Waziri Mkuu kufanya ziara ya siku tatu Geita

Chato.  Waziri Mkuu Kassim Majaliwa anatarajiwa kufanya ziara ya siku tatu mkoani Geita kuanzia Mei 31, hadi Juni 02, 2024.

Lengo la ziara hiyo ya kikazi ni kushiriki Wiki ya Mazingira inayotarajiwa kuanza Juni mosi mwaka huu.

Akitoa taarifa kwa waandishi wa habari leo Alhamisi Mei 30, 2024 wilayani Chato, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigella amesema Majaliwa anatarajiwa kutua kwenye uwanja wa ndege Chato Mei 31,2024 saa tisa alasiri kisha kuzungumza na watumishi wa Halmashauri ya Chato na wakuu wa taasisi.

Katika Wiki ya Mazingira Duniani, Waziri Mkuu atakuwa mgeni rasmi Juni mosi ambayo kwa Kanda ya  Ziwa itaadhimishwa wilayani Chato kwenye Hospitali ya Kanda atakapopanda mti na kufanya usafi katika maeneo mbalimbali.

“Kwenye kanda yetu ya Ziwa Victoria Waziri Mkuu Majaliwa ameteuliwa kuwa mgeni rasmi na maadhimisho yetu yatafanyika katika Hospitali ya Kanda Chato kuanzia saa 12 asubuhi, hivyo kila mwananchi ajitokeze kushiriki usafi wa mazingira na upandaji wa miti ikiwa ni sehemu maadhimisho ya mazingira duniani yatakayohitimishwa Juni 5, 2024.”

Shigella amesema Majaliwa akiwa Chato atatembelea pia soko la samaki na kuweka jiwe la msingi, baadaye atahutubia mkutano wa hadhara katika kituo cha zamani cha mabasi Chato.

Juni 2, 2024 ataendelea na ziara yake wilayani Nyang’hwale ataweka jiwe la msingi katika jengo la halmashauri  na baadaye atazindua la uwezeshaji wananchi kiuchumi lililopo Kata ya Kharumwa.

Kisha atahutubia mkutano wa hadhara katika Uwanja wa Sabasaba uliopo wilayani humo.

Pia, amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi kumpokea Waziri Mkuu na kushiriki mikutano ya hadhara iliyoandaliwa kwa ajili ya kumsikiliza.

Wakizungumzia ujio wa Waziri Mkuu baadhi ya wananchi wa Chato wamesema ni wa kitaifa na ni sehemu ya kuendelea kuwakumbusha watumishi wa halmashauri kuendelea kuwajibika na kutekeleza majukumu yao kwa ufasaha.

Shida Yohana amesema  mradi wa soko la samaki unaotarajiwa kuwekwa jiwe la msingi ni mradi unaotegemewa kuinua uchumi wa wananchi.

Related Posts