Wakati Israel ikizidisha mashambulizi yake huko Rafah, Msemaji wa Jeshi la nchi hiyo Daniel Hagari ametangaza kuwa Israel imechukua kile alichokiita “udhibiti wa kiutendaji” wa eneo dogo la mpakani kati ya Palestina na Misri, na kwamba wamegundua karibu mahandaki yapatayo 20.
Misri, ambayo imekuwa mpatanishi wa muda mrefu katika mzozo huo na kwa sasa imekuwa ikidhihirisha wazi ukosoaji wake wa operesheni ya Israel huko Gaza, imetupilia mbali madai ya uwepo wa mahandaki hayo yanayodaiwa kutumiwa kusafirisha bidhaa za magendo.
Jeshi la Israel ambalo limeapa kulitokomeza kabisa kundi la Hamas, lilianzisha operesheni yake mjini Rafah mwanzoni mwa mwezi huu wa Mei licha ya pingamizi la kimataifa kuhusu hatima ya raia wa Palestina waliokimbilia eneo hilo.
Mashambulizi ya mwishoni mwa juma ambayo yalisababisha vifo vya watu kadhaa katika kambi ya wakimbizi wa ndani, yalizua wimbi ljipya la lawama kwa Israel ikiwa ni pamoja na kampeni kubwa kwenye mitandao ya kijamii ambayo mojawapo ilikuwa na kauli mbiu ya “Macho Yote yaelekezwa Rafah” ambayo inaendelea kuchapishwa na mamilioni ya watumiaji wa mitandao hiyo.
Soma pia: Israel kuendeleza vita Gaza hadi mwishoni mwa mwaka 2024
Na kwenye Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu, Israel imesema wanajeshi wake wawili wameuliwa katika shambulio la kugongwa na gari katika eneo ambalo vikosi vya Tel-Aviv vimekuwa vikiendesha operesheni kadhaa za kupambana na kile wanachodai ni wanamgambo. Tangu kuanza kwa vita vya Gaza Oktoba 7, inakadiriwa kuwa Wapalestina 500 wameuawa eneo hilo.
Harakati za kidiplomasia pia zinaendelea
Rais Xi Jinping wa China ametoa wito hivi leo wa kuitishwa kwa mkutano wa amani kuhusu vita kati ya Israel na Hamas, alipokuwa akiwahutubia viongozi wa nchi za Kiarabu kwenye kongamano linalolenga kuimarisha mahusiano kati ya Beijing na nchi hizo za kiarabu.
Wiki hii Xi amewakaribisha Rais wa Misri Abdel Fattah al-Sisi, Rais wa Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) Sheikh Mohamed bin Zayed Al Nahyan, na viongozi wengine kadhaa wa Kiarabu. Akihutubia mkutano huo rais Xi amesema:
“Vita havipaswi kuendelea kwa muda usiojulikana. Haki haipaswi kukosekana milele. Kujitolea kwa kutafuta suluhisho la mataifa mawili hakupaswi kuyumbishwa kwa hiari.”
Soma pia:Rais wa China ajiandaa kuzungumza na viongozi wa mataifa ya kiarabu mjini Beijing
China ambayo imekuwa ikilenga kutanua ushawishi wake katika eneo la Mashariki ya Kati katika miaka ya hivi karibuni, inajinadi kama mshirika asiyeegemea upande wowote katika mzozo kati ya Israel na mamlaka ya Palestina kuliko mpinzani wake Marekani ambayo imedhihirisha kuiunga mkono Israel. Beijing imekuwa pia ikitetea uwepo wa suluhu la mataifa mawili na wakati huohuo ikidumisha uhusiano mzuri na Israel.
Vyanzo: Mashirika