba wanataka magari mapya, hivyo ni kumpa maumivu mmiliki ambaye ataingia mkopo kuagiza magari hayo, halafu mwisho wa siku ataondolewa barabarani.”

Ushauri wake mabasi hayo yapelekwe kufanya kazi kwenye barabara za mlisho za mwendokasi ili nao waweze kujikongoja kulipa mikopo waliyoagizia magari hayo na yapewe leseni za kuanzia miaka mitano na kuendelea ili kuweza kurudisha gharama zao.

Wakati Mohammed akisema hivyo, Katibu wa Umoja wa wamiliki wa Daladala Mkoa wa Dar es Salaam (Darcoboa), Shifwaya Lema amepongeza hatua hiyo na kueleza kikubwa ni wananchi kuweza kupata usafiri huku akiwaomba wanachama wao kuchangamkia fursa hiyo.

Related Posts