Necta yafuta maswali ya kuchagua hisabati mitihani shule za msingi

Serikali inazidi kufanyia kazi maoni ya wadau wa elimu kwa lengo  la kuboresha mfumo wa elimu nchini.

Sasa  imetangaza kuachana na mfumo wa kutahini somo la hisabati katika mtihani wa kumaliza darasa la saba,  kwa kutumia utaratibu wa maswali ya kuchagua.

Tamko hilo limetolewa leo Mei 30 jijini Tanga na Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania (Necta),  Dk Said Mohamed, alipokuwa  akiwasilisha  taarifa ya tathmini ya ujifunzaji na ufaulu wa wanafunzi  na kusema kuwa mfumo huo kwa baadaye utahusu pia baadhi ya masomo ya sekondari.

Amesema mtihani wa hisabati kwa shule za msingi mwaka huui, hautakuwa na maswali ya kuchagua kama ilivyozoeleka kwa miaka ya nyuma.

Amesema mafunzo mbalimbali yamekuwa yakiendelea kwa wadau husika  na mafunzo yanaendelea,lengo likiwa ni kuboresha ufaulu,hivyo utaratibu huo kwa  baadaye utafanyika hata kwa baadhi ya masomo ya sekondari.

Ametaja masomo ambayo baadaye yanatarajiwa kuachana na mfumo wa maswali ya kuchagua ni biolojia, Kiingereza na Fizikia.

“Mtihani wa hesabu  hautakuwa wa multiple choice (maswali ya kuchagua) kuanzia mwaka huu. Tunashukuru wadau wamepokea mfumo huo na mafunzo mbalimbali yamekuwa yakiendelea, kwa hivyo tusaidiane kwa pamoja kuhakikisha kwamba tunaliwezesha hilo”, amesema Dk Mohamed.

Necta ilibadili mfumo wa kutahini hisabati kutoka ule wa kukotoa hadi wa maswali ya kuchagua mwaka 2018, hatua iliyozua mjadala mzito wa kitaifa.

Wadau walikosoa mfumo huo   wakisema ulikuwa ukitoa fursa kwa watahiniwa kubahatisha  na kupatia majibu, na hivyo hata wasiokuwa na uwezo waliweza kufaulu na kuendelea na masomo ya sekondari.

Meneja Programu wa Mtandao wa Elimu Tanzania (TenMet) Nicodemus Shauri,  amesema suala hilo ni jambo jema kwa kuwa mwanafunzi anapaswa kuonyesha njia anayotumia kupata jibu badala ya kubahatisha..

“Mtalaa wa sasa unazungumzia umahiri sasa mwanafunzi anawezaje asionyeshe njia halafu akafaulu, itakuwa ni kupingana na mtalaa ambao ndio muongozo wenyewe,”amesema Shauri.

Amebainisha kuwa kuanzishwa kwa mfumo huo, lengo lilikuwa  ni kuwarahisishia walimu usahihishaji lakini kimsingi mwanafunzi anapaswa kuonyesha njia ya  namna ya  kupata  jibu.

Naye mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Udsm) Faraja Kristomus amesema wamekuwa  wakipigia kelele mfumo wa maswali ya kuchagua  kwa muda mrefu, akisema somo kama  hisabati linapaswa kufanywa kwa kukokotolewa.

“Kuondolewa kwa maswali ya kuchagua hilo ndilo litakalopima uhalisia wa somo na kwenye uelewa, ni jambo sahihi na kwa wakati sahihi kwani mfumo huo ulianzishwa mahususi kwa ajili ya kurahisisha usahihishaji,”amesema Dk Kristomus.

Related Posts