Hakikisha mipango yako iendane na hali ya uchumi wako

Huwezi kununua gari kwa sasa, aliongea Cath huku akiwa amekaza macho bila kuyapepesa. Siwezi kushindwa kununua gari wakati ninafanya kazi na ninalipwa mshahara, akajibu Juma.

Mipango niliyonayo mimi ni kukopa pesa na kununua gari, unataka niwe na mipango gani mingine? Juma alilalamika. Nisikilize rafiki, nakubaliana na wewe kuhusu kununua gari, lakini siwezi kukushauri ununue kwa kutumia mkopo.

Nitapataje gari wakati tayari nina mikopo ya nyumba na elimu ya juu ambayo nitailipa kwa muda mrefu? Akauliza Juma kwa kukata tamaa. Lengo langu ni kukutoa katika mikopo hiyo. Huwezi kutoka kwenye shimo kwa kuchimba shimo zaidi, akaongea Cath huku akimtazama Juma.

Gari ulitakalo utalipata ila kwa njia nyingine. Tofauti na nyumba na elimu ulivyopata kwa mkopo, gari utanunua kwa pesa yako, Cath akaongeza. Nitapata wapi pesa hiyo wakati makato ya mikopo ni makubwa na kiasi kinachobaki hakikidhi japo matumizi yangu ya mwezi?

Unahitaji gari la shilingi ngapi? Cath akamuuliza. Milioni kumi na tano, Juma akajibu. Sasa tufanye unalihitaji gari hilo baada ya mwaka mmoja, akaongea Cath. Kupata milioni 15 kwa mwaka mmoja unatakiwa kuweka akiba ya Sh1.25 milioni kila mwezi, hii itakutaka uweke akiba ya Sh312, 500 kila wiki au Sh44,643 kwwa siku.

Ili uweze kupata kiasi hicho unaweza kufanya yafuatayo; unaweza kuamua kufanya kazi hiyo zaidi, unaweza kupunguza matumizi ya kila siku ama unaweza kutafuta kazi nyingine ya ziada.

Kama huoni uwezekano wa wewe kupata kiasi hicho cha akiba kwa siku, unatakiwa kutambua kuwa lengo lako la kupata gari kwa mwaka mmoja halitekelezeki. Unatakiwa kufanya maamuzi ya kubadilisha lengo lako.

Ninabadilishaje lengo, unataka niache kununua gari? Juma akauliza. Hapana sio lengo langu, lengo langu ni kuwa kununua gari kwa akiba unayoweza kuiweka.

Kama lengo la milioni kumi na tano kwa mwaka huliwezi, unaweza kuamua kununua gari la bei rahisi zaidi. Kwa upande wa pili unaweza kuamua kuongeza muda wa kununua gari badala ya mwaka mmoja ukawa miaka miwili.

Njia hii itakusaidia kutoongeza deni jipya katika mlolongo wako wa mikopo. Utapata gari ukiwa hujaongeza kuchimba shimo ambalo umefukiwa, alimaliza Cath.

Related Posts