Uamuzi mgumu ulivyobadili upepo Yanga

YANGA ndio mabingwa tena. Imebeba taji hilo kwa mara ya tatu mfululizo, ikiendeleza ubabe wake kwenye safari iliyokuwa na mabonde na milima.

Yanga imelichukua taji hilo ikiwa na sura fulani tofauti na misimu miwili iliyopita, ikitoka kupitia mabadiliko mbalimbali kwa maana ya namna ya ilivyoanza msimu huu wa 2023/24 na hata muundo wa timu yao. Kumbuka huu ni ubingwa wa 30 wakiwa ndiyo mabingwa wa kihistoria wa ligi hiyo.

YATEMA 10, BENCHI LA NABI LASEPA

Ilipomaliza msimu uliopita, Yanga ikakutana na taarifa ya kushtua, kwanza ikawa kwa kuondokewa na benchi lake la ufundi chini ya Kocha Nasreddine Nabi na wasaidizi wake wanne kuanzia kocha msaidizi Cedric Kaze, kocha wa mazoezi ya viungo, Helmy Gueldich, kocha wa makipa, Milton Nienov na mtaalam wa kuchambua mechi za video, Khalili Ben Yousef aliyeungana na kocha huyo kwenda klabu ya FAR Rabat.

Mbali na benchi hilo, Yanga pia ikapoteza wachezaji 10 kwa nyakati tofauti, wakiwemo Feisal Salum ‘Fei Toto’, beki kiraka, Yannick Bangala waliouzwa Azam FC, mfungaji wao bora msimu huo, Fiston Mayele aliyeuzwa Pyramids ya Misri.

Wengine walioachwa ni kiungo Gael Bigirimana, mabeki Djuma Shaban aliyevunjiwa mkataba, Abdallah Shaibu ‘Ninja’, David Bryson, Mamadou Doumbia, mawinga Dickson Ambundo, Bernard Morrison na kipa Erick Johola.

YAINGIZA SABA, BENCHI JIPYA

Baada ya kimbunga hicho cha walioondoka, wakati mashabiki wa timu hiyo wakiwa na wasiwasi juu ya msimu huu hali itakuwaje, uongozi wa Yanga chini rais wao injinia Hersi Said akisaidiana na mfadhili wao Ghalib Said Mohammed ‘GSM’, ukashusha benchi jipya la ufundi kuanzia kocha mkuu, Miguel Gamondi raia wa Argentina, aliyekuja na wasaidizi wake, kocha msaidizi, Mussa N’dew raia wa Senegal, kocha wa viungo, Taibi Lagrouni, kocha wa makipa Alaa Meskini wote kutoka Morocco na mchambuzi wa video, Msauzi Mpho Maruping.

Baada ya kuunda benchi hilo la ufundi, Yanga ikaingiza wachezaji wapya saba kwenye kikosi chao, ambao ni mabeki Nickson Kibabage, Yao Akouassi, Gift Fred, viungo wakiwa Pacome Zouzoua, Jonas Mkude, Maxi Nzengeli, Mahalatse Makudubela na mshambuliaji mmoja tu, Hafiz Konkon.

Yanga iliuanza msimu kwa mshtuko ikipoteza taji la kwanza mapema tu kwenye mechi za Ngao ya Jamii. Michuano hiyo iliyoshirikisha timu nne, ilichezwa kuanzia hatua ya nusu fainali na Yanga ilikutana na Azam FC na kushinda mabao 2-0.

Mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Bara kwa msimu wa tatu mfululizo, ilikuwa ikilishikilia taji hilo kwa misimu miwili mululizo na kwenye fainali dhidi ya Simba ilipoteza kwa mikwaju 3-1, baada ya dakika 90 kumalizika kwa suluhu.

Hata hivyo, kupoteza Ngao ya Jamii ni kama iliwaamsha na kwenye ligi ilianza kwa gia kubwa kwa kugawa vichapo katika mechi 15 za mzunguko wa kwanza na kukaa kileleni mwa msimamo ikiwa na pointi 40. Ilishinda mechi 13, sare moja na kupoteza moja, huku ikifunga mabao 36 na kuruhusu manane pekee.

