Mrithi wa Dube apatikana Azam FC

AZAM FC imepania. Siku chache baada ya kumtambulisha kiungo, Ever Meza, klabu hiyo imekamilisha dili jingine la kumsajili mshambuliaji mpya, Jhonier Blanco kutoka klabu ya Aguilas Doradas inayoshiriki Ligi Kuu ya Colombia.

Straika huyo (24) amesaini mkataba wa miaka minne kuitumikia klabu hiyo kuanzia msimu 2024 hadi 2028.

Huo unakuwa usajili wa nne kwa Azam kuufanya kwa wachezaji wa kigeni kwani kabla ya Ever Meza, hivi karibuni ilimtambulisha pia kiungo mshambuliaji, Frank Tiesse na beki wa kati Yoro Mamadou Diaby wote raia wa Mali wakitokea Stade Malien de Bamako.

Usajili wa straika huyo mpya kutoka Colombia unatazamwa kuwa mbadala wa Mzimbabwe Prince Dube aliyetimka kikosini hapo. Dube ameisusa Azam katikati ya msimu akidai amemaliza mkataba, huku akihusishwa na klabu ya Yanga na hivi karibuni alikuwa na kesi TFF dhidi ya viongozi wa klabu hiyo.

Taarifa iliyotolewa kwenye mitandano ya kijamii ya timu hiyo ilisomeka: “Tunayo furaha kutangaza kwamba tumekamilisha uhamisho wa mshambuliaji raia wa Colombia, Jhonier Blanco, kutoka klabu ya Aguilas Doradas ya mji wa Rionegro, inayoshiriki Ligi Kuu ya Colombia aliyesaini mkataba wa miaka minne.”

Kabla ya kujiunga na Azam, straika huyo alichezea klabu mbalimbali ikiwemo Club Deportivo Estudiantil na Fortaleza za nchini kwao na sasa anaungana na Wacolombia wenzake waliomtangulia mapema klabuni akiwamo Ever Meza, beki Yeison Fuentes na mshambuliaji aliyeingia dirisha dogo, Franklin Navarro.

Related Posts