Dar es Salaam. Zikiwa zimepita wiki tatu tangu Lilenga Lilenga, mkazi wa Mwandiga mkoani Kigoma kudaiwa kuchukuliwa na watu wanaodaiwa ni polisi, Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Filemon Makungu amesema wameshaanza uchunguzi.
Akizungumza na Mwananchi jana Jumatano Mei 29, 2024, mke wa Lilenga, Johari Kabwe amesema wanawashuku polisi kwa kuhusika na kupotea kwa mume wake kutoka na mfululizo wa matukio kabla ya kupotea kwake.
Hata hivyo, RPC Makungu amekanusha taarifa hizo.
“Taarifa zilizopo ni kupotea kwa mtu sio kukamatwa. Yanayosemwa na ndugu zake mimi siyajui, ila taarifa iliyopo na ndio ndugu zao waliotoa taarifa polisi kwamba kuna mtu aliyepotea. Alikwenda ziwani kuangalia mali zake, wamemtafuta hapatikani,” amesema.
Kamanda Makungu amesema wameshaanza uchunguzi wa suala hilo.
“Taarifa niliyonayo mimi ni ya kupotea kwa mtu kwa kadiri ya maelezo waliyotoa polisi, hayo mengine siyajui. Tumeshaanza juhudi za kumtafuta, tunafanya uchunguzi.
“Ndugu zake walikuja wanaulizia na walishaandika maelezo yao, yapo. Mama yake alinipigia simu, aliniuliza mmefikia wapi kwenye upelelezi, basi,” amesema Kamanda Makungu.
Akizungumza na Mwananchi, Johari amesema ilikuwa Jumamosi Mei 11, 2024 mumewe alikuwa kwenye shughuli za uvuvi Ziwa Tanganyika, ndipo walipowasiliana kwa simu kwa mara ya mwisho.
“Mume wangu alitoka akisema anakwenda kwenye shughuli zake, ilipofika saa 6:43 akasema anajiandaa kurudi nyumbani. Ilipofika saa 7 mchana simu yake ikawa hapatikani, nikahisi labda kuna dharura. Lakini ilifika mpaka usiku akawa hapatikani, nikawauliza wazazi wake kama wamemwona, wakasema hapana,” amesema.
Amesema hadi wanakwenda kulala hakukuwa na mafanikio ya kumpata.
“Jumapili tukaenda kutoa taarifa Kituo Kikuu cha Polisi cha Kigoma, Mkuu wa kituo akasema hayupo, tukaenda kwa RPC naye akasema hana taarifa, Jumatatu tukaenda kwa mkuu wa mkoa akatuambia turudi kwa RPC, tukarudi, ndipo nikaambiwa nitoe maelezo ilivyokuwa, nikaeleza.
Amesema katika maelezo yake aliwaeleza polisi kuwa anahisi mumewe atakuwa amekamatwa kwa sababu kuna vijana nao walikamatwa na hawajaonekana tena.
Hata hivyo, RPC Mangungu amekanusha taarifa za Lilenga kukamatwa akisema hana pia taarifa kwamba aliwahi kukamatwa.
Kwa upande mwingine, Maneno Rashid aliyekuwa akjifanya kazi na Lilenga amesema siku hiyo, Lilenga alikuja kilipokuwepo chombo chake eneo la Kalalangapo muda wa saa 2 asubuhi.
“Alipofika akakuta chombo kimeshafika, akaomba mboga (samaki) tukampatia na aliagiza mtu wa pikipiki ampelekee nyumbani kwake.
“Tumekaa pale mpaka saa 4 asubuhi, akaniaga kwamba anakwenda Kibirizi ili akaagize mafuta kwa ajili ya chombo chake kingine kilichopo Mwamgongo.
“Nikampa dumu mbili na nikamsindikiza, akapanda pikipiki akaenda Kibirizi na huo ndio ulikuwa muda wa mwisho kumwona.
“Baadaye saa 5 alinitumia ujumbe wa simu akaniambia kuna vitu nivipokee, tangu hapo sijawasiliana naye tena na simu zake hazipatikani,” amesema.