Faida na hasara upasuaji wa ganzi na usingizi kwa mjamzito

Dar es Salaam. Wakati ambao tafiti zinaonyesha kuwapo kwa ongezeko la wanawake wanaojifungua kwa upasuaji nchini katika mwaka 2022, umewahi kujiuliza njia ipi ni nzuri kutumia kuondoa maumivu wakati wa upasuaji?

Hiyo nikiwa na maana umewahi kufikiria njia ipi ni salama kutumia ili kuzuia kusikia maumivu wakati wa upasuaji kati ya sindano ya usingizi (nusu kaputi) na sindano ya ganzi mgongoni inayofanya baadhi ya sehemu katika mwili wako usisikie maumivu na wewe kuendelea kuzungumza.

Kwa mujibu wa wataalamu wa afya, mgonjwa anayo haki ya kuchagua njia gani itumike wakati wa kufanyiwa upasuaji, lakini wakati mwingine hali aliyonayo hufanya wataalamu kuamua nini watumie ili awe salama yeye pamoja na mtoto.

Wataalamu wanabainisha, kuna aina ya njia haifai kutumika, hasa mama mjamzito akiwa ametoka damu nyingi.

Akizungumza na Mwananchi, Daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake na uzazi, Dk Isaya Mhando anasema licha ya kuwa mama mzazi anatakiwa kuchagua njia ya kutumia, wakati mwingine hali aliyonayo huweza kufanya wataalamu kujua njia ipi ni salama.

“Mama akitoa damu nyingi ni ngumu kutumia sindano ya kuchoma mgongoni na badala yake hupewa nusu kaputi kwa sababu akichomwa sindano ya mgongoni shinikizo la damu hushuka kwa kiasi,” anasema Dk Mhando.

Anasema wanalazimika kutumia nusu kaputi, ili kupunguza athari kwa sababu shinikizo la damu likishuka mtoto ndani hushindwa kupumua vizuri.

Hata hivyo, alisema sindano ya ganzi mgongoni ni nzuri na ndiyo hutumika mara kwa mara, isipokuwa katika sababu maalumu. “Haishushi shinikizo la damu kwa mtu anayetakiwa kufanyiwa upasuaji,” anasema Dk Mhando.

Anasema matumizi ya nusu kaputi katika upasuaji huhitaji daktari mwepesi anayeweza kumtoa mtoto ndani ya dakika mbili, kwani bila kufanya hivyo mtoto huweza kunywa dawa alizochomwa mama.

“Mtoto akinywa dawa hupewa maksi ndogo, katika kuzalisha mama ndiyo kunaonyesha maisha ya mtu yatakavyokuwa baadaye, ni sawa na mtoto anapolia mapema, anabadilika kutoka maisha ya tumboni kwenda maisha ya kawaida.

“Anapokuwa tumboni damu haiendi kwenye mapafu na anapozaliwa na kulia huruhusu damu kuingia katika mapafu na kuruhusu oksijeni iingie katika ubongo,” anasema Dk Mhando.

Anasema matumizi ya sindano ya ganzi mgongoni ni mazuri, huku akieleza kuwa kabla ya njia hiyo kutumika mama huwekewe dripu za maji kama lita mbili.

“Athari zake, upasuaji ukimalizika ukanyanyua kichwa mapema, utapata maumivu ya kichwa na maumivu ya mgongo ambayo hutibika akienda hospitali, kwani ni ya muda mfupi.”

Pia kama dawa itapanda kifuani inaweza kufanya msuli wa kukusaidia kupumua kupooza, hii inaweza kuondoshwa kwa mtaalamu wa upasuaji kukuwekea mashine ya kukusaidia kupumua. Wakati yeye akiyasema hayo, Dk Paul Masua kupitia ukurasa wake wa Instagram anasema ni haki ya mgonjwa mwenyewe kuamua atumie njia ipi baada ya kuelezwa faida na hasara za kila njia.

Anasema sindano ya ganzi mgongoni ina faida nyingi ukilinganisha na ile dawa ya usingizi, huku akitaja moja ya faida ni kupunguza hatari ya damu kuganda. “Kwa kawaida wanawake wajawazito huwa wako kwenye hatari kubwa ya damu kuganda, faida nyingine ni kwamba unakuwa uko na fahamu zako,” anasema Dk Paul. Anataja tofauti na mgonjwa anapopewa dawa za usingizi, madaktari huwa wanamuweka kwenye mashine ya kupumulia, akiwa na maana kuwa njia hiyo inahitaji mgonjwa awekewe mpira wa kupumulia mdomoni ambao unaingia kwenye njia ya hewa.
 

Daktari bingwa wa kinamama, Cyrill Masawe anasema hakuna tabia zinazoweza kufanywa na mama mjamzito zinazomuweka katika hatari ya kujifungua kwa upasuaji na badala yake mabadiliko yanayokuwepo katika ujauzito.

Anasema mama akipata uchungu kuna vigezo huangaliwa, ikiwamo uchungu kuendelea kama unavyotakiwa na mtoto kushuka. “Kama kuna tatizo kuhusu mama au mtoto hushauriwa upasuaji ufanyike, wakati mwingine upasuaji hufanyika kama njia ya dharura kwa mjamzito kama ana shinikizo la damu ili kumuepusha na kifafa cha mimba au kutoka damu nyingi.

Wakati daktari akiyaeleza hayo, Zaituni Mussa anasema alipotakiwa kufanyiwa upasuaji, daktari aliwapa uhuru wa kuchagua njia ya kuzuia maumivu yeye na mumewe.

“Tuliambiwa njia zote, tatizo zote nilikuwa nimeshazisikia sifa zake mitaani, mwisho wa siku tulitolewa hofu na kuambiwa ipi ni salama zaidi na tulikubaliana na mwenzangu nikatumia.”anasema Zaituni.

Maneno yake yanaungwa mkono na Jane Msaki anayesema, maneno yanayosemwa mitaani kuhusu uzazi huwapa hofu kabla ya kufika hospitalini lakini elimu wanayopewa na madaktari huwatuliza.

Ufafanuzi unaonyesha kuwa ni asilimia nne pekee ya wanawake wasiokuwa na elimu na waishio katika kipato cha chini ndiyo wanatumia njia ya upasuaji wakati wa kujifungua ikilinganishwa na asilimia 20 ya wanawake wenye elimu na asilimia 24 ya wanawake wenye kipato fulani.

Ripoti hiyo pia inaeleza kuwa, kiwango cha wanawake kujifungua kwa njia ya upasuaji ni kikubwa zaidi katika hosptali za binafsi kwa asilimia 30, ikifuatiwa na hospitali za dini kwa asilimia 28 huku vituo vya kutolea huduma vya umma vikiwa na asilimia 12.

Related Posts