Msigwa afunguka baada ya kuangushwa na Sugu

ALIYEKUWA Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Kanda ya Nyasa, Mchungaji Peter Msigwa, amempongea Joseph Mbilinyi (Sugu) kwa kichaguliwa kurithi mikoba yake, katika uchaguzi uliofanyika Jana tarehe 29 Mei 2024. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam…(endelea).

Akizungumza baada ya matokeo hayo kutangazwa jana Jumatano, Msigwa amesema siasa ni mchezo wa kuingia na kutoka na kwamba thamani yake itaendelea kubaki hata kama sio Mwenyekiti wa Nyasa, kutokana na kazi kubwa aliyoifanya.

Mchungaji Peter Msigwa

“Niwapongeze kwa maamuzi yenu na Mimi ni mwanademokraisa ninayapokea na sikuingia kwenye chama hiki kwa sababu niwe kiongozi, kimsingi hiki ni chama cha siasa thamani yangu haitegemei cheo chochote cha siasa, thamani yangu ipo,” alisema Msigwa

Msigwa aliwataka wanachadema wa Nyasa kuendelea kushirikiana naye katika kazi za ujenzi wa Chama.

Naye Sugu aliwataka wanachama wa Chadema Kanda ya Nyasa kuvunja makundi yao ya uchaguzi, bali wabaki wamoja ili kukijenga chama hicho kuelekea chaguzi zijazo.

“Kazi yangu kubwa ya kwanza ni kuwaunganisha na kukiunganisha chama na kwa maana hiyo jiwambie kuanzia leo tutaanza kufanya kazi kwa pamoja hatutarudi nyuma. Kila mtu awe tayari tuna majukumu hapo mbele, chaguzi zinakuwa na mambo mengi kelele nyingi kurushiana maneno kidogo naomba hayo yote tuachane nayo,” alisema Sugu na kuongeza:

“Zile nguvu tulizokuwa tunatumia katika haya mambo  tuachane na migongano ya uchaguzi tujiandae na majukumu yaliyokuwepo mbele kuna uchaguzi wa Serikali za mitaa na uchaguzi mkuu unakuja mwakani.”

Related Posts