Dakika 47 za Mdee akikomalia bajeti Wizara ya Ujenzi

Dodoma. Dakika 47 zimekuwa moto bungeni baada ya hoja ya kutaka ufafanuzi kuhusu utekelezaji wa miradi kwa mfumo wa EPC +F iliyotolewa na Mbunge wa Viti Maalumu, Halima Mdee kusababisha vuta- nikuvute ya wabunge.

Mfumo wa EPC +F ni utaratibu wa utekelezaji wa miradi unaoruhusu kampuni au mkandarasi kuwa jukumu la kusimamia hatua zote kuu nne za mradi – uhandisi, ununuzi, ujenzi na ufadhili.

Wabunge alijadili hoja hiyo usiku jana Mei 30, 2024 wakati Bunge lilipokaa kama Kamati ya Bunge zima kupitisha kifungu kwa kifungu bajeti ya Wizara ya Ujenzi kwa mwaka wa fedha 2024/2025.

Hatua hiyo imewalazimu mawaziri watatu kusimama kwa nyakati tofauti kujibu hoja hiyo, ambayo pia ilichangiwa na Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson.

Mawaziri waliochangia kujibu ni Innocent Bashungwa, Waziri wa Ujenzi, Dk Mwigulu Nchemba (Fedha) na Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa.

Katika hoja yake, Mdee amesema masharti ya zabuni katika miradi ya EPC+F yaliyochapishwa kwenye Mfumo wa Manunuzi wa TANePS, wazabuni walitakiwa kuwasilisha angalau mapendekezo ya wafadhili wawili wa zabuni husika.

Amesema hiyo ina maana hadi mtu anashinda zabuni anakuwa na uhakika wa chanzo cha fedha na ndiyo maana Serikali ilikwenda kusaini mikataba na waliokidhi vigezo kati ya waombaji 129.

“Sasa tunataka utuambie ukweli kwenye hili tulikwama wapi? Kwa sababu kitu kinachonitatiza katika ukurasa wa 36 wa hotuba yako (Waziri wa Ujenzi), unasema Serikali inaendelea na mazungumzo ili kupata fedha za utekelezaji wa miradi hiyo.”

“Kwani ninyi si mnatafuta fedha kwa miradi mnayoitekeleza, hii EPC +F ilikuwa ni wakandarasi wanaoshindanishwa, (wenye fedha) unawapa kazi?” alihoji Mdee.

Amesema kinachozungumzwa katika hotuba ya Waziri wa Ujenzi, Bashungwa; kilichozungumzwa na aliyekuwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa mwaka 2023 na alichozungumza Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu ni vitu tofauti.

Akifafanua, Dk Mwigulu amesema wakati Serikali inaingia mkataba wa utekelezaji wa miradi hiyo, riba katika soko la dunia ilikuwa asilimia nne hadi tano, lakini hivi sasa riba za mikopo ziko kati ya asilimia 10 hadi 12.

“Halima, wewe ungekuwa Serikali ungemwambia endelea tu kwa sababu mzigo utabebwa na Watanzania. Hatuwezi kufanya hivyo. Sasa soko limechafuka, tunaona hii hali si ya kudumu itarejea katika hali ya kawaida. Kwa maana hiyo wana wajibu ule, walitakiwa kuleta fedha lakini riba zimeshabadilika,” amesema Dk Mwigulu.

Amesema Serikali imeona wazabuni hao wataendelea kutafuta fedha kwa masharti waliyowaambia na si kwamba Serikali inakwenda kutafuta fedha hizo.

Hatua hiyo, ilimfanya Spika wa Bunge, Dk Tulia kuhoji iwapo fedha za EPC+F zitatafutwa na Serikali, watapewa wakandarasi haohao au watafuata utaratibu wa kisheria wa kuwapata wajenzi.

Spika alihoji pia iwapo fedha kama zinatafutwa na Serikali, zinakwendaje moja kwa moja bila kupita serikalini.

Akijibu hilo, Dk Mwigulu amesema wao wanafanya wajibu wao kwa yule aliyepangwa kutoa fedha za utekelezaji wa miradi hiyo.

Mdee amesema Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) inaeleza sababu ya kuchelewa kuanza kwa mradi ni kushindwa kuwasilisha dhamana ya benki ya Sh375.5 bilioni.

Amesema mfumo huo umefeli kwa sababu makandarasi walipoambiwa wawasilishe nyaraka walishindwa.

Dk Tulia alipompa nafasi Waziri Bashungwa, amesema neno fadhili katika kitabu chake halimaanishi kutafuta ufadhili na kwamba nia ya Serikali ni nzuri ya kutaka kukopa kwa muda sahihi na riba sahihi.

“Tusije kujenga barabara kwa sababu ya presha ya kujenga Barabara, halafu badala ya kujenga kilomita tano unajikuta unajenga chache, Watanzania wanahoji mnaacha,” amesema.

Waziri Bashungwa amesema Serikali inaendelea kuwafuatilia wale wa EPC+F kuhakikisha wanapata fedha kwa riba inayokubalika.

Hoja hiyo iliwanyanyua wabunge kadhaa kutaka kuichangia, wakiwamo Edward Ole Lekaita (Kiteto), Mohamed Said Issa (Konde), Luhaga Mpina (Kisesa), Kunti Majala (Viti Maalumu), na Profesa Mbarawa, waziri wa Uchukuzi.

Mohamed Issa katika mchango wake amesema iwapo Serikali inakwenda kutafuta fedha badala ya mkandarasi chini ya EPC+F, haioni kwamba hapo kuna suala la rushwa ambalo linafaa kuchunguzwa?

