WIZARA YA MALIASILI NA UTALII YAPONGEZWA KWA ONESHO MAALUM LA KUTANGAZA VIVUTIO VYA UTALII.

Na Jane Edward, Dodoma

Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wameipongeza Wizara ya Maliasili na Utalii kwa ubunifu wa kuandaa Maonesho maalumu ya kutangaza vivutio vya utalii yenye lengo la kuelimisha wabunge kuhusu masuala ya uhifadhi wa maliasili na uendelezaji utalii yanayofanyika katika viwanja vya Bunge kuanzia leo Mei 30,2024.

Akizungumza katika maonesho hayo, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, Mhe. Timotheo Mnzava ambaye pia ni Mbunge wa Korogwe Vijijini ameipongeza Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kuandaa maonesho hayo.

“Huu ni ubunifu mkubwa, tunaipongeza Wizara ya Maliasili na Utalii kwa hatua hii ya maonesho haya yanayotoa fursa kwa waheshimiwa Wabunge, watumishi wa Bunge, watumishi wa Serikali na wageni wengine kuweza kujifunza na kujionea vivutio mbalimbali vya utalii” Mhe. Mnzava amesisitiza.

Amefafanua kuwa uwepo wa maonesho hayo ni moja ya mikakati ya Wizara ya Maliasili na Utalii ya utangazaji utalii kwa Watanzania walioko nchini.

Naye, Mbunge wa Iringa Mjini, Mhe. Jesca Msambatavangu ameipongeza Wizara ya Maliasili na Utalii kwa maandalizi na mpangilio mzuri wa mabanda.

“Nimevutiwa na mpangilio wa mabanda na muonekano wa wanyama mbalimbali na vivutio vyao na wanaotoa taarifa katika idara zao ni wabobezi, hivyo nawapongeza sana na tunamshukuru sana Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki anatuhudumia vizuri sana na tunajisikia vizuri” amesema.

Aidha, amesema kupitia maonesho hayo amepata fursa za kula nyamapori na kuishauri Wizara ya Maliasili na Utalii kuongeza kiwango cha nyama hiyo kwa maonesho ya mwaka ujao.

Kwa upande wake Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki amesema Wizara ya Maliasili na Utalii ina kila sababu ya kufanya maonesho hayo kutokana na ukubwa wake ikiwa ni Wizara yenye sekta nyingi na Taasisi mbalimbali chini yake, ukubwa wa maeneo yake yaliyohifadhiwa unayoyasimamia na pia uwepo wa mazao mbalimbali ya utalii hivyo ni vyema wabunge wakapata uelewa wa masuala hayo.

“Tuna mazao mbalimbali ya utalii ikiwa ni pamoja na utalii wa fukwe, utamaduni, michezo, utalii wa wanyamapori katika hifadhi zetu na utalii wa chakula hivyo, tulitamani waheshimiwa Wabunge waweze kuona thamani ya aina hizi za utalii kuonyesha kwamba kwa nini wageni waje Tanzania na si kwenda nchi zingine” Mhe. Kairuki amesisitiza.

Pia, Waziri Kairuki amewashukuru Watanzania wote waliotembelea maonesho hayo na kuwakaribisha kufuatilia wasilisho la Bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii itakayowasilishwa Mei 31,2024 ili kuweza kujionea maboresho mbalimbali yaliyopatikana katika sekta hiyo.

Maonesho hayo yaliyonogeshwa na Wanyamapori aina ya Tembo, Chui, Simba na Kobe pamoja na utalii wa chakula cha nyamapori yamehudhuriwa na mamia ya watu kutoka katika viunga vya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Related Posts