Kumekucha…! Yanga yatorosha beki mkongo, yampa miwili

NI rasmi sasa kwamba beki Mkongomani Chadrack Boka ni mali ya Yanga. Mwanaspoti limejiridhisha kwamba staa huyo amesainishwa mkataba wa awali wa miaka miwili mjini Lubumbasha, juzi.

Kama hilo halitoshi, Yanga imemtorosha kwa kumuondoa mchezaji huyo Lubumbashi na kumhamishia Kinshasa ili kumuepusha na rabsha za mashabiki wa FC Lupopo ambao kuna hofu kwamba huenda wakamfanyia vimbwanga kama wakisikia taarifa za kutaka kuondoka klabuni kwao.

Ujio wa Boka ni rasmi unafunga ukurasa wa Mkongomani mwenzake mkongwe Lomalisa Mutambala, ambaye licha ya mkataba wake kumalizika mwisho wa msimu huu, Yanga haikuwa na hesabu za kuendelea naye kutokana na kutokuwa na msimu mzuri  uliosababishwa na majeraha yaliyomfanya kukosa mechi muhimu zikiwamo za Simba (Ligi Kuu) na AL Ahly (Ligi ya Mabingwa Afrika).

Habari za uhakika zinasema Boka amekuwa na mchango mkubwa kwenye timu hiyo na ni kipenzi cha mashabiki, hivyo viongozi wamewashauri Yanga kumpa hifadhi Kinshasa wakati akijiandaa kwenda Dar es Salaam kumalizia hatua zingine.

Boka amesaini mkataba huo baada ya mvutano wa maslahi kati ya Yanga na FC Lupopo kumalizika kisha beki huyo kuruhusiwa kumalizana na mabingwa hao wa Ligi Kuu Bara msimu huu.

Licha ya Lupopo mabosi wake wa juu kuja nchini wakiongozwa na rais wa klabu, bilionea Jacques Kyabula Katwe na Yanga kutumia ujio wake na kuzungumzia dili hilo, lakini muafaka haukupatikana.

Baada ya hatua hiyo taarifa kutoka DR Congo zinasema Yanga ilimtuma tena mmoja wa maofisa wake kwenda kuonana tena na mabosi wa Lupopo, achilia mbali safari ya rais wa Yanga, injinia Hersi Said aliyetua nchini humo hapo awali.

Makubaliano ya klabu hizo mbili yaliipa nafasi Yanga kumalizana na Boka kisha kusaini mkataba huo juzi na baada ya kusaini tu akatoroshwa.

Katibu Mkuu wa Lupopo, Donat Mulongoy, ambaye licha ya kugoma kuthibitisha moja kwa moja aliliambia Mwanaspoti kuwa: ”Tumefikia sehemu nzuri lakini Lupopo tutatangaza baadaye.”

Mwanaspoti linajua katika dili hilo Lupopo iliitaka Yanga iweke mezani Dola 100,000 (takriban Sh260 milioni) ili kununua mkataba wa mchezaji huyo ambao ulibakiza mwaka mmoja.

Mwanzoni mwa miaka ya 2000 iliwahi kuwauzia mastaa Patrick Katalay, Pitchou Kongo na Alou Kiwanuka ambao walitamba kwa miaka kadhaa.

Akizungumza na Mwanaspoti, beki wa Lubumbashi Sports ya DR Congo, Mtanzania Abdallah Shaibu ‘Ninja’ aliwaambia Yanga kwamba: “Endapo atafanikiwa kusaini Yanga itakuwa imepata beki atayewasaidia kuongeza nguvu safu ya mabeki. Ukiachana na ubora wake wa kupiga krosi anajitolea kwa timu.”

 “Wakati tumecheza nao muda wote alikuwa anapambana na ana uwezo wa kuwasababisha timu ifanye makosa ambayo yanawapa faulo.”

Kwa upande wake, mshambuliaji wa FC Lupopo, George Mpole aliyecheza na Boka alisema kitu kikubwa alichokiona kwake ni nidhamu ya kazi kuanzia mazoezini hadi wakati wa mechi. “Nikimzungumzia uwanjani kama kweli Yanga itamsajili itakuwa imepata beki ambaye ana uwezo wa kupiga krosi, kukaba na kushambulia. Jamaa ana nguvu na kasi. Nimeona hilo tukiwa tunafanya mazoezi, kwani haogopi kujaribu kufanya majukumu mbalimbali uwanjani. Ukabaji wake anakukaba kama vile mnacheza na wapinzani na ndio kitu anachokuwa anakwenda kukifanya wakati wa mechi,” alisema Mpole mfungaji bora wa Ligi Kuu Bara msimu wa 2021/22.

Related Posts