Kwa upande wake, Kunti amesema Serikali inawachanganya kwa kuwa mwaka jana ilisema haiwezekani barabara hizo kujenga kwa fedha za ndani, na kwamba wakandarasi watakwenda kuwatafuta watu wa kugharimia, lakini hivi sasa wanakuwa kigeugeu.

Mpina amesema Serikali ilikuwa na majibu matatu kuhusu utekelezaji wa utaratibu wa EPC+F; mara ya kwanza ilisema inaanza upya, mara inawapasa kutoa asilimia 10 kwanza kabla ya kuanza ujenzi na pia inasema imeshafanya.

Kutokana na majibu hayo, Mpina aliitaka ikiri ilidanga Bunge.

Mpina alitaka mikataba waliyoingia ivunjwe na watafutwe wakandarasi wengine kwa sababu wameshindwa kukidhi takwa la mikataba.

Kwa upande wake Profesa Mbarawa amesema chini ya utaratibu huo ni wajibu wa mkandarasi kutafuta fedha, lakini Serikali haiwezi kuruhusu riba isiyo na masilahi kwa Taifa.

Amesema si mara ya kwanza kwa Serikali kutumia utaratibu huo katika utekelezaji wa miradi na kueleza kuwa ulishatumika pia kwenye ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR).

Kuifuatia maelezo hayo, Mpina ameomba kumpa taarifa Profesa Mbarawa kuwa, amesema ‘Serikali haijawahi kutumia EPC+F kwa sababu mfumo huo ulikataliwa na akaitaka ipeleke ushahidi wa kutumika kwa utaratibu huo kwenye mradi wa SGR.

“Mbarawa katudanganya, anatutapeli sisi, sijui alikuwa na masilahi gani kwenye mkataba huo,” amesema Mpina.

Hata hivyo, Profesa Mbarawa amesema si yeye alileta utaratibu huo na kwamba, umekuwa ukitumika duniani kote.

Aliposimama Joseph Musukuma, amewataka wabunge kutomsulubu Waziri Bashungwa, badala yake wamsubiri Dk Mwigulu katika bajeti kuu kwa kumpa nafasi pana ya kuelezea utaratibu huo.

Alipohitimisha hoja, Halima amesema CAG ameeleza hadi Machi 2024 wakandarasi wanne waliopewa kazi ya kujenga barabara kwa utaratibu huo wameshindwa kuleta ‘Performance bond’ ya asilimia 10.

Amesema alitarajia kuwa Waziri Bashungwa angesema kwa sababu wakandarasi hao wameshindwa kutekeleza mikataba, wanaivunja na kuanza upya, ndiyo Serikali itazingatia masilahi ya nchi na kutokukurupuka.

Hata hivyo, Bunge lilipitisha bajeti ya Wizara ya Ujenzi ya Sh1.77 trilioni kwa ajili ya matumizi ya mwaka 2024/25.

Serikali kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) Juni 16, 2023 ilisaini mikataba mikubwa ya kujenga kwa kiwango cha lami barabara saba zenye urefu wa kilomita 2,035 kwa kutumia utaratibu wa EPC + F.

Mikataba hiyo saba ya ujenzi iliyosainiwa itagharimu Sh3.775 trilioni na miradi yote ilitarajiwa itekelezwe na kukamilika ndani ya miaka mitano.

Barabara ambazo zingejengwa kwa utaratibu wa EPC + F ziliainishwa kuwa ni Kidatu – Ifakara – Lupiro – Malinyi – Kilosa Kwa Mpepo – Londo – Lumecha/Songea (kilomita  435.8); barabara ya Arusha – Kibaya – Kongwa (kilomita 453.42); barabara ya Handeni – Kiberashi – Kijungu – Kibaya – Njoro – Olboroti – Mrijo Chini – Dalai – Bicha – Chambolo – Chemba – Kwa Mtoro – Singida (kilomita 384.33) na barabara ya Igawa – Songwe – Tunduma -njia nne (kilomita 237.9).

Nyingine ni barabara ya Masasi – Nachingwea – Liwale (kilomita 175); barabara ya Karatu – Mbulu – Haydom – Sibiti River – Lalago – Maswa (kilomita 339) na barabara ya Mafinga – Mtwango – Mgololo (kilomita 81).

Kwa mujibu wa taarifa iliyochapishwa kwenye tovuti ya Tanroads, ujenzi huo ulilenga kuboresha mtandao wa barabara nchini na kuongeza ufanisi katika sekta ya usafiri na usafirishaji ili kuchochea uzalishaji, kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi wa wananchi kwa sehemu zinazopita barabara hizo na kwa Taifa kwa ujumla.

Kupitia utaratibu wa EPC+F, wakandarasi wangewajibika kufanya usanifu wa kina na kujenga barabara hizo kwa viwango na ubora ulioainishwa kwenye mikataba, vihatarishi vyote vinavyohusu usanifu wa mradi na muda wa ujenzi vingebebwa na mkandarasi, hivyo, utaratibu huo kumwezesha mkandarasi kusanifu na kujenga barabara kwa viwango na teknolojia za kisasa.

Wakandarasi wangekuwa na timu nne kwa kila mradi mkubwa ili kuharakisha utekelezaji, hivyo sehemu zote zingeanza kutekelezwa sambamba kwa wakati mmoja na kwa utaratibu huo, kazi zingefanyika kwa umakini na kukamilika mapema.

Related Posts