Johannesburg. Wakati kura zinaendelea kuhesabiwa katika uchaguzi mkuu wa Afrika Kusini yakiendelea kutolewa, matokeo ya awali yanaonyesha kuwa chama tawala cha ANC huenda kikapoteza nguvu zake.
Endapo hilo litatokea, ANC italazimika kufanya makubaliano na vyama vingine ili kuunda serikali ya pamoja. Uchaguzi wa washirika wa muungano utategemea umbali wao kutoka alama ya asilimia 50.
Iwapo ANC itafanya vibaya zaidi kuliko inavyotarajiwa, kuna uwezekano wa kuondolewa kabisa serikalini.
Kwa mujibu wa Aljazeera, katika matokeo hayo ya awali, ANC inaongoza kwa kupata asilimia 42.3 ya kura, ikifuatiwa na Democratic Alliance (DA) yenye asilimia 23.4, chama kinachofuatia ni uMkhonto we Sizwe (MK) chenye asilimia 10.8 na Economic Freedom Fighters (EFF) kimepata karibu asilimia 10 ya kura.
Anguko hili lililotarajiwa linatokea kwa mara ya kwanza tangu chama hicho kilipoanza kutawala Afrika Kusini baada ya Serikali ya makaburu, miaka 30 iliyopita.
Wapigakura wengi wanailaumu ANC kwa viwango vya juu vya ufisadi, uhalifu na ukosefu wa ajira nchini. Baraza la utafiti linaloheshimika, Council for Scientific and Industrial Research (CSIR) na tovuti ya News24 wamekadiria kuwa kura za mwisho za chama hicho zitakuwa karibu na asilimia 42 kutoka asilimia 57 kilizopata mwaka 2019.
Akizungumza na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), mwenyekiti wa shirika lisilo la kiserikali la Democracy Works Foundation, Profesa William Gumede, amesema iwapo chama hicho kitapata matokeo mabaya, Rais Cyril Ramaphosa anaweza kushinikizwa na ANC kujiuzulu.
“ANC inaweza kumfanya kuwa kisingizio, na kundi ndani ya chama linaweza kushinikiza nafasi yake ichukuliwe na naibu wake, Paul Mashatile. EFF na MK pia huenda wakataka ajiuzulu kabla ya kukubaliana na muungano wowote na ANC,” amesema.
Waafrika Kusini hawampigii kura Rais moja kwa moja. Badala yake wanapigia kura wabunge, chama kinachoshinda ndiyo kinamchagua rais.
Katika matokeo hayo, Jacob Zuma anayeongoza MC, amezua mshangao kwa kushika nafasi ya tatu, ikiwa ni miezi kadhaa tangu alipoachana na ANC Desemba 2023.
KwaZulu-Natal ni nyumbani kwa Zuma, na jimbo lenye idadi ya pili kwa wingi wa kura, jambo ambalo linaifanya eneo muhimu katika kuamua, iwapo ANC itadumisha wingi wake bungeni.
Ingawa Zuma amezuiwa kugombea ubunge kwa sababu ya kutiwa hatiani kwa dharau ya mahakama, jina lake bado lilionekana kwenye karatasi za kupigia kura kama kiongozi wa uMkhonto we Sizwe.
Iwapo MK itashinda KwaZulu-Natal, itakuwa pigo kubwa kwa ANC amesema Profesa Gumede.
ANC pia inakabiliwa na hatari ya kupoteza wingi wake katika eneo la kiuchumi la Gauteng, ambako chama hicho kwa sasa kina asilimia 36 dhidi ya asilimia 29 ya DA.