Kampala. Spika wa Bunge la Uganda, Anita Among ni miongoni mwa vigogo watano nchini humo walipigwa marufuku kuingia nchini Marekani kwa madai ya kuhusika na ufisadi na uvunjaji mkubwa wa haki za binadamu.
Taarifa iliyotolewa na Msemaji wa Idara ya Mambo ya Nje ya Marekani, Matthew Miller leo Mei 30, 2024 imesema, vigogo hao wanatuhumiwa kwa ufisadi mkubwa.
“Spika Anita Among anatambuliwa kutokana na ushiriki wake katika ufisadi mkubwa unaohusiana na uongozi wake wa Bunge la Uganda,” amesema.
Msemaji huyo amewataja pia Waziri wa zamani wa Masuala ya Karamoja, Mary Goretti Kitutu, Waziri wa zamani wa Masuala ya Karamoja Agnes Nandutu, na Waziri wa Nchi wa Fedha Amos Lugolobi kwa tuhuma za kushiriki katika ufisadi wa ubadhirifu wa mali za umma.
“Maafisa wote wanne walitumia nyadhifa zao za umma kwa manufaa yao binafsi kwa gharama za raia wa Uganda,” amesema.
Amemtaja pia, Peter Elwelu, Naibu wa zamani wa Mkuu wa Vikosi vya Ulinzi vya Wananchi wa Uganda (UPDF) anayetuhumiwa kwa uvunjaji mkubwa wa haki za binadamu.
“Kwa kusisitiza, Peter Elwelu alihusika, akiwa anaoongoza vikosi vya UPDF, katika mauaji ya bila kufuata sheria yaliyofanywa na wanachama wa UPDF.
“Kama matokeo ya vitendo hivi, maafisa wa Uganda walioorodheshwa kwa uteuzi hawaruhusiwi kwa ujumla kuingia Marekani.”
Idara hiyo pia imechukua hatua za kuweka vizuizi vya visa kwa maofisa wengine wa Uganda kwa kudhoofisha mchakato wa kidemokrasia na kuzima wanachama wa makundi yaliyodhulumiwa au walio hatarini nchini Uganda.
Ikesema watu hao wanawajibika au wanashiriki katika kukandamiza wanachama wa upinzani wa kisiasa wa Uganda, wahamasishaji wa jamii za kiraia, na jamii ndogo nchini Uganda.
“Marekani inasimama pamoja na Wauganda wanaopigania misingi ya kidemokrasia, serikali inayotoa kwa wananchi wake wote.”
Marekani imesema kutowajibishwa kwanwaru hao kunaruhusu maafisa fisadi kubaki madarakani, kupunguza kasi ya maendeleo, kurahisisha uhalifu, na kusababisha usambazaji usio sawa wa rasilimali, ambao unaweza kuathiri makundi yasiyowakilishwa na wale waliotelekezwa kwa kiwango kikubwa.
“Hatua za leo zinathibitisha azma ya Marekani ya kusaidia uwazi katika mchakato wa kidemokrasia nchini Uganda, kupambana na ufisadi kimataifa, na kushughulikia utamaduni mpana wa kutotawajibishwa ambao unazuia Wauganda wote kufurahia haki zao za binadamu na uhuru wa msingi.”
Adaiwa kumiliki nyumba Uingereza
Katika hatuà nyingine, Spika Among ameilaumu Uingereza kwa madai ya kughushi taarifa zinazoonyesha kwamba anamiliki nyumba nchini humo.
Taarifa ya Spika Among imekuja muda mfupi baada ya Rais Yoweri Museveñi kumtaka spika huyo ajieleze kwa umiliki huo wa nyumba tofauti na taarifa alizompa awali.
“Nimepata taarifa tofauti na ulivyonieleza kwamba, unamiliki nyumba nchini Uingereza kwa mfumo wa Flat 4, Silk House, 7 Waterden Road, London E20 3AL Uingereza. Unamiliki nyunba hiyo au unapangisha?” amehoji Rais Museveni katika barua ya Mei 23 iliyovuja.
Katika barua hiyo, Rais Museveni amemtaka Waziri wa Mambo ya Nje kuwasiliana na Serikali ya Uingereza kupata uhakika wa taarifa hizo.
Baada ya barua hiyo kutoka hadharani, Spika Anita ameilaumu Serikali ya Uingereza kwa kumhusisha na ufisadi huo.
“Kama Uingereza inasema namiliki mali l, yenyewe ndio ieleze ni mali gani ninazomiliki mimi Anita Annet Among. Kughushi liwe ni neno la mwishò unalotegemea kutoka kwao,” ameandika Among katika ukurasa wake wa X.
Aprili 30, Serikali ya Uingereza kwa mara ya kwanza iliwawekea vikwazo vya kimataifa dhidi ya rushwa Spika Among na mawazir wawili wa zamani wa Karamoja akiwamo
Mary Goretti Kitutu na Agnes Nandutu, kufuatia kashfa ya wizi wa mabati.
Vikwazo hivyo pia vimewekwa kwa viongozi 42 katika nchi za Zimbabwe, Honduras, Bosinia- Herzegovina, Colombia, Russia, Kosovo, Israel, Equatorial Guinea na Lebanon.
Hata hivyo, Spika Among amepuuza vikwazo hivyo, akisema ni matokeo ya Uganda kupitisha sheria inayopinga vitendo vya ushoga.