Dar es Salaam. Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Jumanne Sagini ameitaka Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo (LST), kutoa mrejesho wa uwezo wa wanafunzi wanaowapokea.
Msingi wa kauli hiyo, ni kile alichodai kutoridhishwa na asilimia 59 ya ufaulu wa jumla wa wahitimu wa LST tangu ilipoanzishwa.
Tangu kuanzishwa kwa taasisi hiyo, Mkuu wa LST, Profesa Sist Mramba amesema wanafunzi 17,782 wamedahiliwa katika makundi 38 na kati yao 8,999 sawa na asilimia 59, wamefaulu na kuwa mawakili.
Kutokana na kiwango hicho cha waliofaulu, ambacho Sagini amesema ni kidogo, amesisitiza umuhimu wa LST kutoa mrejesho wa uhalisia wa uwezo wa wanafunzi inaowapokea.
Sagini ametoa kauli hiyo leo, Mei 30, 2024 katika kikao kazi na menejimenti ya LST kilichofanyika jijini, Dar es Salaam.
Amesema anatambua sababu ya kiwango hicho cha ufaulu si LST, bali ni namna wanafunzi anavyoandaliwa.
“Tunapaswa tujiulize kwa nini mfumo unasababisha wengi wafeli, najua hili sio la kwenu.
“Mnapaswa kuwasiliana na vyuo vinavyowaleta wanafunzi waangalie maeneo yenye changamoto na hili halitoshi kuwa la LST peke yenu nasi Wizara tutaliangalia,” amesema.
Sagini amesema amewahi kusikia malalamiko kuhusu ufaulu wa wanafunzi katika taasisi hiyo, akisisitiza si makosa ya LST.
Ingawa amesema LST haihusiki na changamoto hiyo ya ufaulu, amesisitiza umuhimu wa kubadili mitazamo ya wanafunzi inaowapokea.
Kutoka kuwa na fikra za kukariri, Sagini ameitaka LST iwajengee mtazamo kwamba katika taasisi hiyo wanajifunza maisha ya kitaaluma.
“Kama huko walikotoka walikuwa wanakariri na wanafaulu, wakifika hapa muwajenge kifikra kwamba wanajifunza namna ya kuwa mawakili hii ni tofauti na walikotoka,” ameeleza.
Aidha, amesema hatua ya taasisi hiyo kuanzisha programu ya wasaidizi wa kisheria itasaidia wananchi ambao aghalabu hupoteza haki kwa kutojua hatua sahihi za kisheria.
Mkuu wa taasisi hiyo, Profesa Mramba amesema mwaka huu taasisi hiyo, inatarajia kuanza kutoa mafunzo ya usaidizi wa kisheria ngazi ya stashahada.
Amesema huu ni mwaka wa 17 tangu taasisi hiyo ianzishwe na kwamba pamoja na wakufunzi wenye ajira ya kudumu, pia ina kanzidata na wakufunzi 80 wa muda.
Katika hatua nyingine, Profesa Mramba amesema taasisi hiyo imetekeleza hoja 22 kati ya 38 zilizopendekezwa na kamati iliyoongozwa na Dk Harrison Mwakyembe.
Kamati hiyo iliundwa Septemba mwaka jana na aliyekuwa Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Damas Ndumbaro kuangalia mwenendo wa ufaulu wa mtihani katika taasisi hiyo.
“Taasisi imezingatia hoja zilizotolewa na imefanyia kazi, kwa zile zinazopaswa kutekelezwa na taasisi. Hadi sasa tumetekeleza kwa asilimia 95,” amesema Profesa Mramba.