Ngoto ashinda nafasi ya uenyekiti Chadema Kanda ya Serengeti

Simiyu. Aliyekuwa Kaimu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Kanda ya Serengeti, Gimbi Masaba ameshindwa kutetea nafasi ya mwenyekiti wa kanda hiyo baada ya kupata kura 44 kati ya 89 huku, Lucas Ngoto aliyepata kura 45 kuibuka kidedea.

Akitangaza matokeo ya uchaguzi huo Jana usiku Mei 29, 2024, Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Grace Kiwelu amesema Ngoto ameshinda nafasi ya uenyekiti Kanda ya Serengeti inayojumuisha mikoa ya Shinyanga, Simiyu na Mara kwa asilimia 51 huku, Gimbi ambaye pia aliwahi kuwa mbunge wa viti maalumu wa chama hicho akipata asilimia 49.

Kiwelu amesema katika uchaguzi huo uliofanyika siku ya jana mkoani Shinyanga waliojisajiri kupigakura walikuwa 89 na hakukuwa na kura hata moja iliyoharibika.

“Idadi ya kura zilizopigwa ni 89 na hakuna kura iliyoharibika, Gimbi Masaba alipata kura 44 sawa na asilimia 49 na kwa upande wa Ngoto alipata kura 45 sawa na asilimia 51, hivyo namtangaza Ngoto kuwa Mwenyekiti wa Kanda ya Serengeti,” amesema.

Amesema uchaguzi huo ulitegemewa  kuhudhuliwa na wajumbe 120 wa kanda hiyo  walioshiriki katika Uchaguzi wa viongozi Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwaka huu na  Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika  Oktoba 2025.

Mwenyekiti mteule wa kanda hiyo, Lucas Ngoto alisema kuwa uchaguzi huo ni mpango mkakati wa kusimamisha chama kiweze kushika hatamu katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwaka 2025 akidai mbali na nafasi ya urais,  chama kimejipanga kuongeza idadi kubwa ya wabunge na madiwani katika mikoa yote ya kanda ya Serengeti.

“Uchaguzi huu umetupa taswira nzima ya kuelekea mipango na mikakati ya Uchaguzi Mkuu wa mwakani, tutajipanga kusimamisha wagombea wanaoukubalika na wataoweza kuleta mabadiliko kwa ngazi zote kuanzia ngazi ya mitaa na vijiji, madiwani, wabunge na ngazi ya urais,” amesema Ngoto.

Related Posts