VIONGOZI wa serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) wamejipambanua kuwa mabingwa wa siasa za masikini jeuri: mara hatutaki fedha za mabeberu, mara tunataka msaada wa mabeberu. Anaandika Mwandishi Wetu… (endelea)
Mmoja wa watu waliokuwa watetezi wa safari za nje za Jakaya Mrisho Kikwete alizokuwa akifanya kila uchao wakati wa awamu yake ni aliyekuwa Waziri wa Ujenzi, John Pombe Magufuli. Magufuli alikuwa akisifu manufaa makubwa ya kiuchumi kutokana na safari hizo katika kuvutia uwekezaji, mitaji mipya na misaada. Msaada mojawapo uliosifiwa wakati ule (2008 na 2013) ni kutoka Shirika la Changamoto za Milenia (MCC) la Marekani.
MCC ilitoa msaada wa dola za Marekani 698 milioni ambazo zilichangia kuboresha miundombinu ya barabara, usambazaji umeme na maji. Tanzania ilipata msaada ule kwa sababu ilitekeleza masharti yaliyomo katika sera za MCC.
Kwa mujibu wa sera ya MCC, nchi wanufaika wa misaada yake zinapaswa kuzingatia demokrasia: kuendesha uchaguzi huru na haki; ushiriki huru wa vyama vya siasa. Pia zinapaswa kuimarisha utawala bora: kuheshimu haki za binadamu, kupambana na ufisadi na kuruhusu uhuru wa kujieleza. Kikwete alizingatia masharti yote.
Mwaka 2015 Magufuli alipoingia ikulu alikumbana na mambo mawili yaliyokiuka sera za MCC. Kwanza, mwaka mmoja kabla, serikali ilipalilia ufisadi katika sakata la fedha za akaunti ya Tegeta Escrow; pili, MCC walikwazwa na matokeo ya uchaguzi wa Zanzibar yaliyodaiwa kumpa ushindi Ali Mohamed Shein. Magufuli akawa katika mtego huo.
Ndipo tarehe 16 Aprili 2016, katika hafla ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa barabara ya kwanza ya juu (Flyover) iliyopo makutano ya Barabara za Mandela na Nyerere, kwenye eneo la Tazara alitangaza kukataa misaada ya nchi wahisani inayoambatana na masharti.
Wakati wana CCM walikuwa wakishangilia alipokuwa akitetea misaada zama za Kikwete, siku ile umati wa aina ile ile ulishangilia hotuba kali iliyompambanua Magufuli kuwa ni maskini jeuri. Katika hotuba ile aliita misaada yenye masharti kwa jina la ‘mkate wa masimango’ na akasisitiza kuliko kula mkate huo ni bora kushindia muhogo.
Kwa ujeuri huo, msaada wa dola za Marekani milioni 472.8 kutoka MCC uliokuwa utumike kuongeza kasi ya usambazaji umeme, ulifutwa. Badala yake serikali ilikopa fedha kwenye mabenki ya mabeberu kwa riba kubwa.
Magufuli alitaka kuwa Mkristo asiyezingatia nguzo ya imani ya kukiri Utatu Mtakatifu au alitaka kuwa Mwislamu asiyetaka kukiri shahada kwamba Mungu ni mmoja na Muhammad (S.A.W) ni Mtume wake. Maana, mtu yeyote anayetaka kubatizwa au kusilimishwa lazima afuate nguzo za dini husika.
Kwa msimamo huo, shirika hilo la Marekani, lilisitisha msaada wake pamoja na kusitisha uhusiano wake na Serikali ya Tanzania. Wakaondoka nchini.
Kilichofuata, Magufuli akafuta safari zote za nje (hata za matibabu), akavuruga uhusiano na majirani, akachoma vifaranga, akaiondoa Tanzania katika Mahakama ya Haki za Binadamu ya Afrika, wapinzani wakajuta kumjua Magufuli. Tanzania ikawa kama kisiwa cha mateso.
Wazito waliokuwemo kwenye Serikali ya Magufuli (sina hakika kama waliridhia uamuzi wa bosi wao au la) ni Rais Samia Suluhu Hassan ambaye alikuwa makamu wa rais na Makamu wa Rais Dk. Phillip Isidori Mpango ambaye alikuwa waziri wa fedha na mipango.
