Dar es Salaam. Mahakama ya Rufani imeshindwa kuendelea kusikiliza rufaa ya kupinga uteuzi wa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere kutokana na kukosekana kumbukumbu za rufaa.
Rufaa hiyo ilikatwa na aliyekuwa Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe akipinga sehemu ya hukumu ya Mahakama Kuu iliyokataa maombi na hoja zake za kubatilisha uteuzi wa Kichere kushika wadhifa huo.
Zitto anapinga hukumu ya Mahakama Kuu katika kesi ya Kikatiba aliyoifungua dhidi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), CAG Kichere na aliyekuwa CAG kabla ya Kichere, Profesa Mussa Assad.
Mahakama Kuu katika hukumu iliamua kuondolewa kwa Profesa Assad katika wadhifa huo kulikuwa ni batili, kwa kuwa aliondolewa kabla ya muda wake wa kikatiba, lakini ikakataa kubatilisha uteuzi wa Kichere.
Zitto akikata rufaa kupinga sehemu ya hukumu hiyo, Serikali ilikata rufaa kinzani kupinga hukumu yote ya Mahakama Kuu.
Rufaa hizo zilipangwa kusikilizwa leo Mei 30, 2024 na jopo la majaji watano wa Mahakama ya Rufani likiongozwa na Ferdinand Wambali, akishirikiana na Barke Sehel, Panterine Kente, Dk Mary Levira na Mustafa Ismail.
Kabla ya kuanza kusikiliwa, Jaji Wambali aliibua hoja ya kukosekana baadhi ya nyaraka muhimu katika vitabu vya kumbukumbu ya rufaa na kasoro ya taarifa katika baadhi ya nyaraka zinazohusu mwenendo wa kesi hiyo Mahakama Kuu, akihoji mahali zilipo.
Jaji Wambali ameitaja nyaraka hiyo kuwa ni uamuzi wa Mahakama Kuu kumruhusu mdai (Zitto) kuongezewa muda wa kuwapatia nyaraka za kesi wadaiwa baada ya kuifungua.
Amesema Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufani ni Mahakama za kumbukumbu, basi nyaraka hizo zinapaswa kuwepo na ziwe na taarifa sahihi ili kuakisi kilichofanyika katika kila hatua na kuweka kumbukumbu sawa.
Mahakama pia imeibua kasoro ya maudhui katika baadhi ya nyaraka hizo ikiwamo kutaja kimakosa namba ya kesi ya msingi, ambayo kwenye hukumu inayokatiwa rufaa imetajwa kama hukumu ya kesi namba 8 ya mwaka 2022 badala ya namba 8 ya mwaka 2020.
Mawakili wa Zitto, Dk Rugemeleza Nshala na Nyaronyo Kicheere na mawakili wa Serikali, Hangi Changa na Daniel Nyakia wamekiri kutokuonekana kwa nyaraka hizo.
Wakili Fulgence Massawe anayemwakilisha Profesa Assad, ambaye ni mjibu rufaa wa nne, ameieleza Mahakama hata nyaraka za mteja wake alizoziwasilisha Mahakama Kuu hazionekani kwenye kumbukumbu za rufaa hiyo.
Wakili Changa amesema katika rufaa kinzani kuna kasoro katika mwaka wa kesi inayokatiwa rufaa akibainisha imetajwa kama kesi namba 8 ya mwaka 2022 badala ya kesi namba 8 ya mwaka 2020.
Amedai walinukuu kosa hilo kama ilivyoandikwa kimakosa kwenye hukumu, na akaiomba Mahakama ruhusa waweze kuwasilisha rufaa kinzani iliyofanyiwa marekebisho ya kasoro hiyo.
Wakili Massawe amezitaja nyaraka hizo kuwa ni majibu ya Profesa Assad (aliyekuwa mdaiwa wa nne katika kesi ya msingi) dhidi ya hati ya madai, kiapo kinzani na maelezo yake ya maandishi kuhusu hoja za kesi hiyo na kiapo kinzani.
Kutokana na kasoro hizo Mahakama imeshindwa kuendelea na usikilizwaji wa rufaa hiyo.
