Songwe. Baada ya shida ya miaka mingi, wakazi wa Kijiji cha Iseche wilayani Songwe wameanza kupumua baada ya mradi wa majisafi na salama uliokuwa ukijengwa katika eneo hilo kukamilika.
Baadhi ya wanawake kijijini hapo wanasema kero ya maji ilikuwa ikiteteresha ndoa zao, kukamilika kwa mradi huo.
Wamesema walikuwa wakitumia muda mwingi na kusaka maji kiasi cha kufanya wasiaminiwe na waume zao.
Shukuru Mwashilindi, mkazi wa Iseche amesema leo Alhamisi Mei 30, 2024 kuwa awali ndoa nyingi zilikuwa shakani.
“Tulikuwa tunatembea kilomita tatu kufuata maji, tukichelewa waume zetu walikuwa hawatuelewi, wengine wanadhani wake zao wameenda kwa wanaume wengine.”
Ameishukuru Serikali kwa kuukamilisha mradi huo akisema hawakutarajia kama kuna siku watachota maji ya bomba kijijini hapo.
“Tunaishukuru sana Serikali imekuwa kama ndoto kupata maji, kabla ya mradi tulikuwa tunatumia maji ya kwenye madimbwi ambayo ni hatari,” amesema Mwashilindi.
Mkazi mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Matatizo Mwasilanga amesema kukamilika kwa mradi huo kutasaidia waache kutumia ya madimbwi na mifugo.
Amesema Serikali imesikia kilio chao na mradi huo utapunguza kero kwa wanawake kutembea umbali mrefu kusaka maji yasiyofaa.
Meneja wa Wakala wa Majisafi na Usafi wa Mazingira (Ruwasa) wilayani Songwe, Boniface Mfungo amesema mradi huo umejengwa kwa Sh310 milioni.
Amesema fedha hizo zilizotengwa kupitia mradi wa Lipa kwa Matokeo katika bajeti ya mwaka wa fedha 2022/23 umelenga kuondoa changamoto mbalimbali kwa wananchi.
Mkuu wa Wilaya ya Songwe, Solomoni Itunda amesema mpaka sasa Ruwasa wanaendelea kupokea maombi kwa wananchi wanaohitaji kuunganishiwa huduma ya maji nyumbani.
Ametoa rai kwa wananchi wenye uhitaji wa kuunganishiwa huduma hiyo kujitokeza kuomba.
“Niwaombe sana wana Iseche mtunze hii miundombinu ya maji, Serikali imesikia kilio chenu mmepata maji, sambamba na hilo tunzeni mazingira ili vyanzo vya maji visikauke,” amesema Itunda.