Dar es Salaam. Serikali imewataka wadau wa sekta ya ununuzi wa umma kuhakikisha wanazingatia misingi ya uadilifu, uaminifu na haki katika michakato ya ununuzi wa umma ili kuiwezesha Serikali kupata thamani ya fedha.
Hayo yamesemwa leo Alhamisi Mei 30, 2024 na Mkurugenzi wa Sera na Mipango kutoka Wizara ya Fedha, Moses Dulle wakati akifunga mafunzo ya siku mbili juu ya moduli ya uwasilishaji wa malalamiko au rufaa kwa njia ya kielektroniki yaliyofanyika jijini hapa.
Akiwa amemuwakilisha Naibu Katibu Mkuu Waziri wa Fedha, Dk Natu El-maary katika hafla hiyo, Dulle amesema asilimia 70 ya matumizi ya Serikali huelekezwa katika ununuzi wa umma.
“Kwa kutumia mfumo mpya, uwazi na uwajibikaji utaisaidia Serikali kupata thamani halisi ya fedha katika miradi yake, hivyo ni vema wadau wa sekta ya ununuzi wa umma kuhakikisha wanazingatia misingi ya uadilifu, uaminifu na haki katika michakato ya ununuzi wa umma,” amesema Dulle.
Dulle amesema umuhimu wa mafunzo kuhusu moduli ya uwasilishaji wa rufaa kwa njia ya kielektroniki umechagizwa na mabadiliko ya sayansi na teknolojia yanayoendelea duniani, hususani kutungwa upya kwa Sheria ya Ununuzi wa Umma ya mwaka 2023 na kuruhusu hatua za mageuzi kuchukuliwa.
“Kutungwa upya kwa sheria hii kumesaidia kuongeza ufanisi, haki, uwazi na uwajibikaji katika ununuzi wa umma,” amesema Dulle.
Dulle ametumia nafasi hiyo kuitaka Mamlaka ya Rufani ya Zabuni za Umma (PPAA) kuiwezesha kufikia malengo ya kutoa uelewa wa moduli ya uwasilishaji wa rufaa kwa njia ya kielektroniki kwa wadau wa ununuzi na kujenga uelewa wa pamoja.
Katibu Mtendaji wa PPAA, James Sando amesema Mamlaka ya Rufani itaendelea kushirikiana na Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) kusimamia kutoa mafunzo ya mfumo mpya wa kuwasilisha na kushughulikia rufaa kwa njia ya kielektroniki ili kuwawezesha wengine kujua jinsi ya kutumia moduli ya malalamiko.
“Pia, PPAA itaendelea kuzielimisha taasisi za ununuzi na za wazabuni wa kanda nyingine, kuhusu mfumo huu mpya hususani moduli ya kuwasilisha na kushughulikia rufaa kielektroniki,” amesema Sando.
Mafunzo hayo yaliandaliwa na PPAA kwa kushirikiana na PPRA kwa ajili ya wataalamu kutoka mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Morogoro na Pwani.