Dodoma. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewaondoa hofu Watanzania waliomiliki hati za kimila akisema zipo kisheria kama zinazotolewa na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Majaliwa ametoa kauli hiyo leo Alhamisi Mei 30, 2024 wakati wa maswali ya hapo kwa papo alipokuwa akijibu swali la mbunge wa Busekelo, Atupele Mwakibete.
Mbunge huyo amesema hati za kimila zimekuwa hazidhaminiwi na benki hivyo wananchi wamekuwa wakizungushwa wakati wanaomba kupatiwa mikopo.
“Hivyo wananachi wa vijijini wameendelea kuwa masikini kwa kutokopesheka na tatizo hilo limetokana na Sheria ya Ardhi namba Tano yam waka 1999,” amesema.
Amehoji Serikali ina mkakati gani wa kuhakikishia wananchi wa vijiji wanapata hati kama wanazopata wa mijini ili waweze kudhaminiwa na mabenki kwa kubadilisha sheria hiyo namba tano.
Akijibu swali hilo, Majaliwa amesema kwa kwa mujibu wa sheria za ndani ya nchi hati hutolewa na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na kuna hati za kimila ambazo zote zinatambulika kisheria.
“Hati zote zinazotoa fursa ya mwenye hati hizo kupata mikopo kwenye taasisi zote za kifedha. Inawezeka kuna taasisi ambazo hazikubali kwa sababu ya matakwa yao tu,”amesema.
Ametoa wito kwa taasisi zote za kifedha ambazo zimeridhia kufanya kazi nchini kuendelea kutumia na kutoa fursa kwa watu wenye hati za kimila na hati zinazotolewa na wizara ya ardhi kwa kuwa ni hati halali zinazotambulika.
Amesema hati hizo zinatoa fursa kwa mmliki wa ardhi nchini kupata stahiki ya mikopo na kuwataka wananchi kuendelea kuziona kuwa ni hati kamili.
Katika hatua nyingine; mbunge wa Biharamulo, Ezra Chiwelesa amesema kutoka Bandari ya Dar es Salaam kuelekea katika nchi za Burundi na Rwanda kumekuwa na vituo vya ukaguzi 44 na mizani za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) zaidi ya tatu lakini mizani zaidi ya nane kutokea Dar es Salaam hadi Lusumo.
“Serikali kupunguza trans time na kuwasaidia wasafirishaji wakaona kuwa ni mzigo mkubwa, ilianza kujenga vituo vya ukaguzi wa pamoja, kulikuwa na ujenzi ufanyike Manyoni na Nyakanazi. Lakini kuna baadhi ya vituo bado havijajengwa na ujenzi wake ulisimama,”amesema na kuongeza.
Mbunge huyo amehoji nini kauli ya Serikali kukamilisha ujenzi wa vituo hivyo ili hatimaye Bandari ya Dar es Salaam iweze kufanya kazi katika viwango ambavyo Serikali ilitarajia.
Akijibu swali hilo, Majaliwa amesema uko mpango wa kuimarisha ukaguzi na mapato kupitia mizigo inayopitia Bandari ya Dar es Salaam kwa kujenga vituo vya ukaguzi kimkakati.
Amesema ni lazima kuimarisha vituo vya ukaguzi na usalama hata maeneo yanayoingia na kutoka kwa mizigo nchini na kwamba kazi ya ujenzi wa vituo hivyo inaendelea.
“Mpango mkakati upo na sasa tumeamua tunajenga katika umbali ambao hauwezi kuleta usumbufu kwa wasafirishaji kwa kukaguliwa kila mahali wanapopita,”amesema.
Majaliwa amehamasisha mataifa ya nje kutumia Bandari ya Dar es Salaam na bandari nyingine za Tanga na Mtwara kwa ajili ya kusafirisha na kupokea mizigo yao.
Amesema Serikali inaendelea kuziimarisha na kujenga Bandari ya Bagamoyo na korido zote ili kuhakikisha usalama wa nchi.