Buku 5 tu kuwaona Aziz KI, Fei Toto

MASHABIKI wa soka visiwani Zanzibar wana kiu ya kuona udambwidambwi wa Stephane Aziz KI, Pacome Zouzoua na Yao Kouassi wa Yanga pamoja na mziki mnene wa vijana wa Azam FC wanaoongozwa na Feisal Salum, Kipre Junior, Abdul Suleiman na Gjibiril Sillah.

Katika kuhakikisha wanapata burudani ya fainali ya Kombe la Shirikisho (FA) kati ya Yanga na Azam, Shirikisho la Soka nchini (TFF) imerahisisha kazi kwa kuweka kiingilio cha chini cha pambano hilo kuwa Sh 5,000 (buku tano tu) eneo la mzunguko maarufu kwenye Uwanja wa New Amaan kama Saa.

Kwa mujibu wa tangazo la viingilio vya pambano hilo litakalopigwa Jumapili kwenye Uwanja wa Amaan kuanzia saa 2:15 usiku ni kwamba Jukwaa Kuu la VIP, watu watatoboka kwa kutoa Sh 30,000, huku eneo la Wings ni Sh20,000 wakati Jukwaa la Urusi ni Sh15,000 na lile la Orbit kila shabiki atalipa Sh 10,000.

Hilo ni pambano la kwanza la Kombe la Shirikisho Bara kupigwa visiwani Zanzibar na ni la tisa tangu kurejeshwa kwa michuano hiyo mwaka 2015 baada ya kusimama wakati ikifahamika kama Kombe la FA.

Azam na Yanga zinakutana kwa mara ya tatu katika fainali za michuano hiyo iliyoasisiwa mwaka 1967.

Katika fainali mbili ilizokutana msimu wa 2015-2016 na 2022-2023, Azam ilishindwa kufurukuta mbele ya Yanga kwa kufungwa mabao 3-1 na 1-0 mtawalia na sasa zinakutana kila moja ikitoka kushinda mechi ya nyumbani ya Ligi Kuu Bara msimu uliofungwa mapema wiki hii.

Yanga ilishinda nyumbani kwa mabao 3-2 kabla ya Azam kulipa kisasi kwa ushindi wa 2-1 na kuisaidia kumaliza nafasi ya pili katika msimamo wa ligi hiyo mbele ya Simba iliyomaliza ya tatu, huku Yanga ikibeba ubingwa kwa msimu wa tatu mfululizo na kufikisha taji kla 30 tangu Ligi ya Bara ilipoasisiwa mwaka 1965.

Tayari Kocha Mkuu wa Azam, Youssouf Dabo ametamba mapema kwamba anajua Yanga ni timu nzuri, lakini hata wao ni wazuri na kiu yake ni kuona klabu hiyo inabeba taji hilo kwa vile mipango ya kutwaa Ligi Kuu ilikwama mbele ya wababe hao wa Tanzania.

“Tunajua hautakuwa mchezo rahisi, lakini vijana wapio tayari kuipa Azam taji la Kombe la Shirikisho, kwani ni muda mrefu timu hii haijachukua ubingwa Tanzania Bara,” alisema Dabo anayewategemea zaidi Fei Toto, Sopu, Yannick Bangala, Idd Seleman ‘Nado’, Kipre Jr na Sillah kuinyamazisha tena Yanga.

Related Posts