Baada ya majadiliano baina ya Mahakama na mawakili wa pande zote, Mahakama imeahirisha usikilizwaji wa rufaa hiyo mpaka tarehe nyingine itakayopangwa katika kikao kijacho.
Uamuzi huo umefikiwa ili kutoa nafasi kwa mawakili kuzitafuta na kuziwasilisha mahakamani nyaraka hizo kuweka kumbukumbu sawa na kurekebisha kasoro zilizobainika.
Mahakama imetoa siku 60 kuwasilisha mahakamani nyaraka hizo na kufanya marekebisho hayo.
Pia, imeelekeza hati ya sababu za rufaa za Zitto ifanyiwe marekebisho kubainisha sababu zinazoonyesha moja kwa moja kile kinachopingwa, ili kuendana na matakwa ya Kanuni ya 93 ya Kanuni za Mahakama ya Rufani.
“Ushauri wetu ni kwamba shirikianeni na ofisi ya msajili (wa Mahakama Kuu) kupata nyaraka zinazokosekana na marekebisho, hasa namba ya kesi kwenye hukumu ili kuwahisha. Tusichukue muda mrefu kwa vitu ambavyo vinaweza kurekebishwa kwa muda mfupi,” amesema Jaji Wambali.
Amesema wametoa amri hizo kwa mdomo na kwamba, ya maandishi itatolewa kesho Mei 31.
Katika kesi namba 8 ya mwaka 2020, Zitto alikuwa akipinga Profesa Assad kuondolewa katika wadhifa huo kabla ya muda wake.
Profesa Assad aliteuliwa kushika wadhifa huo Novemba 5, 2014 na alihudumu katika nafasi hiyo kwa miaka mitano hadi Novemba 4, 2019, baada ya aliyekuwa Rais, hayati John Magufuli kumteua Kichere kushika wadhifa huo.
Kutokana na hilo, Zitto aliiomba Mahakama itamke kuwa kifungu cha 6(1) cha Sheria ya Ukaguzi, ni batili kwa kuwa kinakinzana na Katiba.
Pia, aliiomba itamke kuwa kuondolewa kwa Profesa Assad kabla ya kutimiza umri wa kustaafu ni batili na uteuzi wa Kichere kuwa CAG mpya ilikuwa batili.
Alidai Ibara ya 144(1) ya Katiba ambayo inaeleza kuwa CAG atatumikia wadhifa huo mpaka umri wake wa kustaafu, yaani miaka 60 Kikatiba au 65 kwa mujibu wa kifungu 62(a) cha sheria hiyo ilikiukwa.
Mahakama Kuu katika hukumu ya Desemba 5, 2022 iliyotolewa na majaji watatu, Dk Benhajj Masoud (kiongozi wa jopo) Juliana Masabo na Edwin Kakolaki ilibatilisha uamuzi wa kuondolewa kwa Profesa Assad katika wadhifa huo kabla ya umri wake wa kustaafu.
Ilikubaliana na hoja za Zitto kuwa kifungu cha 6(1) cha Sheria ya Ukaguzi kuweka mihula ya miaka mitano ya utumishi wa CAG ni batili kwa kuwa kinakinzana na Ibara ya 144 ya Katiba.
Ilisema wakati kifungu hicho kinaweka mihula ya utumishi wa CAG, Katiba inazungumzia umri wa kustaafu na si mihula.
Hivyo, ilisema kuondolewa kwa Profesa Assad kabla ya kufikisha umri wa kustaafu kulikuwa batili.
Hata hivyo, ilikataa maombi ya Zitto kutaka uteuzi wa Kichere utangazwe ni batili, ikisema uteuzi wake ni halali kwa kuwa aliteuliwa kwa mujibu wa Katiba na anazo sifa za kuwa CAG.
Mahakama Kuu ilionya kukubali maombi hayo ya Zitto kutoa amri kubatilisha uteuzi wa Kichere kungesababisha ombwe katika nafasi hiyo na kuibua mgogoro mwingine wa Kikatiba kwa kuwa, tayari Kichere alishatekeleza majukumu yake ikiwamo kufanya ukaguzi na kuwasilisha taarifa mbalimbali za ukaguzi.