Majaliwa atoa muda kwa halmashauri kuanzisha madawati ya sayansi

Tanga. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amezitaka halmashauri zote nchini ifikapo Julai, 2025 ziwe zimekamilisha uanzishwaji wa madawati ya sayansi, teknolojia na ubunifu.

Pia ameagiza masuala hayo yawe sehemu ya mipango ya halmashauri na kutengewa bajeti kila mwaka ili kuhudumia vijana wanaojishughulisha na ubunifu.

Kwa kufanya hivyo, amesema kutasaidia uimarisha uwezo wa nchi katika utafiti, matumizi ya sayansi, teknolojia na ubunifu.

Waziri Mkuu Majaliwa amesema hayo leo Mei 31, 2024 katika maadhimisho ya kilele cha Wiki ya Kitaifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu 2024, katika viwanja vya Shule ya Sekondari Popatlal jijini Tanga.

Maadhimisho hayo ni sehemu ya mikakati ya Serikali ya kuongeza hamasa ya kukuza elimu, ujuzi na matumizi ya sayansi, teknolojia na ubunifu.

Mbali na hayo, ameagiza Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na Ofisi ya Rais Tamisemi, zihakikishe kuwa ifikapo Julai 2025 shule zote za msingi, sekondari, vyuo vya ualimu na vyuo vya maendeleo ya wananchi viwe vimeanzisha majukwaa ya sayansi, teknolojia na ubunifu.

Kwa mujibu wa Majaliwa, Serikali inaendeleza bunifu 283 zilizotokana na Mashindano ya Kitaifa ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu (Makisatu).

Waziri Mkuu amesema bunifu 42 kati ya hizo zimeshaingia sokoni na zimewezesha kuanzishwa kampuni 94.

Amesema bunifu na teknolojia zilizoanzisha kampuni hizo zimebuniwa na wabunifu wa Kitanzania.

“Nitoe wito kwa wabunifu nchini, mmebuni kazi na kazi hizo zina matokeo, jipangeni kuboresha kazi zenu, fungueni kampuni na mtangaze biadhaa hizo,” amesema.

Majaliwa amesema Serikali imeanzisha vituo vya umahiri 12 katika Taasisi za Elimu ya Juu na Taasisi za Utafiti na Maendeleo kwa lengo la kuchagia utafiti na ubunifu.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda amesema Profesa Mkenda alisema Serikali inaendelea kuwabeba wabunifu waliogundua na kubuni vifaa mbalimbali, kuwatafutia soko ili wapate ajira.

Pia amesema wizara inaendelea na hatua mbalimbali zinazolenga kuimarisha fursa na ubora wa elimu kwa kutumia Tehama na teknolojia nyingine za kufundishia na kujifunzia.

Alizitaja hatua hizo kuwa ni pamoja na mkakati wa Taifa juu ya matumizi ya teknolojia za kidijitali katika elimu, utoaji wa mafunzo kabilishi kwa walimu, na mradi wa ‘Smartwasomi’ utakaojumuisha kuanzisha madarasa janja yanayotoa fursa ya kufundisha wanafunzi katika maeneo tofauti kwa wakati mmoja.

Mwenyekiti wa Kamati ya  Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo, Husna Sekiboko amesema Serikali iangalie jinsi ya kuzitumia bunifu zilizoonyeshwa, kwani zinatakiwa kutumika na kuleta faida kwenye jamii na siyo katika maonyesho pekee.

Amesema kila taasisi na mamlaka ambayo kuna bunifu inawagusa, waichukue na kuangalia utaratibu wa kuitumia ili kuleta faida kwenye jamii na bunifu husika kuwa na tija.

Mkuu wa Mkoa wa Tanga,  Balozi Batilda Burian ameiomba Serikali kuhakikisha Mkoa wa Tanga unapata chuo kikuu kwani kipo kimoja huria na ahadi moja ya kuwepo tawi la Chuo cha Mzumbe.

Kuhusu vyuo vya ufundi amesema kila wilaya inacho, hivyo suala la kuendeleza vipaji na bunifu zinaendelea, lengo ni vijana kujiendeleza.

Mshiriki wa maadhimisho hayo, Msajili Msaidizi wa Chuo Kikuu cha The Aga Khan, Agath Damas ameipongeza Serikali kwa maadhimisho hayo, akishauri nguvu iwekwe katika kuhamasisha wanafunzi kupenda masomo ya sayansi.

Amesema kwa kufanya hivyo itasaidia kuongeza idadi ya wataalamu hao nchini.

Ameeleza watoto wengi wamekuwa na woga wa masomo ya sayansi, hivyo upo umuhimu wa kuwashauri umuhimu wake katika jamii.

Related Posts