Kiwango hicho cha Yanga kilichagizwa na mabadiliko makubwa ya timu hiyo kutokana na falsafa mpya za kocha Gamondi na alikifanya kikosi kuwa na ubora mkubwa na pumzi ya kutosha. Timu ilikaba kwa nguvu na utamu zaidi ikawa inafunga mabao mengi tofauti na msimu uliopita chini ya Nabi.

Usajili wa dirisha dogo, Yanga iliachana na wachezaji watatu, winga Lucapel Moloko, washambuliaji Konkon, Crispin Ngushi aliyetolewa kwa mkopo kwenda Coastal Union na kuingiza watatu wakiwemo mshambuliaji Joseph Guede na viungo Shekhan Hamis na winga Augustine Okrah.

Msimu huu, Yanga ilikuwa na deni kubwa ambalo lilitokana na kurejea kwao Ligi ya Mabingwa, ikitoka kufanya vizuri kwenye Kombe la Shirikisho baada ya kucheza fainali dhidi ya USM Alger ya Algeria iliyobeba uningwa kwa faida ya bao la ugenini.

Macho ya wengi walitaka kuona Yanga itafika wapi kwenye ligi ya mabingwa hasa baada ya kufikisha miaka mingi ikishindwa hata kutinga makundi wala robo fainali.

Yanga ikafanya kweli kwa kuvuka hatua ya mtoano kibabe na baadaye hata makundi na kuishia hatua ya robo fainali ikibaki kidogo tu kuwang’oa Mamelodi Sundown ya Afrika Kusini.

Mzuka wa matokeo ya ligi ya mabingwa ni kama yaliibeba Yanga pia kwenye ligi baada ya kuwa na moto mkali wa kushinda mechi zake ikipoteza nne pekee ikitoa sare tatu na kushinda mechi sita za mashindano hayo tangu ilipoanza hatua ya mtoano.

Unaweza kusema ukiondoa ubora wa ukuta wake bora ambao umeruhusu mabao 14, ikiwa timu iliyoruhusu mabao machache zaidi kuna ubora mkubwa ulionyeshwa na viungo wake.

Msimu huu Yanga imebebwa na mabao ya viungo wake Stephanie Aziz KI aliyeibuka Mfungaji Bora wa Ligi akiwa na mabao 21, nyuma yake wamo Nzengeli mwenye mabao 11, Mudathir Yahya (9) kisha Pacome Zouzoua (7), wakati washambuliaji wakibebwa na Joseph Guede mwenye mabao sita.

Yanga ilijihakikishia ubingwa wake msimu huu ikiwa ugenini ilipoichapa Mtibwa Sugar kwa mabao 3-1 ikiwa imebakiza mechi tatu kabla ya ligi kumalizika ilipofikisha pointi 71 ambazo hakuna timu ambayo ingeweza kuzifikia.

Msimu huu hakuna timu ambayo haikufungwa na Yanga lakini zipo klabu zitawakumbuka vibaya mabingwa hao baada ya kuwa ndio klabu zilizokutana na vipigo vikali kutoka kwa kikosi cha Gamondi kila moja ikilamba mabao matano ambazo ni KMC, JKT Tanzania, Simba na Ihefu, hakuna timu iliyoweza kushinda kwa idadi hiyo ya mabao kwenye mechi nyingi kuliko wao.

Yanga imeweka rekodi ya kuwa timu iliyofunga mabao mengi (71) ambayo hakuna timu iliyofanya hivyo kwa msimu mmoja tangu mfumo wa timu 16 uanze kutumika, pia imeweka rekodi ya kukusanya pointi 80 ambazo ni nyingi zaidi.

Ubora ambao Yanga iliuonyesha msimu huu ni wazi kikosi hicho kilistahili mafanikio haya ya kuwa mabingwa kutokana na ubora wa kikosi chao na hata matokeo yao ya uwanjani, yote haya yakitokana na ubora wa wachezaji wao na benchi lao la ufundi.

Nini maoni yako; 0658-376 417

Related Posts