Baada ya Magufuli kufariki dunia tarehe 17 Machi 2021, Samia aliapishwa kuwa rais naye akamteua Mpango kuwa makamu wa rais. Viongozi hao wakuu wamerejesha pumzi mpya: safari za nje zimerudi, wamefufua uhusiano na biashara na nchi jirani, wamefuta kesi zote za kubambika hasa za kisiasa, na wametoa wito kesi za jinai zifunguliwe baada ya upelelezi kukamilika tofauti na ilivyokuwa enzi za Magufuli.
Kuonesha hakuridhishwa na maamuzi ya Magufuli, haraka Rais Samia akamtuma Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba kwenda Marekani kuwapigia magoti MCC warejeshe misaada yao kwa Tanzania. Tayari MCC wameridhia ombi hilo. Hii ina maana Tanzania imetimiza masharti yanayohitajika iweze kunufaika na misaada kutoka shirika hilo.
*Serikali imechukua hatua za kuheshimu uhuru wa kujieleza na uhuru wa kujumuika katika utekelezwaji wa Sheria ya Uhalifu wa Mtandao.
*Serikali imeahidi kuendesha uchaguzi ulio huru na haki kwa Tanzania Bara na Zanzibar na ambao utashirikisha watu wote na kuakisi maoni ya wote.
*Vyama vya siasa vimeachwa vifanye mikutano ya ndani na nje yakiwemo maandamano bila ukomo wala kuvurugwa na vyombo vya ulinzi na usalama. Kwamba kutakuwa na demokrasia na kujitolea kwa nchi kufanikisha uchaguzi huru na wa haki.
*Kesi zote za mchongo dhidi ya wapinzani, ikiwemo ya ugaidi dhidi ya mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe zimefutwa na wapinzani waliokimbia nchi, akiwemo Tundu Lissu wamerejea. Halafu yakaanzishwa maridhiano kati ya CCM na Chadema.
Mazingira hayo ndiyo yamewezesha, Februari mwaka huu, Naibu Afisa Mtendaji Mkuu wake, Chidi Blyeden kuongoza ujumbe wa MCC kuja nchini kukutana na mafiasa wa serikali.
Waziri wa Fedha, Dk. Mwigulu aliishukuru Marekani kupitia MCC kwa kuiteua Tanzania kuwa moja ya nchi zilizoko kwenye mpango wa kunufaika na ruzuku zinazolenga kusaidia mageuzi ya kisera na kitaasisi ili kutatua vikwazo vya ukuaji uchumi.
Dk. Mwigulu aliueleza ujumbe huo kuwa Tanzania imepiga hatua kubwa katika kusimamia uchumi wake, masuala ya utawala bora, haki za binadamu, demokrasia, na kwamba imetekeleza kwa kiwango kikubwa vigezo vilivyowekwa na Shirika hilo ili nchi iweze kunufaika na mpango huo.
“Mheshimiwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, ameituliza nchi kisiasa, na kuwa na nia ya dhati ya kuituliza nchi kwa kuruhusu masuala ya kisiasa kufanyika kwa uwazi na hata hii si tu kwa ajili ya kutekeleza vigezo vya taasisi yoyote bali ni nia yake ya dhati ya kulinda uhuru wa watu,” alisema Dk. Mwigulu.
Hatua hii imefikiwa baada ya Desemba 2023, Bodi ya MCC, kuzichagua Tanzania na Ufilipino, kama wabia wake katika kuandaa programu za awali (threshold programs) zitakazolenga katika mageuzi ya kisera na kitaasisi ambazo nchi hizi zinaweza kuyafanya ili kupunguza umasikini na kuchochea ukuaji wa uchumi.
Bodi hiyo ya MCC ilichukua uamuzi huo baada ya Tanzania na Ufilipino, kuonesha dhamira mpya ya kusukuma mbele mageuzi muhimu ya kuimarisha utawala wa kidemokrasia, kulinda haki za binadamu na kupambana na rushwa.
Kwa kuwa Tanzania imejifunga MCC, Chidi Blyeden, aliipongeza Tanzania kwa hatua kubwa ilizopiga katika kuimarisha masuala ya utawala bora, demokrasia na haki za binadamu chini ya utawala wa Rais Samia, hatua iliyolifanya Shirika lake kurejesha ushirikiano na Serikali.